Ifahamu Misingi ya Kusifu na Kuabudu
IFAHAMU MISINGI YA SIFA NA KUABUDU KATIKA ROHO NA KWELI KAMA BIBLIA FUNDISHAVYO UNDERSTAND THE BIBLICAL BASIC PRINCIPLES OF WORSHIP IN SPIRIT AND IN TRUTH.
IFAHAMU MISINGI YA SIFA, IBADA NA KUABUDU KATIKA ROHO NA KWELI KAMA BIBLIA IFUNDISHAVYO
Kitabu hiki kimeandikwa Na Mch. Absolom O. Mwalubalile
S. L. P 61012, Dar es Salaam –Tanzania
Tel: +255 718 806 840, +255 784 251 041
E-mail: [email protected]
Kitabu hiki kinatoa maelekezo muhimu kwa mwamini jinsi ya kumkaribia Mungu katika ibada ya Kiroho, na njia mbalimbali za kumwabudu Mungu, kwa mujibu wa Biblia, na mafundisho yenye ufafanuzi wa kimaandiko pamoja na elimu ya matumizi ya mwili katika kuabudu, kuijua sauti nakuwa mwimbaji bora wa kwaya, sifa na muziki. Ningependa viongozi wa kanisa wakisome na kukitumia katika huduma zao Makanisani
HATIMILIKI © copyright
ABSOLOM OBED MWALUBALILE
WAKATI WA IBADA NI WAKATI WA KILELE CHA FURAHA
YA MWANADAMU
IBADA NA KUABUDU NI KUMSHANGAA MUNGU
AMBAYE NI MFALME WA AJABU MILELE
YOH 4:23-24
BABA ANAMTAFUTA MTU ATAKAYEMWABUDU
KATIKA ROHO NA KWELI
IFAHAMU MISINGI YA SIFA,
IBADA NA KUABUDU KATIKA ROHO NA KWELI KAMA
BIBLIA IFUNDISHAVYO
SHUKRANI
Napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuandika kitabu hiki kuhusu ibada. Naamini kwamba bila ya himizo la Roho Mtakatifu ndani yangu nisingeweza kukamilisha kazi hii.
Ni matumaini yangu kwamba kila atakayesoma atapata msaada na kukua kiroho.
Natoa shukrani za dhati kwa mke wangu mpenzi Feda A. Mwalubalile, ambaye kwa miaka mingi ya utumishi wetu kwa Mungu aligundua na kuliona jambo hili kwangu na kunipa ushauri wa kuandika kitabu juu ya sifa, ibada na kuabudu na kuchochea maono haya. Mungu ambariki, kwa uvumilivu na kwa maombi yake. Nawashukuru watoto wangu kwa kunitia moyo, natoa shukrani maalumu kwa, Nikusuma A. Mwalubalile kwa kujitoa kwake katika kuchapisha kitabu hiki mpaka hatua ya mwisho.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba na Ushirika wa Roho Mtakatifu, ukae nasi sote, sasa na hata milele.
Baraka na Amani ya Mungu viwe juu ya kila mtu asomaye kitabu hiki.
Absolom O. Mwalubalile
YALIYOMO
SURA YA KWANZA
CHIMBUKO LA IBADA YA MWANADAMU
a) Chimbuko
b) Kuabudu
c) Kusifu
d) Ibada
SURA YA PILI
IBADA NA UIMBAJI
a) Uimbaji ndani ya ibada
b) Nyimbo na aina ya Ibada
SURA YA TATU
HUDUMA YA MUZIKI KATIKA SIFA NA KUABUDU
a) Muziki
b) Ufunguo wa kuabudu
c) Vidokezo
d) Uimbaji kitaaluma
e) Sifa za mwimbaji
SURA YA NNE
SIFA, KUABUDU, NA MAANDALIZI YA IBADA
a) Kwa nini ibada ni lazima
b) Maandalizi ya ibada
c) Nafasi ya mchungaji
d) Kiongozi wa ibada
e) Vigezo vya kuongozea nyimbo
SURA YA TANO
FAIDA ZA KUABUDU
SURA YA SITA
UMUHIMU WA MWILI KATIKA KUABUDU
a) Matumizi ya mwili
b) Kazi ya Roho Mtakatifu
c) Mwili wa Yesu
d) Mwili wa mwamini
SURA YA SABA
MATUMIZI YA MWILI KATIKA KUABUDU
SURA YA NANE
BIBILIA – MWONGOZO WA IBADA
a) Mchakato wa mifano
b) Mambo muhimu kufahamu
SURA YA TISA
ZANA ZA MUZIKI KATIKA SIFA NA IBADA
a) Uchunguzi katika maandiko
b) Angalizo kwa wana muziki
SURA YA KUMI
NAFASI YA KWAYA KATIKA IBADA
a) Kwaya ni njema
b) Angalizo kwa mwana kwaya
SURA YA KUMI NA MOJA
KANISA NA KIZAZI KIPYA
a) Njia panda
b) Mabadiliko
SURA YA KUMI NA MBILI
SIKU TEULE YA IBADA TAKATIFU
a] Mwanzo wa siku ya Bwana
b] Siku ya Bwana
c] Jinsi siku hiyo ilivyo anza
d] Sabato ikafanywa amri
e] Umuhimu wa siku ya Bwana
f] Kuishika sabato ni lazima
g] Siku ya Bwana Jumapili
h] Siku hii hajatanguliwa
i] Utii mkamilifu kwa Yesu
j] Jumapili ni siku ya utakatifu wa Bwana
SURA YA KUMI NA TATU
ZABURI NA NYIMBO
a] Nyimbo
b] Zaburi
DIBAJI Mungu ameweka mzigo moyoni mwangu wa kutaka kumfanyia Mungu ibada inayompendeza, jambo hili limekuwa mzigo moyoni mwangu na kunipa hamu kubwa kiasi shauku yangu ni kuona mwili mzima wa Kristo (Kanisa) unaelewa ibada ya kweli katika Roho mbele za Mungu ni nini na hufanywa kwa jinsi gain.
Katika uchunguzi nilioufanya nimegundua wakristo hawana uelewa sahihi juu ya ibada ambayo inapaswa kufanywa na mwanadamu kwa Muumba wake. Ukosefu huu wa ufahamu unawanyima haki yao ya kiroho katika kufurahia uzuri wa kuabudu na kufahamu neema ya kumjua Mungu katika uhalisi wake unaopatikana katika sifa na kuabudu.
Pengo hili lisipozibwa, mkristo anayeabudu hatamgusa Mungu na hivyo kupelekea ibada yake kuwa tupu, ingawa ana nia njema ya kumwabudu Mungu, lakini amekosa maarifa ya jinsi anavyopaswa kuabudu.
Mungu ni Roho na mwanadamu naye ana Roho, ni katika ibada ya rohoni atamwabudu. Yoh 4:24 Mungu anamtafuta mtu atakayemwabudu katika Roho na kweli, kila mtu mwenye kiu ya kweli anakaribishwa kuabudu katika Roho. Ningependa ufuatilie kwa makini fundisho la sifa na kuabudu katika haki, ili ufahamu mambo ya msingi kuhusu kuabudu.
Inasemekana kwamba ibada ni sanaa iliyopotea na kusahaulika kwasababu watu wameshindwa kujituma na kuzama katika kumtafuta Mungu kama neno linavyomfunua na kuishia kufanya chochote kinachouridhisha moyo kwamba ni kumwabudu, jambo ambalo si sahihi. Mungu haabudiwi kama mtu anavyotaka, bali anaabudiwa kwa utaratibu anaoutaka yeye na uliomo ndani ya neno lake. Nakusihi ufuatane nami hatua kwa hatua ukitafakari yale usomayo na kuyaweka katika vitendo, bila shaka mfumo wako wa ibada utabadilika na utahisi chemchem na bubujiko la Roho Mtakatifu moyoni mwako. Kanisa la Kristo kwa ujumla wake litakapofanya ibada katika Roho na Kweli, mapinduzi makubwa yatatokea ndani ya kanisa, katika ulimwengu wa Roho, na katika ulimwengu wa mwili. Maana hili ndilo kusudi la Mungu kuwa na ushirika na mwanadamu. Ushirika wetu na Mungu katika ibada ni mwanzo wa ushirika tutakaokuwa nao milele na Mungu.
MCH. A. O. MWALUBALILE
Rev. Absolom Obed Mwalubalile ni mume wa mke mmoja na familia ya watoto saba. Kwa muda wa miaka 40 amekuwa akimtumikia Mungu katika nafasi mbalimbali ndani ya kanisa la mahali pamoja.
Wito wake na huduma yake ni sifa na ibada, kama kiongozi wa sifa na kuabudu, huduma hii ameifanya kwa miaka 26 katika makanisa mbalimbali ya kiroho katika jiji la Dar es salaam, na sehemu zingine za nchi .
Ameendesha semina za sifa na kuabudu na mafundisho ya uimbaji wa kwaya nyingi hapa nchini na kuhusika sana na mabadiliko ya kwaya yaliyopo sasa hapa Tanzania.
Amekuwa mwalimu wa kwaya kanisani kwake, na kuongozi kwaya kubwa yenye waimbaji 350 kwa huduma za mikutano mikubwa ya injili jijini Dar sa salaam.Pia Mungu anamtumia katika huduma za kiinjilisti nchini na nje ya nchi. Ni mwalimu wa shule ya Biblia. Chuo Enezi na Chuo cha Biblia cha K. A. Paulo Dar es salaam
Anaendesha semina za Neno la Mungu katika makanisa mbalimbali, na kwa sasa anafanya huduma na kanisa kama Mchungaji hapa Dar es salaam. Ana Shahada ya kwanza ya Bible and Theology kutoka Chuo Kikuu cha Global University USA.
Wito wake kwa Kanisa la Kristo ni kuwataka waamini waijue ibada ya Kiroho na ya Kweli yenye upako wa Roho Mtakatifu. Ambapo waabuduo watamwabudu Mungu katika Roho na Kweli, na kurejesha maana ya sifa, ibada na kuabudu kulikopotea hekaluni mwa Bwana. Ibada ya kweli italeta furaha ya Roho Mtakatifu maishani mwa waamini na kurejesha tumaini la utukufu mioyoni mwao maana tayari wameona uwepo wa Mungu katikati yao, kisha kujenga imani zao, na shauku yao kwenda kuwa pamoja na Bwana Mbinguni.
SURA YA KWANZA
CHIMBUKO LA IBADA YA MWANADAMU
1.Chimbuko la Ibada ya mwanadamu katika Biblia:
Chimbuko
Kusudi la Mungu kumuumba mwanadamu ni USHIRIKA (FELLOWSHIP) Mwanzo 1:26-27, 2:7, 21:-25, 3:8-10 Katika ushirika huo ndiko tunapata chimbuko la ibada ya mwanadamu. Mungu hawezi kufanya Ushirika na mwanadamu katika asili ya mwili moja kwa moja maana yeye ni ROHO, kwahiyo Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake, na mfano huo ni katika ROHO.
Ushirika wetu na Mungu uko katika ROHO, na kwa Roho tunafanana na Mungu. Mwanzo 2:7. Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi yenye uhai, mtu akawa nafsi hai. Mwili ni jengo au makao, hema, na kifuniko cha Roho ambayo ni pumzi yenye uhai, ili kwa huyo Roho Mungu ajidhihirishe kwa ulimwengu katika ufahamu wetu. Yaani mwili ambao ni mavumbi. Katika msingi huo kusudi la Mungu kutuumba linatimia. Yapo makusudi makuu mawili ambayo ni:- Kumtumikia na Kumwabudu. Mwanadamu awaye yote asiyefanya mambo hayo mawili amekosea lengo na kusudi la asili ya kuumbwa kwake. Katika mambo haya mawili, wajibu wa kwanza ni kuabudu, yule unayemwabudu hatimaye unamtumikia na kuyakubali matakwa yake kwa kumtumikia. Wajibu wa kwanza wa Adamu ulikuwa ni kuabudu na siyo kuhubiri ama kufanya huduma zingine, Mungu alikuja katika ibada wakati wa jua kupunga jioni ili kufanya ushirika nao, kuhubiri neno ni matokeo ya anguko la Adamu kumuasi Mungu na kuacha wajibu wake wa ibada na Mungu. Msingi mkuu wa mahusiano ni Ibada.Mw 3.8 unasema wakasikia sauti ya Mungu akitembea bustanini . Hii inaonyesha kwamba Adamu alikuwa na ushirika na MUNGU kiasi cha kuzijua hatua za MUNGU alivyotembea ikiwa ni ushahidi wakutosha kwamba walikua na ushirika mzuri.
2. KUABUDU:- ASILI YAKE
Kuabudu asili yake ni mbinguni, kuabudu kulikuwepo kabla ya Adamu kuumbwa. Maana walikuwepo viumbe kabla ya Adamu huko mbinguni waliomwabudu Mungu. Ibada ina asili katika Mungu mwenyewe, Uungu una asili ya kuabudiwa kwa hiyo chanzo cha ibada ni Mungu. Ayubu 38:4-7, Zaburi 148:2-14. Hapa tunaona malaika wanamwabudu na kumsifu Mungu. Mstari wa 5 zaburi 148 unaonyesha agizo la Mungu akiagiza viumbe vyote kumwabudu na kumsifu kutoka mbinguni mpaka duniani kuanzia viumbe vyenye uhai na visivyo na uhai kama ifuatavyo:-
a) Malaika na jeshi lake
b) Jua , mwezi na nyota zote
c) Mbingu na maji ya mbingu
d) Ms. 5 viumbe visivyoonekana
e) Nchi yaani uumbaji wake wa dunia
f) Samaki wa baharini
g) Moto, mvua , theluji na mvuke, upepo na dhoruba
h) Milima, na miti , wanyama wa porini na wa kufugwa
i) Wadudu na ndege wa angani
j) Wafalme na watu wakubwa kwa wadogo wazee na watoto
Hawa wote wanaamuriwa kulisifu Jina la Bwana, Jina Pekee lililotukuka lenye adhama juu ya mbingu na nchi. Hii ni amri ya milele ambayo haitapita.
Midundo ya shangwe za malaika na mirindimo ya ibada hiyo ikaijaza mbingu wakati Mungu alipoumba ulimwengu. Malaika waliimba na kushangilia kazi ya uumbaji. Imekuwa ni shauku ya Mungu kutaka ushirika huu wa ibada na viumbe vyake alivyoviumba, tangu hapo na mpaka milele katika mbingu mpya na nchi mpya, ambayo ni masikani yake pamoja na mwanadamu. Uf. 21:3
Jambo hili linafunuliwa na kufafanuliwa kwa ufasaha na Yesu alipomwambia mwanamke msamaria pale kisimani “Lakini saa inakuja nayo sasa ipo ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika Roho na kweli” kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu, Mungu ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na Kweli. Yohana 4:23-24. Mungu anamtafuta mtu atakayemwabudu – kwanini? kwasababu anataka ushirika na mwanadamu Ili aufurahiye Upendo wa mwanadamu aliyemuumba kwa mfano wake na kutimiza kusudi lake la USHIRIKA.
Kuabudu katika Roho na Kweli huo ndiyo ushirika ambao Mungu anautafuta. Kwa kuwa Jawabu la moyo wa Mwanadamu ni ushirika ambao unamgusa Mungu na kumtukuza Mungu kwa roho yake yote na kumfurahia pasipokuwa na kitu kingine zaidi ya Mungu moyoni mwake na kufanya uamuzi huo kuwa jambo la milele. Ibada siyo kitu cha muda mfupi bali ni shughuri inayo endelea milele na milele kati ya mwanadamu na Mungu.Luka 1:46-47
3. KUABUDU NI HISIA ZA UPENDO MKUU
Kuabudu kunahusisha hisia kali zenye upendo mkuu zinazogusa ufahamu na kuzama katika upendo wa ndani kabisa na kuhusudu. (Adoration) Kuhusudu ni mguso ambao unaachilia hisia za papo kwa hapo, na kusema kwa sauti ya kusikika maneno yenye kujaa mlipuko wa upendo mkuu, na kwa sauti ya upole na kugugumiza maneno, pamoja na ubembelezi mwingi, ukiambatana na maombi yaliyojaa unyenyekevu, heshima , adabu, na hofu na kijikita katika ibada ya dhati mbele ya Mungu, kumsifu na kumwabudu.
4. KUABUDU: MAANA YAKE
Ni tendo linalogusa akili , hisia, nafsi na utu wa mtu na mwili pia kwa kusujudu, kuanguka kifudifudi, au uso kwa uso. Mw. 17:3 Tendo hili linafanywa pasipo ushawishi wa kitu, wala si nje ya Moyo wa kumtambua Mungu kuwa wa thamani kuliko kitu chochote anayestahili kupewa ibada ya pekee na kupelekea kujitoa kwake bila unafiki wala ubinafsi. Ni dhana zaidi ya ufahamu wetu, taratibu, desturi na mipango ya ibada, ni ibada inayojumuisha utu wako mzima na kuwasha moto katika mawazo, fikra na hisia zako zote, kiasi cha kuhisi unampapasa na kumwona Mungu katika Roho na kuwa halisi.1Yoh1.1-2,Lile lililokuako tangu mwanzo tulilolisikia ,tuliloliona na macho yetu tulilolitazama,na mikono yetu ikalipapasa kwa habari ya neno la uzima.na uzima huo ulidhihirika nasi tumeona tena twashuhudia huo uzima.Uhalisi huu unampeleka mtu kumwabudu MUNGU.
Angalizo:-
– Ibada lazima ifanywe katika roho. Hamasiko liwe la Roho Mtakatifu na siyo misisimko ya mwili na akili tu.
– Ibada ifanyike katika moyo wa dhati na wa kweli iliyofunuliwa na Yesu yaani sawasawa na NENO lake.
– Kuabudu nje ya Roho na kweli huko sio kuabudu ni kuabudu kitu kingine kama, kutafakari, sala zenye viwango Fulani, kuwa na idadi ya sala, mpangilio wa sala kwa kuhesabu shanga,kuchoma udi, maji maalum,ama kuvaa mavazi maalum na kujiweka katika muonekano Fulani, kumtumia mtu wa kati ili awakilishe maombi yako mbele za Yesu na Yesu ampelekee Mungu. Hayo si maana ya kuabudu.
5. KUABUDU NI UJUZI WA KIPEKEE
Wakati wa kuabudu ni wakati muhimu mno, ni wakati wa shughuli ya utukufu kupita zote ambazo mwanadamu anafanya katika maisha yake, wakati wa kuabudu unazidi nyakati zote anazoweza kuzifurahia, tena kuabudu huacha kumbukumbu ndani yake, kumbukumbu ya kuabudu inapita vilele vyote vya furaha hizo maana ni wakati wa kukutana na Mungu. Je mwanadamu ninani hata akapewa nafasi tukufu kama hiyo? Kwakuwa, kuabudu ni sehemu ya maisha na ushirika na Mungu na ni jambo la rohoni, basi, kuabudu kunakuwa sehemu ya kila jambo analofanya, na ni ufunguo wa maisha yenye mafanikio na mwelekeo wa fikra na mawazo ya moyo, na kuwa mtindo wa maisha
6. KUABUDU NA MAOMBI
Maombi ni njia kuu na bora zaidi ya kumsifu na kumwabudu Mungu. Maombi ni wakati ambao mtu anazungumza na Mungu mambo yake na kujimimina moyo wake mbele za Mungu. Katika maombi ya dhati na ya kweli, mtu hujiachia akawa wazi kujieleza na kutoa siri za moyo wake akijua Mungu ndiye msaada wake na kimbillio lake. Zab. 46:1-3
Kwa kutambua ukuu wa Mungu na uwezo wake ndipo ibada ya kweli toka vilindi vya moyo huanza, na mtu hushuka chini sana katika ufahamu wake kumtambua Mungu ninani na kumwabudu na kumpa sifa katika maombi. Katika hali hiyo ya maombi humfanya mtu ajione sikitu bali astahiliye ni Mungu, ndipo wengine huanguka chini na kugaragara kuonyesha upendo mbele za Mungu. Math 26: 39 Luka 22: 44, Ay 19: 25 -27
Hata malaika wanaabudu na kuanguka mbele za Mungu. Yesu naye aliabudu hata akalia na kutoa machozi ya damu akiomba. Ayubu aliomba na kujiachia mikononi mwa Mungu akisema, najua mtetezi wangu yu hai na pasipo mwili huu nitamwona Mungu. Maombi huvuka mipaka yamazingira ya mwili wa nyama na kumleta mtu mahali alipo Mungu katika Roho kiasi kwamba muombaji anakuwa na mazungumuzo na Mungu ana kwa ana kama Paulo asemavyo ABA yaani Baba aliye karibu naye kama mwana. War 8: 15
Maombi kama haya yanafanyika katika dhana ya kumtambua Mungu mwenyezi na ukuu wake, uweza wake, mamlaka na nguvu. Kisha moyo wa mtu huyu huzama ndani ya ibada kwa maombi na kumwabudu, na kumpa sifa yeye aliye juu Mungu mkuu.
Ufahamu huu unamfanya mtu amheshimu Mungu na kumwabudu kwa mshangao mkuu, na kumvuta kumpenda na kuichukia dhambi, kama Isaya asemavyo, Isaya 6:1-5 Mimi ni mtu mwenye midomo michafu na ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu. Petro naye anasema, Ondoka kwangu Bwana mimi ni mtu mwenye dhambi. Luka 5:8-9. Heshima hii kwa Mungu huona utukufu wa Mungu ulivyo mkuu na utakatifu wake ulivyo wa ajabu, na kushindwa kustahimili mbele ya Mungu kisha kusema maneno hayo ya unyenyekevu katika maombi.
7. KUSIFU – MAANA YAKE
A) SIFA,Ni neno linalotumika katika,kuinua , kuadhimisha na kutukuza kitu ,mtu, kwa heshima ya matendo aliyofanya .Sifa zetu ni kwa Mungu ,katika kumtukuza ,kumwinua na kumwadhimisha kwa matendo yake makuu aliyoyafanya katikati yetu.Biblia inatupa mifano mingi ya sifa kama ifuatavyo.
B) WALIOKOMBOLEWA TOKA DHIKI KUU YA MPINGA KRISTO
Sifa ni shughuli kuu mbinguni, angalia waliokombolewa kutoka katika dhiki kuu wanavyompa sifa Mungu. Ufunuo 15:2-4 Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kandokando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana Kondoo, wakisema, ni makuu na ya ajabu matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenye Enzi: ni za haki na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. Ni nani asiyekucha Ee Bwana na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako uu Mtakatifu: kwa maana mataifa yote yatakuja nakusujudu mbele zako kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.
C) SIFA ZA MFALME DAUDI
1Nyak 29.10-13 Pia Mfalme Daudi anatoa sifa za hali ya juu sana kwa Mungu Kwahiyo Daudi akamhimidi Bwana mbele za mkutano wote, naye Daudi akasema , Uhimidiwe ,Ee Mfalme baba yetu milele na milele,Ee Bwana ukuu ni wako , na uweza,na utukufu, na kushinda , na Enzi , maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako , ufalme ni wako,Ee Bwana ,nawe umetukuzwa , U, mkuu juu ya vitu vyote ,Utajiri na heshimahutoka kwako wewe ,nawe watawala juu ya vyote,na mkononi mwako mna kuwawezesha wote.
Sifa hizi zinatoka katika moyo wenye kuguswa na kazi za Mungu zinazo pita ufahamu wa mwanadamu kisha mwanadamu kumwinulia Mungu Sauti yenye kujaa maneno ya mshangao wa ukuu wa Mungu na kumimina maneno matukufu yenye kumpa sifa Mungu.
D) SIFA ZA WANA WA ISRAELI BAHARI YA SHAMU
Mfano mzuri wa sifa zenye maneno makuu kwa Mungu ,ni sifa za wa Wana Israeli walizompa Mungu kwa muujiza mkuu alioutenda kukausha bahari ya Shamu, na kuwavusha mpaka nga’mbo, na kuwaokoa na mkono wa mfalme Farao na jeshi lake lote likazama baharini .
KUT 15.1—21. Mistari ifuatayo inasema sifa hizo.Ms 1-12 Nitamwimbia Bwana kwa maana ametukuka sana,Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,Naye amekuwa wokovu wangu, Yeye ni Mungu wangu,nami nitamsifu,Bwana ni mtu wa vita,Bwana ndilo Jina lake,Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini,Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza,walizama vilindini kama jiwe, Bwana mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo.Bwana mkono wako wa kuume wawasetaseta adui ,kwa wingi wa ukuu wako wawangusha chini wanaokuondokea.Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa,Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu,Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari, Adui alisema nitafuatia nitapata nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao,Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawangamiza, Ulivuma kwa upepo wako bahari ikawafunikiza,Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu.Ee BWANA Katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe mtukufu katika utakatifu? Mwenye kuogopwa katika sifa zako,mfanya maajabu, Ulinyosha mkono wa kuume nchi ikawameza.Ms 17-18 Utawaingiza(ISRAELI) na kuwapanda katika mlima wa urithi wako,Maahali pale ulipojifanyia Ee Bwana ili upakae,Pale patakatifu ulipopaweka imara ,Bwana,kwa mikono yako.Bwana atatawala milele na milele.
Kusifu ni kumkubali Mungu katika uwezo wake na nguvu, adhama, ukuu, enzi na mamlaka, utukufu na heshima, katika kutenda kwake kusikokuwa na mfano wala mipaka, katika mambo yasiowezekana kwa kadiri ya asili yake ya Uungu ilivyo, na hivyo kuleta utoshelevu na kuridhika kwa ufahamu wetu, na kumpa sifa na kumwinua, kumheshimu na kumtambua alivyo wa thamani, mkuu na wa kutisha na alivyo mwema na wa kupendeza mzuri pasipo mfano.
Kusifu ni kumkubali Mungu bila shaka yoyote juu ya tabia zake kwamba Mungu ni wa haki, wa rehema na huruma zake ni za milele. Amejaa upendo, mwaminifu na wa kweli na habadiliki milele. Kusifu kunaweza kutafsiriwa kwa kina cha ufahamu wa mtu anavyoguswa na ukuu wa Mungu, na akajikuta analipuka kumpa sifa Mungu kwa viwango vyake kama tunavyoona katika Zaburi sifa zikitolewa na watakatifu wa kale, kufuatana na mapito yao jinsi Mungu alivyoingilia kimiujiza kuwaokoa na kuwaponya. Zaburi 130:3-4, 124:1-8, 46:1,136:1-36. Sifa za Mungu zinaonekana katika majina yake yanayowakilisha, ukuu wake, uweza, uponyaji, ulinzi, amani, uumbaji, utoaji, utukufu na nguvu zake kama vile, Yehovayire, Yehova Shama, Yehova Rafa, Yehova Shalom, Yehova Elishaddai, Yehova Nissi ,Zaburi 113—118 Ni Zaburi za Sifa za matendo makuu ya Mungu.
8. IBADA
Ni tendo la heshima ya hali ya juu linalofanywa na mtu kwa kiumbe aliye mkuu katika mazingira yake yote, kiroho na kimwili na kiumbe huyo akaaminiwa kuwa ni MWENYE ENZI asiyefananishwa na kiumbe kingine mkamilifu katika matendo yake.
Kuabudu Mungu katika Roho na Kweli kunaweza kukafanywa wakati wowote na mahali popote mradi lengo ni kumfanyia Mungu IBADA.Jambo la muhimu ni yule tunayemwabudu kuliko mahali tunapofanyia ibada ingawa mahali tunafanyia ibada ni kitu chema ,lakini pasipewe nafasi mioyoni mwetu na kuheshimiwa kama sehemu ya ibada.Pamoja na hoja hiyo mahali pa ibada pasipuzwe na kudharauliwa maana pamewekwa wakfu kwa huduma ya Mungu pametakaswa . Mtu akionyesha dharau au kuto paheshimu anaweza kupata madhara ,hivyo ni muhimu kila mtu ajue jambo hili na kuenenda kwa utaratibu na kwa heshima mahali hapo.
Kwa vile Ibada ni shughuli ambayo inashikamana sana na mfumo wa maisha ya mwanadamu, na kwamba ibada hutofautiana sana katika maana na mitazamo kulingana na imani ya mtu juu ya Mungu anayemwabudu, ni vema tukaelewa kwa usahihi ibada ninini kwa mujibu wa Biblia ifundishavyo.
Rum 12:1-2 Tendo la Ibada ni tendo la kujitoa kama dhabihu ,lakini ibada ya kweli lazima dhabihu hiyo iwe hai na takatifu,Mwili, Roho na ufahamu viwe na lengo moja lakumfanyia Mungu Ibada takatifu basi, ambapo ibada nje ya utakatifu si ibada inayompendeza .
IBADA – MAANA YAKE
Ibada ni kumshangaa Mungu. Kwa ufahamu tulio nao na akili ya kibinadamu tuliyo nayo hatuwezi kumwelewa Mungu kikamilifu tukamfahamu. Isaya 55:8-9: “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.” Mungu ni mkuu kuliko uwezo wa ufahamu wa mwanadamu na yuko juu sana kuliko mawazo ya mwanadamu na yuko juu sana kuliko njia za mwanadamu kwahiyo hatuwezi kumfahamu vyema” Hivyo basi siku zote tutakapokusanyika pamoja au mtu akiwa peke yake kumwabudu na kukutana naye atamshangaa (tutamshangaa). Hutaweza kukaa mbele za Mungu ukimwabudu katika Roho na Kweli ikawa jambo la kawaida, maana Mungu huyo ni Mfalme Mkuu lazima utamshangaa Mfalme huyo. Utukufu wake utakushangaza na kutamani kumwangalia.
Wafalme wa dunia japokuwa ni wanadamu, raia wao hutetemeka na kuwaheshimu wanapojitokeza mbele zao, na kila mtu hutamani kumwona na kumshangaa, na kukusanyika mahali pamoja ili wamsikilize Mfalme wao. Mungu ni Mfalme wa ajabu anayejihudhurisha kati ya watu wake wanapomfanyia ibada kwa kumwabudu na kuwashangaza waabuduo ambapo na wao wanazama katika mshangao. Zab. 47:7, 66:3, 68:35, 71:16, 89:7
9. IBADA INAYOKUBALIKA
Si kila Ibada inayofanywa na mwanadamu ni halali na kukubalika na Mungu,hapana .Mungu ni Mungu wa utaratibu na mipango mikamilifu.
Mungu amesema wazi ni ibada ipi anaikubali na kuipokea akaisikiliza. Lakini kwakuwa ulimwengu ni mpana na wenye tofauti za watu walio na itikadi tofauti na ibada za walimwengu pia ni tofauti. Mungu wa kweli ni mmoja na njia ni moja ya kumfikia ambayo ni Yesu. Yohana 14:1-6, ITim 2:15. Ni katika Yesu ambaye ni mpatanishi wetu na Mungu na ambaye ni kweli, njia na uzima tutasikilizwa na kukubaliwa,Yesu anasema mtu yeyote hawezi kwenda kwa Mungu isipokuwa kwa njia yake,hakuna njia ya mkato bali ni Yesu tu.
Kwahiyo ibada lazima iwe
a) Ibada katika Roho na Kweli yenye kumtambua Yesu kuwa kiini na mlengwa wa Ibada hiyo Mdo 4:11-12 Waef 2:4-8
b) Si ibada ya mdomoni wala makusanyiko ya kidini na taratibu za kibinadamu zilizobuniwa kwa umahiri na wala si mapokeo ya mila na desturi za watu. Mdo17:22-27
c) Ibada ambayo haimchanganyi Mungu aliyejifunua katika maandiko na miungu mingine, japokuwa miungu hiyo inaabudiwa na mamilioni ya watu pamoja na vitu vilivyotukuzwa kiasi cha kukubalika kuwa Mungu. Zab 115:4-8 Sanamu zao ni fedha na dhahabu, kazi ya mikono ya wanadmu. Zina vinywa lakini havisemi, zina macho lakini haioni. Zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazisikii harufu. Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, wala hazitoi sauti kwa koo zake. Wazifanyao watafanana nao, kila mmoja anayezitumainia.
Sasa ili tujiridhishe na ibada ya kweli inayokubaliwa na Mungu hebu tuangalie ibada ya mbinguni ilivyo, na jinsi viumbe wa mbinguni wanavyomwabudu Mungu.
10. IBADA KUU MBINGUNI Ufunuo 5:6-14
Biblia inafunua ibada kuu inayoendelea mbinguni ambayo washiriki wa ibada hiyo ni wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne, wenye vinubi na vitasa vya dhahabu vyenye maombi ya watakatifu, wakiwa mbele za kiti cha enzi cha Mungu. Viumbe hawa wapo hapo kufanya ibada maalum ili kumwabudu na kumpa sifa Mwanakondoo, wanafanya hivyo kwa kuimba wimbo mpya wenye sifa kwa Mwanakondoo kisha malaika wengi, elfu kumi mara elfu kumi, elfu mara elfu, ambao wamekizunguka kiti cha enzi wanajiunga katika SIFA hizo. Uf 4.8-11 Hapa ndipo ibada hii kuu inaanzia ,ambapo wenye uhai wanne wasiopumzika mchana na usiku wanamsifu Mwanakondoo wakisema Mtakatifu, Mtakatifu ,Mtakatifu na kusababisha wazee ishirini na nne kuanguka chini na kumsujudia aliye Hai milele na milele,huku wakivua taji zao na kuzitupa mbele ya kiti cha Enzi,wakisema ,Umestahili wewe Mungu kupokea utukufu na heshima na uweza kwakuwa ndiwe uliyeviumba vitu vyote kwa sababu ya mapenzi yako vilikuweko navyo vimeumbwa.
Kisha kwa sauti ya pamoja wanasema: Anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, heshima, utukufu, na Baraka Mwanakondoo aketiye kwenye kiti cha enzi. Maneno haya saba ni sifa kuu kwa Yesu ambaye ni Mwanakondoo wa Mungu.
Hatimaye baada ya ngurumo hizo za sauti ya sifa, kila kiumbe kilichoko mbinguni, duniani, na baharini vikamsifu Mwanakondoo, na wote wakaanguka wakamsujudia Mwanakondoo. Sifa hii ikatikisa ulimwengu, ulimwengu mzima ukamwabudu Mwanakondoo, Ibada hii haifanywi kwa mtume, nabii, malaika ,miungu wala kwa mwanadamu bali Ibada hii inamlenga Yesu Mwanakondoo. Ibada inayofanywa kwa mtu mwingine mbali na Yesu siyo Ibada ya kweli na Mungu haisikilizi. Inasikitisha kuona Ibada za mamilioni ya watu hazisikilizwi na Mungu kwakuwa zinafanywa nje ya kumwabudu Yesu.
Katika Zaburi 98:1-9 na 96:1-8 Mfalme Daudi anatoa mwaliko wa kumwabudu Bwana kwa wimbo mpya kwasababu Bwana Ametenda mambo ya ajabu, Daudi anasema”,
• Inueni sauti, imbeni kwa furaha,
• Nayo mito ipige makofi, na kulibariki jina lake,
• Na kutangaza wokovu wake,
• Kwa kuwa Bwana ni mkuu na mwenye kusifiwa sana.
Wito huu ni wito wakumwabudu BWANA peke yake.
Paulo naye anatia mkazo wa kumwabudu Mungu kwakutoa mwongozo jinsi ya kufanya ibada katika roho ya uimbaji anasema “Neno la Kristo likae kwa wingi mioyoni mwenu (ndani yenu) katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu. Mkisemazana kwa zaburi na tenzi, na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Mungu mioyoni mwenu, nakumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo Kol 3:16-17, Ef 5:19-20. Ibada ya kweli ni ile inayomlenga Yesu na si vinginevyo.
Unaweza kuona jinsi mwanadamu anavyotoa muda wake, nguvu na mali katika ibada hewa kwa viumbe na sanamu, badala ya kumfanyia Mungu ibada katika Kristo Yesu, wito huu ungali na nguvu ile ile kwetu kumgeukia Mungu na kujiunga na viumbe hawa wa mbinguni kumfanyia ibada sahihi Mwanakondoo. Mungu ni mtakatifu na wa haki hana kigeugeu na habadiliki, ni mwadilifu. Hawezi kuweka njia tofauti tofauti za kumwabudu kwa kila mtu. Hiyo ingekuwa sawa na wasafiri wawili waendao mji mmoja lakini kwa njia tofauti zinazoweza kuwafikisha pale waendapo, hilo haliwezekani kwa Mungu maana ni Mtakatifu,kwa utakatifu huo ,Mungu ameweka njia moja ya kumwabudu ambayo ni Yesu Kristo.
SURA YA PILI
IBADA NA UIMBAJI
A. Zaburi 96.1, 98.1
Mungu anapenda uimbaji na anapenda kuimbiwa wimbo mpya kama tuonavyoona katika zaburi hizi,Kwa asili yake yeye ni mpya kila siku hajawahi kuzeeka wala kuchakaa,basi kwa asili hiyo hupenda vitu vipya,ni muhimu kuwa na nyimbo mpya na pambio mpya katika ibada zetu.
Ibada inayofanywa katika Roho na Kweli haiwezi kuendeshwa bila ya kumwimbia Mungu nyimbo za sifa na za kumwabudu. Huu ndio utaratibu na mfumo wa ibada ya kiroho, kuanzia mbinguni mbele ya kiti cha enzi na katika agano la kale na Agano jipya mpaka leo.Asilimia sabini na tano ya shuguli za kanisa ni kuabudu,na asilimia tisini ya kuabudu ni uimbaji yaani kuimba.
Nyimbo zinazoimbwa ziimbwe katika Roho na akili pia, zikielekezwa kwa Mungu, zikikoleza maombi na sala zetu, zikiibua sifa za dhati toka moyoni nakunyosha misisimiko ya nafsi, fikra, mwili isipotoke kwenda nje ya ibada ya kweli, kwa hiyo nyimbo zisiimbwe kwa lengo la burudani, bali ziimbwe kwa lengo la kumsifu Mungu, kumshangilia, kumshukuru, kufariji, kutia moyo, kumkaribisha Mungu, kusaidiana, kuonyana nakujengana na kuachilia neema ya Mungu iwafunike wanaomwabudu mahali hapo. Matokeo ya Ibada kama hii ni makubwa, 2Nyakati 5:11-14. Wakamfanyia Bwana ibada kuu, Bwana akaijaza nyumba utukufu, makuhani wakashindwa kufanya kazi zao maana Bwana ameshuka katikati yao na kuwabariki. Ibada inayoendeshwa bila uimbaji ni ibada bubu na haitaleta matokeo mazuri kwa waabuduo.Kwakuwa Mungu ni mpenzi wa uimbaji ndani ya ibada zetu,hivyo ni muhimu mno kuimba kwa sauti zilizopangiliwa vizuri ili tumbariki.
B. UIMBAJI NDANI YA IBADA
Ni vigumu kutenganisha uimbaji na ibada, uimbaji umetawala matendo ya mwanadamu kwa asilimia kubwa, kiasi kwamba uimbaji ni lugha inayomuwezesha mtu kujieleza alivyo, ni kama chakula cha lishe chenye virutubisho vya aina zote kwa afya ya mwanadamu. Uimbaji unagusa maeneo yote ya utu wa mtu na mahitaji ya mwanadamu, kiroho na kimwili.
Uimbaji ni chakula kilicho bora kabisa kukidhi matamanio ya mtu mzima. Mtu akiwa na huzuni, msiba, ataimba ili afarijike na kujiliwaza au ataimba ili aomboleze, katika sherehe umetawala, dhifa, mikutano ya aina zote ya kiroho na ile ya kisiasa, matambiko, kazi, hata katika vita, matangazo ya biashara, vyombo vya habari, matukio yote haya hutanguliwa na uimbaji na kumaliziwa na uimbaji.
Uimbaji huleta uponyaji wa Roho na mwili na huondoa mkandamizo na msongo wa mawazo. Hii ndiyo nguvu iliyomo katika uimbaji. Ni vema basi kila mmoja wetu akaelewa uimbaji ninini, na unafanyikaje ili aweze kutumia katika kumwabudu Mungu wakati wa ibada. Si jambo jema kuimba ovyo bila mpangilio ama bila kujua nakuelewa.
C NYIMBO NA AINA YA IBADA
A. Kila ibada ni muhimu na ina malengo yake na madhumuni,ama makusudi ya kufanya ibada hiyo.Kwahiyo ni lazima kila ibada ipewe nafasi katika nyimbo zinazoimbwa katika ibada hiyo.Iwapo nyimbo zinazoimbwa haziendani na lengo ,kusudi au madhumuni ya ibada, basi ibada hiyo imevurugika na watu watashindwa kuabudu kuelekea lengo la ibada hiyo.mwisho watu watachanganyikiwa na kuwa watazamaji na kuwaondoa kabisa katika ibada inayoendelea hapo Ingawa kimwili watakuepo.
B.Si vema kuimba wimbo wa maombolezo katika ibada ya arusi au wimbo wa pasaka katika ibada ya krismasi ama wimbo wa uinjilisti katika ibada ya meza ya Bwana.IBADA si jambo la mzaha bali ni tendo la kumuabudu MUNGU, Kwahiyo ni lazima ufanyike upangaji na uchambuzi makini wa nyimbo zipi ziimbwe katika ibada ipi ili kukidhi hitaji la ibada husika
Ufuatao ni mchakato wa aina ya ibada.
Ibada ya kuabudu ziimbwe nyimbo za kuabudu,Ibada ya SIFA, Ibada ya uinjilisti, Ibada ya maombi na kujitoa ,Maisha ya Kikristo kwa ujumla wake.Imbisha nyimbo zinazoendana na ibada hizo.
Nyimbo za Matukio.Hakikisha unaimba nyimbo zinzokwenda na matukio hayo. Meza ya Bwana,Krismas, Pasaka, Arusi, Maziko na Maomboleza,Siku kuu, Mwaka mpya,Watoto,Mwaliko wa mtu kwa Yesu,Nyimbo za taarifa au ushuhuda wa matendo makuu ya Mungu,Utakaso na Kutia moyo na IMANI,Ujasiri,Mashambulizi kwa shetani au Vita ya kiroho,Roho Mtakatifu na nyimbo zenye ujumbe maalum kwa matukio maalum kama vile ,uzinduzi wa nyumba ya IBADA ,au jambo lolote linalogusa kanisa au jamii.Ni muhimu kuimba nyimbo zinazogusa ujumbe wa matukio hayo. Huu ni mwongozo wa jinsi ya kuendesha ibada na uimbaji utakaoleta Baraka na kutufikisha katika kusudi la ibada husika.
Ili kufikia azma hiyo nitatoa historia ya uimbaji nakueleza baadhi ya mambo muhimu yatakayokuwezesha kufahamu kidogo uimbaji katika sura inayo fuata.
Katika somo hili la uimbaji nitalenga uimbaji wa kikristo wenye mtazamo na misingi ya kibiblia. Uimbaji ni somo pana lenye kuwa na mielekeo tofauti tofauti kulingana na matumizi ya mtu anavyotaka. Ingawa kanuni za muziki (uimbaji) ni zilezile kwa kila mwelekeo.
SURA YA TATU
HUDUMA YA MUZIKI (UIMBAJI) KATIKA SIFA NA IBADA
A. 1. Muziki ni nini?
Ni sanaa inayoishi iliyo hai ambayo inadumu mpaka ulimwengu ujao katika umilele. Huduma zingine zote zitakomea hapa duniani bali muziki hautokoma utakuwepo milele na milele. Isaya 35: 10 msitari huu unahusu watu waliokombolewa kwamba wataimba milele! Na hao walio kombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba, na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao, nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia ,Furaha ya milele, ni kiashirio cha uimbaji wa watu hawa kwamba wataimba milele.
Muziki Ni lugha ya kiulimwengu inayozungumza na hisia za mtu yoyote, lugha hii hueleweka na msikilizaji, kwa kuguswa utu wake na fahamu, kisha nafsi, moyo, akili na mwili. Haijalishi lugha iliyomo katika wimbo, muziki, kwamba unajua au la, mawasiliano sahihi yanakuwepo na kueleweka katika hisia za msikilizaji. Muziki una nguvu ya kuleta amani na furaha moyoni, burudiko na pumziko la akili kiasi cha kumshawishi mtu kukubali nakujiachia katika mivuto yake.
Nguvu ya muziki imeujaza ulimwengu na kupenya katika utamaduni wa kila kabila, taifa, jamii, na lugha, hii inaonyesha muziki hauna mipaka. Muziki umesafiri bila kizuizi kwa njia za mawasiliano ya vyombo vya habari popote ulimwenguni. Ni vigumu kwa mtu kujizuia kuitikia mara asikiapo muziki ukiunguruma , muziki ni chakula cha masikio na ubongo, muziki mtamu unapoingia masikioni mwa msikilizaji hupenya kwenye akili zake, na akili zake huusukuma mwili na kuanza kutikisa kichwa, miguu, mikono na kiwiliwili, na kucheza, kutokana na utamu wa wimbo na ujumbe wa wimbo huku akirukaruka kufuata midundo ya muziki unaopigwa.
Katika zama zetu, muziki umekuwa ni utambulisho wa taifa na heshima ya nchi, kila nchi duniani ina wimbo maalumu wa Taifa ambao huimbwa kuutukuza utaifa na heshima ya Taifa. Kila wakati tukio la kitaifa, wimbo huo huimbwa, mgeni anapotembelea nchi, huimbwa ambapo kila mtu aliye mahali hapo hutakiwa kusimama kimya huku akiimba wimbo huo.
Hapa ni muhimu tuelewe kwamba muziki si uhuni, ama kudhani kwamba ni kazi ya watoto, watu wasio na kazi au watu maskini, hapana hiyo ni dhana potofu, na mtamzamo hasi dhidi ya muziki, tunapaswa kubadilika kimtazamo na kuona utajiri uliomo katika muziki, kwamba ni hazina tuliopewa na Mwenyezi Mungu kuwa urithi wetu. Na kumshukuru Mungu kwa vipaji na karama alizowajalia waimbaji na wanamuziki wanaohudumia katika huduma hii ndani ya Kanisa la Kristo.
Dunia ingekosa muziki ingekuwa katika giza nene na maisha yangekuwa butu katika nyanja zote. Muziki ni nyenzo fanikishi katika kuelimisha jamii kwa jambo lolote kwa wepesi na kwa haraka, bila vikwazo ama vizuizi.
Biblia imejaa rejea nyingi za muziki, zaidi ya rejea 800 zinazungumzia muziki. Huu ni ushahidi wa kutosha juu ya umuhimu wake. Msisitizo huu wa maandiko unaonyesha wazi kwamba muziki ni huduma ya kiroho kweli kweli, na kwamba Biblia ni kitabu cha nyimbo, pia ni kamusi ya uimbaji wa kiroho kwa waabuduo, na kwamba kila rejea ya uimbaji itokane na Biblia.
2. MUZIKI NI UHAI wa Tamaduni, desturi, mila za jamii za watu ulimwenguni kila jamii ina mifumo na mitindo iliyojengeka tokea zama za mababu zao wa kale, ambao waliachia maadili vizazi vyao vitakavyokuwepo baada yao. Historia hiyo ya maadili ilitunzwa na kuhifadhiwa katika nyimbo – muziki umetumika kama Benki ya kutunzia maadili na tamaduni za utaifa. Benki hii ilifanya kazi kabla ya uvumbuzi wa kuandika vitabu kuweka kumbukumbu za taifa na jamii husika. Haya tunayaona kwa Musa na wana wa Israeli Kumb. 31:29-, 32:1-44-47 Maandiko haya yanahusu Musa alipokuwa akiwaaga na kuwapa wosia Israeli kabla ya kufa kwake. Akawafundisha wimbo wa wosia na kuwaamuru wawaimbie watoto wao na watoto wao wawaimbie wimbo huo watoto wao na kuendelea.
B. UFUNGUO WA KUABUDU NA KUSIFU
Zab: 100:1-4, 95:1-7
Mungu yuko mahali palipotukuka sana na kuinuliwa: Hili linanipa wazo kwamba kuabudu na kusifu ni stahili ya MUNGU. Isaya 57:15-16. Maana yeye aliye juu aliyetukuka akaaye milele ambaye jina lake ni Mtakatifu – anasema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka palipo patakatifu tena pamoja na yeye aliye na Roho iliyotubu na kunyenyekea na kuifufua mioyo yao waliotubu. Hii ndiyo sifa na ufunguo unaotakiwa na Mungu. Tutamkaribiaje Mungu kama huyu aliyeinuliwa na kutukuka sana?
1. Jibu linapatikana katika maandiko haya Zab 95:1-5
a) Njoo tumwimbie Bwana
b) Tuje mbele zake kwa shukrani
c) Kwakuwa Bwana ni Mungu Mkuu na mfalme mkuu juu ya miungu yote.
e) Mikononi mwake zimo bonde za dunia , mikono yake iliumba bahari na nchi kavu
Katika ms 6 mwaliko unatolewa kwenda kumwabudu, kumsujudia kwa kumpigia magoti (kupiga magoti ni tendo la kumkiri na kumtambua kuwa ni Mungu) Bwana aliyetuumba- Mungu wetu ambapo sisi tu malisho yake na kondoo wa mkono wake (yeye ni Mchungaji).
Mungu hukaa na mtu aliyetubu na kunyenyekea, kamwe hawezi kukaa na mwenye dhambi ingawa anampenda. Ibada ya mtu huyu itakubaliwa na Mungu Zab 96:9 Huu ni wito mwingine: Mwabuduni Bwana kwa uzuri, na hofu ya utisho ndani ya moyo wa utakatifu – tetemekeni mbele zake nchi yote. Utakatifu na hofu ni funguo za mlango wa sifa na ibada ya kweli. Njia kuu kwa mwanadamu kumfikia Mungu katika enzi yake ni kumpa shukrani na sifa anazostahili – tukishajitakasa kwa Toba
2. UMUHIMU WA IBADA YA KWELI
Ibada ya kweli ambayo ni BORA ni pale tunapomgusa MUNGU katika ENZI YAKE kwa roho ya unyenyekevu na kupondeka kwa moyo. Zab 100:1-4 zaburi hii inatuonyesha njia nzuri ya kumwabudu Mungu na kuhimizwa kumfanyia Bwana shangwe, sifa na shangwe ni stahili ya Mungu.
Uimbaji wa sifa – ni ufunguo Mkuu wa kuingia ndani ya nyumba ambamo Mungu yumo (ibada ni huduma, na kuabudu ni kazi) kuabudu ni utumishi angalia anavyosema
– Mtumikieni Bwana kwa furaha
– Njooni mbele zake kwa kuimba
Huwezi kuingia ndani ya nyumba pasipo kufungua mlango lazima uwe na ufunguo. Kama Zaburi ya 100 inavyosema Ingieni malangoni mwake kwa kusifu na kwa kushukuru.
Isaya 1:12 Naye anasema, Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ninani aliye taka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Mungu anauliza mnapoingia nyuani mwake Kwa utaratibu upi maana huwezi kukanyaga nyua za Bwana kiholela hapo ni Ikulu pana heshima yake na jinsi ya kuingia. Mungu kama Mfalme yumo ndani ya ikulu, nyumba yake, hekalu, yaani mahali palipowekwa wakfu kwa Ibada. Tunapaswa kwenda hapo na ufunguo. Jueni Bwana ndiye Mungu, ametuumba na sisi ni watu wake na kondoo wa malisho yake. Zab 100:1-4 anasema kwa msisitizo, Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru, haya ni malango ya hekalu (hekalu la kale) Nyuani au barazani mwake kwa kusifu na kwa kushukuru na kuhimidi Jina lake .
Uimbaji ndiyo ufunguo wa malango ya Bwana kuingia barazani pake, Hodi yetu ni sifa, kuimba na kushukuru kunatupa kibali cha kuingia patakatifu pa patakatifu.
Kanisa na Mkristo asiyeimba na kusifu ni bubu, kamwe hawezi kuingia na kumwona mfalme Barazani pake. Mkristo huyo amekosa ufunguo hawezi kujieleza, hana shangwe, hana shukrani ni kama mtoto mchanga aliyezaliwa wodi ya wazazi lakini bado hajalia, anakasoro ni kilema, ipo hatari ya kupoteza maisha. Hivyo hivyo mkristo asiye na ufunguo huo atapoteza maisha ya kiroho. Ibada ya kweli yenye funguo hizo ni uhai wa Mkristo.
Kusifu na kuabudu kunaonyesha uhai wakati tunpomwimbia nyimbo za sifa na shangwe namshnagaa mtu wa aina hiyo ambaye haabudu maana hana uhai. INJILI ilienezwa kwa nyimbo katika karne ya 17 huko ulaya – Martin Luther, John Wesley, John Calvin, John Hus, John Wyclife walitumia nyimbo kuhubiri neno. Kwa sababu kuna nguvu yenye uhai wa Mungu katika sifa.
Katika Mathayo 26:26-30 Hapa Yesu aliimba pamoja na wanafunzi wake, aliimba Zaburi 115 hadi 118. Zab 89:5-7 inasema mbingu zitayasifu maajabu yako na uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. Hii inaonyesha kwamba walioko mbinguni wanaabudu. Kutojali na kudharau uimbaji ni kumdharau Yesu ambaye aliimba – ni kupoteza ufunguo mkuu ambao hufungua nyumba na baraza la Mungu. Kumbuka Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu. Baraza la watakatifu ni pale watakatifu wanapokusanyika kuabudu Mungu.
Katika 1Kor. 14:26 Paulo anasema mkutanapo pamoja kila mmoja ana Zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri, mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga. Hizi ndizo faida za kuwepo barazani pa watakatifu, na umuhimu wa ibada ya kweli
3. Vidokezo vya msaada unaopata unapoimba:
a. Unawezeshwa kujieleza kwa undani jinsi unavyompenda na kumwabudu Mungu
b. Uimbaji unakupa ufasaha wa kumsifu Mungu kwa furaha na uchangamfu.
c. Utakaso na toba huambatana na kuimba bila kizuizi.
d. Unawezeshwa kumfanyia Mungu ibada kama alivyo kuagiza na kwa wepesi.
e. Ibada huongozwa na kuendeshwa vema kwa muziki na kumwabudu Mungu kwa utamu na kwa raha.
f. Unawezeshwa kuonyesha upendo wako tena baada ya maungamo na ukiri wako kwa Mungu na kudhihirisha kwamba moyo wako umefunguliwa na umewekwa HURU.
Dondoo hizi ni nyenzo za muhimu kutusaidia kumwabudu Mungu ili tusipungukiwe na kukosa neema na Baraka zake zilizomo barazani mwake. Ingia na uzichote baraka kwa funguo ulizojifunza na utazipata tu kadiri unavyonyenyekea moyoni mwako.
C. TUIMBE KWA JINSI GANI ?
Zab 150:1-6, 33:1-3, 98:1-9, 100:1-4
Maandiko haya yanatuelekeza jinsi ya kumwabudu Mungu kwa vifaa mbalimbali vinavyotumika katika muziki, ikiwa ni pamoja na hali ya mtu anayeabudu inavyotakiwa kuwa
Huduma ya muziki wakikristo ni muhimu iwe na mwelekeo wa kibiblia mifumo na malengo pamoja na utekelezaji wake lazima upatikane ndani ya maandiko matakatifu. Kwa maana lolote tulifanyalo tunalifanya kama kwa Bwana. Basi kama ni hivyo tuyaangalie maandiko mbalimbali:
Zab 98:1 – Tumwimbie Bwana wimbo mpya, tumshangilie, tumpe shangwe, na sifa, shukrani, furaha, faraja na kumtukuza, vigelegele na kucheza. Mambo haya ni sehemu ya muziki wa kikristo na wa kiroho. Ni muhimu na lazima tuimbe kwa ustadi na kwa ubora, kwa ari kubwa na shauku, kwa kupania bila kujibakiza wala kujihurumia, hii ni kazi nzito sana.
– I Nyak 16:4-11, 23-34 Hapa tunaona uimbaji ni huduma ya makuhani – hii ndiyo ofisi ya mwimbaji ni kuhani wa Mungu afukizaye uvumba mbele ya madhabahu kwa sadaka za sifa na shukrani, INyak 6:31 tunaona Walawi waliimba kwa utaratibu ulioeleweka INyak 16:4-11, 23:35 waliimba kwa zamu, walikaa kwa mtindo wa kueleweka wakati wa huduma. Walijifunza kwa waalimu wao kwa bidii. WALITABIRI KWA KINUBI, WAIMBAJI NI MANABII wanatabiri kwa vinanda wanavyovipiga kwa ustadi. 1Nyak 25:1-9
D. HALI YA MOYO NA JINSI YA KUTUMIKA
1) Mungu ndiye anatoa karama na huduma hii, basi ni lazima watumishi
waishi maisha matakatifu na moyo safi. Na unyofu wa moyo yaani
mwenendo wenye tabia njema hilo halikwepeki, wakiwa wamejitakasa
mwili na roho, ibada ni tendo la kumcha Mungu. IIKor 7:1 Amos 5:21
2) Yatupasa kumwimbia Mungu tukiwa na vifaa vya muziki au vyombo vya muziki. Accompanyments – vikolezo. Maandiko yanakazia sana kuimba pamoja na vyombo vinubi, vinanda, zeze la nyuzi kumi, filimbi na matari Mungu wetu ni mpenzi wa muziki kuliko mfalme yoyote wa duniani. Ili ibada ya sifa na kuabudu ikamilike, muziki wa vyombo ni muhimu, bila kusahau mfumo, mtindo na utaratibu mzuri.
E. UIMBAJI KITAALUMA
Mwimbaji asiyejua kuimba hawezi kuwa huru kuhudumu ni muhimu afahamu uimbaji ili aimbe kwa uhuru na kwa ufanisi. Ufanisi unahitaji muda wa mazoezi yakutosha pamoja na mwalimu mwenye uwezo wakukuelekeza jinsi ya kuimba Muziki (uimbaji) upo katika mafungu makuu mawili :
I. Vocal
II. Instrumentals
VOCAL: Ni sauti ya wanadamu. Sauti isiyochanganywa kitu chochote. Sauti asilia ya mtu (Natural voice)
INSTRUMENTALS:
Ni sauti zitokanazo na vyombo. Sauti pasipokuchanganywa na kitu chochote yaani ala za muziki. Sehemu hizi mbili zikichanganywa pamoja hufanya kitu kinachoitwa muziki (uimbaji) na kukamilisha maana ya NENO MUZIKI.
SAUTI. Ni hisia inayonaswa na masikio na hutokana (hutengenezwa) na msuguano wa hewa katika mzunguko, mgongano wa vitu au mkwaruzo kiasi cha kutoa mlio (sauti).
SAUTI –MLIO (AUDIBLE, SOUND)
1. Kitaalamu Sauti ina misingi au kanuni .
Misingi hiyo ni Miwili. Ni kwa misingi ya sehemu hizo mbili kuu- Sauti hujengwa/huumbika, tutaelewa misingi hiyo vizuri kwa kuziangalia tabia za sauti (Characteristics of Musical Sound) Au tabia za milio.
2. Msingi wa kwanza:
a) Sauti ina tabia ya – Melody – Yaani kwa Kiswahili – Ghani
Melody – Ghani – Ni mistari ya sauti ya muziki inayotambulisha chanzo (tone) cha wimbo ni sauti yenye kuelekeza ubora wa mtiririko wa ghani (melody) unaokupa hisia ya mlio unaohusika au unaousikia.
b) Rhythm – Ni utaratibu au mfumo wa aina ya mwendo wa sauti katika wakati au mfululizo wa sauti katika muda, mwendo, pigo, mdundo au msisimko. Uwezo wa sauti wa kutembea katika wakati usiobadilika.
c) Harmony – Mkusanyiko wa sauti unaopendeza, utaratibu au mfumo wa ulinganifu wa sauti, usawa, muafaka, kusikilizana pasipokuachana kwa sauti au kuwa nje ya tune hasa wakati kuna watu wengi wanaimba, katika ngazi tofauti yaani sauti ya msitari wa 1, 2, 3 na 4 pamoja.
d) Unison—Ni sauti ya aina moja inayoimbwa na watu wengi bila ya kutofautisha ngazi za sauti ya kwanza, pili,tatu na nne. Na kwa kawaida sauti ya unison hutumia sauti ya kwanza.
e) Form – Ni mwonekano wa kipekee, utaratibu au mfumo wa kuweka uimbaji katika aina ya mfumo unaojitambulisha katika mtindo wake wenyewe kama vile mtindo wa kizungu, wa kiafrika, kigogo, kihaya nakadhalika.
f) Tone Color – Aina mbalimbali za sauti kufuatana na chombo au mtu anayeimba – kwa mwanadamu sauti hutegemea mapafu yake na mishipa ya fahamu ya kichwani. Yaani sauti kavu, sauti laini, yenye mikwaruzo, yenye mawimbi nakadhalika, kusikika kwa sauti kipeke, kivyake kwa kadri ya mtu anavyotoa sauti au chombo kinavyo toa sauti kwa namna ya mlio wake
3. Msingi wa Pili:
Sehemu ya kwanza Nimetaja nadharia ya tabia za sauti, tabia hizi huwezi kuziona wala kuzihisi, ama kuzisikia, ila unaweza kuzifikiria katika mawazo. Kuimba sio nadharia wala mawazo ni matendo halisi. Nadharia hiyo lazima itafsiriwa katika vitendo tunavyoweza kuviona, kuhisi, kusikia tabia za sauti au milio hiyo. Haya yanawezekana kwa kutumia nyenzo , njia za muziki za kiufundi zinazotuwesha kutenda.
(Musical Skills Performance Methods)
Nyenzo au njia hizo ni:
a) Kuimba – (Singing – Melody) Unapoimba ndipo Ghani itajitokeza katika mpangilio wa sauti kwa njia inayopendeza na kwa utaratibu, hapo Tone Color itasikika yaani kwa kuimba wimbo, ghani na aina za sauti katika ubora wake utasikika.
b) Kupiga vyombo vya muziki – Accompanyments – vikolezo. Melody ambayo ni Ghani itasikika – Tone color pia itasikika.
c) Form, Kutenda vitendo – (Moving – Movement –Steps) Rhythm na Form itaonekana yaani kucheza kwa mwendo wa mapigo. Yaani sauti na maneno unayoimba yataenda kwa kufuata mapigo na midundo ya wimbo na kuwa na muonekano wa kipekee.
d) Harmony. Kusikiliza ndiko kutakuwezesha kuleta ulinganifu katika mkusanyiko wa sauti za kupendeza na kukuwezesha uimbe sawasawa na sauti nyingine bila kuhitilafiana wala kuachana au kuwa nje ya ghani.
e) Kuunda au Ubunifu (Creation – Form, Rhythm na melody) Wimbo utakamilishwa kwa kuunganisha nyenzo hizo nakuwa halisi yaani wimbo halisi wenye kusikika vizuri.
Katika msingi huu wa pili tunafika katika kukamilisha muziki na
ndiyo uimbaji. Muziki ni sayansi lakini kila mmoja wetu
anayo na anaweza kuitendea kazi kwa kujifunza na kujizoeza.
F. SIFA ZA MWIMBAJI.
Kazi ya kumwimbia na kumsifu Mungu ni huduma inayodai maisha ya mtu kujitoa kikamilifu na kuwa na mwenendo uliosafi. Mungu aliwaweka waimbaji katika hekalu waifanye huduma hiyo maalumu. Kwa hiyo ni lazima pawepo na sifa za kutosha na mchakato yakinifu kuhusu mwimbaji anayefaa kuifanya huduma hii kubwa. Mwimbaji ni chombo cha sifa za Mungu ni lazima chombo hicho kiwe na sifa zinazoendana na sifa za Mungu na heshima kimfaacho Bwana kwa kazi hiyo. Zab. 33:1 11Tim 2.21.
ROHO YA UIMBAJI
Ni kujaa Neno, kusemezana, kushangilia, kuimba kufundishana, kuonyana, kujaliana, umoja na shukrani, Ef 5:18-20 Kol 3:16-17 hii ndiyo Roho ya uimbaji.
Mwimbaji anatakiwa awe na sifa muhimu 13 zifuatazo:-
1. Mwimbaji awe mtu aliyeokoka Isaya 5:11-12, Zab 50:16-17
2. Mwimbaji awe Mshirika, Mwanachama mwaminifu wa Kanisa
3. Mwimbaji awe na tabia njema, mwenendo mzuri kiroho
4. Mwimbaji awe na wito na Msukumo wa Kimungu katika huduma hii na si vinginevyo
5. Mwimbaji aifahamu sauti yake vizuri, hisia zake azielekeze sawasawa katika ujumbe wa wimbo, asikilize miundo ya sauti, asitende vitendo au kuzidisha vitendo katika wimbo isivyo kawaida.
6. Mwimbaji ahudhurie mazoezi pasipo kukosa, mazoezi
huleta ukamilifu wa huduma .
7. Mwimbaji awe tayari kutoa huduma wakati wowote bila masharti
8. Mwimbaji ajitahidi kujiendeleza, kuboresha, na kuikuza sanaa ya
muziki na kupandisha viwango vyake vya uimbaji.
9. Mwimbaji awe mtu wa maombi akiombea huduma.
10. Mwimbaji awe mtiifu, mnyenyekevu, akiheshimu viongozi wa kanisa
na huduma yake.
11. Mwimbaji awe na bidii katika upendo wa kweli na kudumisha umoja
na mahusiano katika huduma.
12. Mwimbaji aimbe kwa upako wa Roho, kamwe si kwa
mazoea wala kwa ujuzi pasipo kusahau maandalizi ya
mwili, usafi na muonekano usio na maswali
13. Mwimbaji aimbe kwa lengo la kumwinua, kumsifu, na
kumtukuza Mungu kwa utukufu wake. Na si kwa lengo la
kupata umaarufu na fedha.
Mwimbaji na mtumishi asiyekuwa na sifa hizi, hawezi kuwa mtumishi katika huduma ya mwili wa Kristo ambalo ni Kanisa, ambalo lipo kwa ajili ya kumpa sifa, utukufu na enzi Mungu aliye mkuu. Sifa hizi zinatufikisha katika utumishi mwema wa huduma ya kimbinguni ya sifa na ibada ya kweli katika Roho.
SURA YA NNE
SIFA NA KUABUDU NA MAANDALIZI YA IBADA
I. KWANINI IBADA NI YA LAZIMA
Ibada ni ya lazima kwa sababu kuabudu ni tendo linalofanywa kwa kiumbe aliye Mkuu kuliko kitu chochote na ambaye ana uwezo wa kutenda mambo pasipo msaada wa mtu, wa kitu, yeye ndiye mwanzo na msababishaji wa mazingira yanayomzunguka mtu amwabuduye kiumbe huyu. Na hivyo kiumbe huyo ingawa si kiumbe huitwa MUNGU – Kwa hiyo mtu anayebudu anamwabudu Mungu huyu mkuu
2. KWANINI TUMSIFU NA KUMWABUDU
Zipo sababu nyingi kama Mfalme Hezekia anavyoelezea katika Isaya 38:17-20 na katika amri kumi za Mungu Kutoka 20: 3-5 Katika utu wa mwanadamu alivyoumbwa, iko silika na kiu na njaa ya ndani ambayo inamsukuma mtu kutafuta mawasiliano na Mungu hata kama mtu hajawahi kufundishwa kwamba Mungu yupo, njaa na kiu iliyomo ndani itajitokeza na kutaka ushirika na Mungu.
Hii ndio njaa na kiu ambayo Bwana Yesu anaisema katika Mathayo 5.6 anaposema Heri wenye Njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa.ingawa katika kutojua kwao njaa na kiu yao hupotoshwa kuelekea mahali pasipo sahihi. Na ms wa 3 Unasema Heri walio maskini wa Roho,hali ya umaskini wa roho hutufanya tutafute mahali pa kuegemea na kuumba ndani yetu hali ya uhitaji na unyenyekevu,kujisalimisha,kupondeka na kumheshimu Mungu,kumwabudu,kumtukuza,kumwinamia, kujiaminisha kwake,kumwangalia yeye katika mahitaji yetu yote ya kiroho na kumtegemea..
Ndiyo maana watu huabudu sanamu, miti, mawe, mizimu, jua, mwezi na nyota na miungu kwa kudhani vitu hivyo ni Mungu na hivyo kupata afueni ya madai hayo ndani ya mioyo yao. Mdo. 17:22-29Watu wa Athene walikuwa na njaa na kiu ya Mungu kiasi kwamba waliona ni afadhari watengeneze madhabahu ya Mungu asiyejulikana na wamwabudu bila kumjua ili mioyo yao ilidhike na kupata amani na ahueni.
Kuabudu ni agizo, agizo hilo limo katika amri 10, Kut 20:3-5 linasema
1. Tusiwe na miungu wengine ila Mungu mmoja wa pekee
2. Tusifanye sanamu za kuchonga kwa mfano wake
3. Tusivisujudie wala kuvitumikia viumbe
4. Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu asiyechangamana na miungu
5. Kama utaabudu viumbe hivyo ameapa kwamba atatuhukumu (atatupatiliza)
Mfalme Hezekia anatoa sababu za kuabudu kama ifuatavyo Isa 38:17-20
1. Amekuokoa na shimo la uharibifu Zab 55:23
2 .Amezitupa dhambi zako nyuma yake. Hii ni pamoja na magonjwa Yer
31:34, Isaya 53:4-5, Mika 7:19.
3.Kuzimu haiwezi kukusifu mtazamo wa Agano la kale kuzimu ni makao ya
wafu
4. Mauti haiwezi kukuadhimisha
5. Wala washukao kuzimu hawawezi kukusifu
6. Aliye hai ndiye atakayekusifu, kaburini hakuna sifa
7. Bwana amekupa wokovu. Sababu hizi zinatupa ukweli wa msingi wa kuabudu
8. Na kuazimia kumwimbia na kumsifu Bwana maisha yako yote nyumbani mwa Bwana
9. Kusifu ni sadaka kwa Mungu Waeb 13:14-16 kusifu ni tunda la midomo yetu, Mpe Mungu haki yake toka midomoni mwako, moyoni ujaze sifa na kukiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na Mwokozi.
10.Kwa kutambua kuwa Mungu anastahili Ibada yetu kama Mungu
mwenyezi, hata kama tusingepata chochote chenye manufaa kwetu,
hiyo haiondoi stahili ya kuabudiwa. Daniel 3:16-18 Ndipo Shadrack
Meshak na Abednego wakajibu wakamwambia Mfalme Ee
Nubekadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo
Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo
moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee Mfalme. Bali kama si hivyo,
ujue, Ee Mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako wala
kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
Vijana hawa walikuwa tayari kumwabudu Mungu ndani ya tanuru ya moto hata kama Mungu asingeliwaokoa.Kuabudu hakuhusiani kabisa na mazingira yanayokuzunguka ,bali ni haki ya Mungu anayostahili kupewa na mwanadamu mahali popote alipo. Paulo na Sila walimwabudu na kumsifu Mungu wakiwa gerezani huku wamefungwa minyororo, ibada yao ilimgusa Mungu,nao wakapokea muujiza wa kufunguliwa wakawa huru.Mdo 16.22-28.
10. MAANDALIZI YA IBADA
Kutoka 19.9-25
A. Mungu ni Mtakatifu na mahali alipo ni patakatifu mno
Maandalizi ya ibada ni muhimu sana kutokana na hali ya Mungu alivyo,Ibada sio matembezini wala ibada sio mchezo wa mpira ambao kila mtu anaruhusiwa kwenda uwanjani kuangalia.Kuna masharti na taratibu za kufika mahali pa ibada na kuabudu,Math 5.8 Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Bwana, na Waebrania 12.14, anasema Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na HUO UTAKATIFU ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao Hatuwezi kumkaribia Mungu Mtakatifu bila ya kuwa watakatifu.
Hebu tungalie mchakato wa maandalizi ya wana Israeli walipotakiwa kuonana na Mungu katika mlima wa Sinai ili wamwabudu.
• M 9 Mungu angekuja katika wingu zito,wingu liliubeba utukufu wa Mungu na kupunguza makali ya utisho wake mtakatifu ili angalau waweze kufikia viwango vya sifa ya kumkaribia na kumwabudu.
• Mungu aliamuru wajitakase kwa siku tatu,wafue nguo zao .Utakaso wa siku tatu ungetosha kuwafanya wajinyenyekeshe mbele za Mungu na kuondoa uchafu wa mawazo maovu na kumtafakari Mungu.
• Mungu aliamuru mipaka iwekwe ,wasiukaribie mlima,wasiuguse atakayegusa atakufa na atakayemgusa aliyekufa naye atakufa.
• Waliamriwa wasikaribiane na mwanamke,ili wasivutwe na kitu kingine chochote kile zaidi ya kuweka shauku yao kwa Mungu peke yake.Swala la kuabudu halina ubia, Mungu anataka mfumo mzima wa akili zako na ufahamu ukamatwe na yeye kwa kumwabudu.
• M 16 Mlima Sinai ukatoa ngurumo,umeme, wingu zito likatua juu ya mlima ,baragumu ikalia sana ,tetemeko likatokea ,moshi na moto ukalipuka juu ya mlima,Haya yote ni ishara kwamba Mungu ameshuka tayari kwa ibada yake na wana wa Israeli , Mungu hukaa katika mlima wa moto na mahali ambapo yupo na utukufu wake upo .
• Ms 19 Bwana akashuka juu ya kilele cha mlima na kusema na Musa kwamba watu wasithubutu kupasua mlima na kupanda Hii ikimaanisha apandaye ni lazima awe anamfanana Mungu kwa utakatifu.
• Makuhani nao waliamriwa kujitakasa ili wasiangamie.Kujitakasa ni sharti la kila mtu bila ya kuangalia cheo cha mtu bali nafsi ya mtu ilivyo.
• Mkazo mkubwa wa masharti haya ni utakaso wa mioyo kabla ya kukutana na Mungu,ulazima wa kujitakasa unatokana na utakatifu wa Mungu asiyekaribiwa na mtu aliye na dhambi,na hasa mtu ambaye anajua Mungu hapendezwi na dhambi lakini kwa makusudi hataki kutubu, mtu huyu hawezi kumkaribia Mungu na kumwabudu.
B.Ibada inaanzia moyoni katika mazingira yako ya kawaida ,kazini , nyumbani, ibada si jambo la kukurupuka, ibada ni jambo nyeti lenye kuhitaji kumakinika. Ibada Inahitaji maandalizi ya uhakika na utaratibu unaoeleweka. Ibada inaanza mapema kabla ya kufika mahali ambapo ibada inafanyika.Tunapofika hapo ni kilele cha ukamilifu wa ibada ambayo ulianza mapema.Ibada haianzi katika mlango wa kanisa.
IINyak 29:5,11, 15-17, 29-31. Hezekia Mfalme alifanya maandalizi makubwa ya ibada na akawambia walawi,
Ms 5, Nisikieni enye walawi, jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya Bwana, Mungu wa Baba zenu, mkautoe uchafu katika patakatifu. Ms 11 Basi wanangu, msijipurukushe sasa, kwa kuwa Bwana amewachagua ninyi msimame mbele yake, kumuhudumia, nanyi mpate kuwa watumishi wake mkafukize uvumba. Ms 15 – 17 wakawakusanya ndugu zao, wakajitakasa, wakaingia kama alivyo amuru Mfalme kwa maneno ya Bwana, ili waisafishe nyumba ya Bwana. Nao makuhani wakaingia nyumbani mwa Bwana, katika mahali pa ndani ili waisafishe, wakatoa uchafu wote walio uona hekaluni mwa Bwana, wakautupa nje uani mwa nyumba ya Bwana. Walawi wakautwa iliwauchukuwe nje mpaka kijito cha Kidroni. Basi wakaanza kutakasa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, hata siku ya nane ya mwezi wakafika katika ukumbi wa Bwana wakaitakasa nyumba ya Bwana katika muda wa siku nane, wakaimaliza siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza. Ms 28 – 31 Na kusanyiko lote wakaabudu, waimbaji wakaimba, wenye mapanda wakapiga, haya yote yakaendelea hata ilipomalizika sadaka ya kuteketezwa. Hata walipo kwisha kutoa sadaka, Mfalme, na hao wote walikuapo naye, wakasujudia, wakaabudu. Tena Hezekia Mfalme na wakuu wakawamuru walawi, wamwimbie Bwana sifa kwa maneno ya Daudi, na ya Asafu mwonaji. Wakaimba sifa kwafuraha, wakainama vichwa, wakaabudu. Ndipo Hezekia akajibu, akasema, Sasa mmejifanya wakfu kwa Bwana, karibuni mkalete dhabihu na matoleo ya shukurani nyumbani mwa Bwana. Basi kusanyiko wakaleta dhabihu na matoleo yashukrani, na wote wenye moyo wa ukarimu wakaleta sadaka za kuteketezwa.
Hapo tunaona Mfalme Hezekia anafanya maandalizi yakinifu kwa ajili ya ibada – hatuwezi kufanya ibada kwa kulipua, mfalme Daudi naye anajieleza moyo wake ulivyo tayari kumwabudu Mungu: anasema, NALIFURAHI WALIPONIAMBIA NA TWENDE NYUMBANI KWA BWANA Zab. 122:1
Je unakuja kanisani kimazoea au unakuja kukutana na Bwana? Moyo uliojaa ibada hautatoa nafasi ya kupoa na kulegea katika mambo ya kiroho. Mtu aliyepoteza hamu, shauku, mapenzi na Mungu – HANA ROHO YA IBADA NA HAWEZI KUABUDU.
I Kor 11:27-30 inahusiana na ibada ya meza ya Bwana. Ilihitaji kujihoji kabla ya kula (kushiriki) Lakini Wakorintho walishiriki meza ya Bwana pasipo maandalizi, walipoteza maisha yao (walikufa) Katika agano la kale kuhani asingeingia hekaluni patakatifu pa patakatifu bila kujitakasa, maana kuingia bila kujitakasa kungemaanisha kifo, hivyo Kuhani alijiandaa. Mambo yaliyowakuta Wakorintho yanaweza kumkuta mtu yeyote leo ikiwa atapuuzia na kutojali ibada takatifu kwa kutojianda vema,Mungu wa Wakorintho ndiye Mungu wetu Waeb 13.8,Yesu Kristo ni yeye yule jana Leo na hata milele hajabadilika anadai viwango vile vile vya utakatifu.
Ibada ni wakati wa muhimu sana, wakati wa nafasi ya kipekee na wa dharura, wakati wa jambo tukufu katika maisha ya mwanadamu. Ni muhimu uwepo mahali pa ibada ukiwa kamili umejiandaa vyema, kama neno linavyosema ya Kaisari mpeni Kaisari na ya Mungu mpeni Mungu. Huwezi kwenda kwenye sherehe bila kujiandaa bali unajiandaa vyema katika hali zote ili usijiabishe bali upendeze. Ibada ni sherehe kuu mno ni lazima ujiandae na kuipa stahili yake. Angalia waislamu wanafunga biashara zao wakati wa ibada kwa kuwa ni wakati muhimu sana kwao kuliko kazi na fedha, kwao ibada ni kila kitu.
JIWEKE TAYARI KWA SIKU YA IBADA
2Wakor 7:1
Utayari wa moyo kukabili ibada ni wa muhimu sana. Pasipo utayari huo ibada inakuwa ni maigizo na unafiki, maana ibada huanza moyoni. Ukishajiweka tayari moyoni unapaswa kujiweka tayari kimwili, pamoja na vifaa vitakavyoboresha ibada na kukupa wepesi wa kufanya ibada ili utimize utakatifu na kumcha Mungu
HAKIKISHA UNAJIANDAA KAMA IFUATAVYO:
a) Andaa mavazi yako na ya mtoto mapema na siyo jumapili asubuhi. Inasemekana kwamba wanawake huchelewa kufika katika shughuli kwa miezi minne kati ya miezi kumi na mbili ya mwaka, kwa kushughulika na vitu ambavyo wangeviandaa mapema na kumfanya awahi mahali anapotakiwa. Shughuli hizo zinapofanywa asubuhi Jumapili husababisha uchovu na kuharibu hamu ya ibada kabisa. Huwezi kujiachia moyo wako kuabudu kwa raha na furaha ukiwa na presha na mafadhaiko.
b) Acha kufanya miradi yako ibadani hapo siyo ofisini bali wewe tuliza mawazo yako kabisa na kuzingatia ibada. Na kuelekeza akili zako katika ibada,acha kuwa mkaguzi na mpelelezi wa mambo kanisani.
c) Fuata maelekezo yote unayopewa na kiongozi wa ibada na kushiriki bila kutilia shaka au kusita yale unayo agizwa.
d) Fanya urafiki baada ya Ibada sio wakati wa ibada , usikae nje ya ibada, kaa ndani ya nyumba ya ibada na kuzama katika ibada.
e) Heshimu na kuwa na adabu muda wote wa ibada usizoee kanisa. Kutembea au kugeukageuka bali tulia.zima simu yako,usitoketoke nje kila dakika ,mwangalie kiongozi wa ibada na kumsikiliza .
f) Mwone Mungu, Hisi uwepo, Baraka zipo ukiwa karibu naye atakuwa karibu na wewe pia.
g) Jitoe kama sadaka mwenyewe, lete sadaka, mali zako , usije mikono mitupu. Kuabudu ni kazi siyo starehe, abudu kwa bidii mpaka jasho likutoke. Kwa kuwa hakuna ustaarabu katika ibada zaidi ya Mungu aliyekuumba. Kwasababu Mungu ni wa kuuogopwa sana barazani pa watakatifu Zab 89:5-8 kwa hiyo abudu kwa hofu na kutetemeka, na kuweka kando kila mzigo mzito moyoni na katika fikra zako.
h) Njoo na Biblia, kitabu cha nyimbo – vitunze na shika vizuri, usiviweke chini ya sakafu na vibebe kwa heshima wakati wote
i) Kamwe usichelewe kufika katika IBADA kwa wakati uliopangwa maana Mungu ni mwaminifu katika kila jambo kwahiyo usimwibie muda wa ushirika wake na wewe.Saa ya ibada ni saa ya ushirika wako na Mungu .
5.UIMBAJI WA KANISA Ef 5:19, Rum15:9-11,Zab 113.1-3,Mdo 13.2-3
Mahali pekee tunapoweza kukaa kwa pamoja kwa umoja kama ndugu tukapendeza ni Kanisani wakati wa ibada .Hapo Mungu anashuka na kutumwagia Baraka .Pia husema nasi kwa Roho Mtakatifu wake.Basi ni muhimu kila mshirika awe sehemu ya kumpa Mungu sifa kwa uimbaji wa pamoja kama mtu mmoja huku tukisemezana kwa nyimbo za rohoni .Bila shaka Mungu atatenda makuu kama alivyofanya kwa Kanisa la Antiokia.
A: Uimbaji wa kanisa zima ni muhimu sana, na ibada ya pamoja ina nguvu tena ni tamu na ina upako. Maana unahusu kila mtu katika ibada. Mwamini anapata nafasi ya kuhubiri na kutabiri kwa njia ya nyimbo. Yesu anahubiriwa kwa njia ya nyimbo sio madhabahuni tu. Itumie nafasi hii vizuri. Shiriki kuimba, imba vizuri, jitahidi kuzijua nyimbo ili uabudu kwa raha bila kuburuzwa na wale wanao zijua nyimbo.Acha tabia ya kuwa msikilizaji,msikilizaji mkuu wa nyimbo zetu awe ni Mungu na watu walio nje ya ibada.
B. Uimbaji wa nyimbo kwa kanisa zima ni njia nyepesi ya kujifunza Neno kwa ujumbe uliomo katika nyimbo. Nyimbo zinagusa mafundisho mbali mbali ya kikristo. Kwa njia ya nyimbo watu hukunjwa kiroho kwa urahisi na kujikuta wanapomoka katika kuabudu na kusujudu. Mtu akikosa ibada ya sifa anaweza kukosa kabisa baraka na utamu wa ibada ya siku hiyo. Nyimbo ni burudoza la Roho linalong’oa vikwazo vyote vinavyozuia moto wa ibada moyoni. Hakikisha unashiriki ibada ya sifa kila wakati bila kukosa. Na uwe sehemu ya kuchochea moto wa Roho Mtakatifu katika ibada. Usiwe zima moto kwa kutoshiriki maelekezo, au kutotenda maagizo ya kiongozi wa sifa.
6. WAJIBU WA MCHUNGAJI KATIKA IBADA (NAFASI YA MCHUNGAJI)
Mchungaji ni mtu namba moja katika ibada, na msimamizi mkuu wa ibada, uwepo wake katika ibada una nguvu ya kuvuta usikivu kwa waamini kutulia na kuzingatia ibada.
Tabia ya mchungaji kuchelewa kufika ibadani hupunguza nguvu ya ibada. Ina maanisha mchungaji ana sehemu kubwa ya kufanikisha kuabudu kwa waamini wa kanisa lake kuwa bora. Mchungaji ni kuhani, kama kuhani anatakiwa kuwa na ufahamu wa kila kitu kinachofanyika katika ibada na kushiriki shughuli zote akiwaongoza waamini kufuata maelekezo yatolewayo na kiongozi wa sifa aliyeko mbele ya ushirika. Kwa kadri Mchungaji anavyo onyesha moyo wa kupenda ibada na ushabiki katika sifa na kuabudu, ndivyo waamini watakavyo ipenda ibada vilevile.
Ni muhimu atoe ratiba ya mpango wa ibada utakavyokuwa mapema kwa kiongozi wa sifa na kumshirikisha yatakayokuwepo siku ya ibada. Ibada inapofikia kileleni mchungaji ajiunge na kiongozi wa sifa kulipeleka kanisa madhabahuni pa Mungu ili watu wahudumiwe kwa maombezi, na kumpa Mungu shukurani na sifa kwa kelele za shangwe, utukufu na heshima. Kama Mchungaji ana kipaji cha uimbaji aongoze nyimbo za kuabudu katika mtiririko ule ule na kwa kiwango kile kile, ama zaidi ya kiongozi wa sifa. Kama hana kipaji cha uimbaji basi amwachie kiongozi aendelee na yeye awaombee waumini Neema na mibaraka ya Mungu 1Wakor 16:23-24
6. KIONGOZI WA IBADA
Asili ya ibada ni mbinguni Mungu amezungukwa na jeshi la malaika mamilioni wanaomwimbia usiku na mchana. Uf 5:1-14 hapa tunaona ibada ya ulimwengu. Lucifer alikuwa ni mkuu wa malaika na kiongozi wa ibada ya mbinguni Ez 28:13-15. Katika ibada ya kanisa lazima awepo kiongozi wa ibada, mtu huyu ni muhimu sana, ni kama dereva wa gari moshi yuko mbele kwenye injini na nyuma anafuatiwa na mabehewa mengi yenye shehena mbalimbali. Usalama wote wa abiria unakuwa umeachwa mikononi mwa dereva kufika au kutofika, kupumzika katika vituo au kwenda mfululizo moja kwa moja ni dereva ajuaye.
Haya ndiyo majukumu ya kiongozi wa ibada. Tunamtazamia atufikishe mahali alipo Mungu ili tumsujudie na kumwangukia. Kwa hiyo ni muhimu kumsikiliza kiongozi kwa makini. Ibada ni kama gwaride ambapo amri ni moja inayotoka kwa kamanda wa kikosi na ni yeye peke yake anayesikilizwa. Kiongozi wa sifa ni kamanda wa kikosi, yaani ibada na waabuduo.
Mambo muhimu
A: Kiongozi wa ibada apate ushauri wa Mchungaji kabla ya huduma ili apewe ratiba au utaratibu wa ibada kwa siku husika.
• Aweke uwiano mzuri wa nyimbo za vitabuni,zinazohusu kuabadu ,kusifu
Na pambio hivyo hivyo pia.
? Apange nyimbo atakazoimba mapema, ni hatari kutokupanga nyimbo, kutokupanga nyimbo ni sawa na dereva asiyejali kazi yake,anaye endesha gari lake bila ya kulikagua, bila shaka atasababisha ajali.
? Awe na uwezo wa kuwasiliana na ushirika na kusimamia kila kitu wakati ibada inaendelea,kwa kuhisi kama mambo hayako sawa ayadhibiti.
? Aendeshe ibada ya Uimbaji kwa njia nyepesi ambayo kila mtu ataaabudu bila shida.
? Afahamu ujumbe wa mhubiri na kufuata mtiririko huo katika nyimbo. Azijue nyimbo atakazoimba kwa usahihi.
? Afahamu mtiririko wa Roho. Mtiririko wa nyimbo uwe sahihi, utukufu hadi utukufu kuelekea kileleni nakumaliza ibada kwa moto kuliko ibada ilipoanza.
B: Imbisha nyimbo zinazofahamika
Nyimbo hizi watu watazimba kwa uhuru na kwa msisimko, mtu hawezi kuimba wimbo toka rohoni wimbo asioujua maneno. Kutojua maneno kutamzuia mtu kuzama rohoni na kujimimina mbele za Bwana, maana akili yake imegawanyika katika kutafuta maneno ya wimbo.
C: Imbisha Nyimbo Mpya
? Fundisha nyimbo mpya kila baada ya muda Fulani, tumia muda mfupi wa dakika tano mwanzoni mwa ibada.
? Tumia vitabu na kukariri – wazoeshe waamini kukariri maneno ya nyimbo
? Tumia mbinu kufundisha wimbo mpya – fundisha kwaya ili ilete athari ya wimbo huo kwa kanisa wakati wa ibada
? Fundisha kikundi cha Praise na siku maalumu itengwe kwa Praise Team kufanya mazoezi, kwa kuwa kuabudu ni shughuli kuu ya Kanisa. Kamwe usiyapuuzie mazoezi. Jambo hili lifanyike kwa nidhamu kubwa
? Fundisha wimbo mmoja kila mwezi tangu mwanzo mpaka mwisho wa mwezi na kuongeza idadi ya nyimbo zinazojulikana na waumini.
? Jifunze nyimbo za vitabu na pambio kwa usahihi, usipindishe na kuimba tofauti na mtunzi aliyeuandika wimbo au pambio, uwe mwaminifu kwa hilo. Ni makosa kuimba wimbo kinyume na mtunzi aliye uandika
D: Imbisha nyimbo zinazogusa uzoevu wa maisha
Watu unaowaongoza wana mapito mbalimbali, imba nyimbo zenye kugusa hisia za maisha, mazingira yao, mapito yao, nyimbo hizi zitakuwa na maana kwao, uwe mwepesi kutambua hali ya kusanyiko lako, na kuimba nyimbo zinazokidhi mahitaji hayo, zitawagusa na kuwafanya waabudu kwa dhati toka moyoni
E: Imbisha nyimbo tofauti tofauti
Jihadhari sana na mawazo mgando na kujisahau kwa kuimba nyimbo zilezile ulizozizoea, kila wimbo una ladha na mvuto wake kama utaimba kwa dhati toka moyoni, usije ukapewa jina la Bwana, Hakuna Mungu kama wewe, au Mama, Mungu yu mwema ama, Ninani kama wewe Bwana, utawakinaisha watu.
? Nyimbo zipo tele, Nyimbo za haraka, za polepole, za vitabuni, pambio za ushuhuda, zenye nukuu ya maandiko, za kitamaduni wa aina zote. Fanya utafiti wa nyimbo na kuzielewa na uwe mbunifu kutunga nyimbo zako.
? Jifunze kwa waimbaji wenye uzoefu na kufanya zoezi la kutosha kila wakati. Uwe msikilizaji mzuri wa nyimbo, ili ujenge uwezo wako na ujuzi wa kuimba kwa mbinu tofauti za matumizi ya sauti, na kuzitumia mbinu hizo kwendeleza kipaji chako bila kuwaiga wengine.
F: Muonekano wako mbele ya Ushirika
Mara ukishasimama, kila jicho liko kwako, lazima uonyeshe unyenyekevu na adabu, hofu na heshima ,Fahamu umesimama mahali patakatifu .Kut 3.2-5.
? Tumia lugha fasaha sio lugha mbovu, ngumu, au lugha ya mafumbo na ya mitaani na usitumie ukali.Kama vile washikaji wangu,usiwe na noma,mambo poa, vipi huko uswazi.asiyeimba ndiye shetani wa Ibada .
? Jua upo hapo kuwaabudisha watu, na siyo kuonyesha maungo yako au kuuza sura kwa muonekano wako.dhibiti miondoko yako ukiwa madhabahuni.
? Onyesha ibada ya kweli na ya dhati mwenyewe ili uwavute waumini kuelekea ibada ya kweli na ya dhati pia. Kiwango chako katika kuabudu ndicho kiwango watakachokuwa nacho waamini unaowaongoza,ukilia watalia na ukijazwa ROHO nao watajazwa Roho.
? Usiende mbele yao haraka unapoimba wala usiwe nyuma yao na kupoozesha ibada, hakikisha unapiga makofi yanayokubalika na mwendo wa wimbo.
? Sema, elekeza na imba, kila mtu asikie maneno, usiyabane maneno, sema wazi
? Fahamu ukumbi, idadi ya watu, na usipige kelele, tumia kipaza sauti vizuri, na hakikisha vyombo vya muziki havina hitilafu itakayo vuruga ibada.
? Taja kitabu, wimbo, ukurasa, namba , wakaribishe watu kuabudu na anza kuimba kwa nguvu yaani kwa makini.
? Usiwe na maneno mengi mwachie Mhubiri aseme na watu maneno mengi
? Sauti yako iwavutie watu, iwe na upako, jifunze kuitumia vizuri usipayuke payuke, tulia
? Usiache mwanya wa ukimya kati ya wimbo na wimbo isipokuwa kwa sababu maalum
G: JIANDAE
Kuongoza ibada kunahitaji maandalizi mazito, maombi, tafakari. Kariri nyimbo na kufanya mazoezi ya kutosha. Wakati wa mazoezi tumia kioo kikubwa ili ujiangalie unavyoonekana na kujiweka sawa utakavyoonekana mbele ya watu siku ya huduma. Fikiria utakavyowahamasisha watu waabudu. Wajue watu, vijana, wazee, wagonjwa, wageni na watoto wote wape nafasi ya kuabudu kwa kuzingatia hali zao. Mfano ukiwamuru watu kusimama muda mrefu wazee na watoto watashindwa na hivyo hawataabudu, kila kitu kiwe na kiasi.
Maliza na kufunga ibada au kipindi kwa uangalifu mkubwa kwa maombi, wimbo, au kwa makofi ikiwa hali inaruhusu kufanya hivyo, kisha kabidhi ibada kwa mhusika na kuondoka madhabahuni kwa adabu na heshima
6. VIGEZO VYA KUONGOZEA NYIMBO
Orodha ya nyimbo utakazo imba ipatikane kwa mpiga kinanda na mpiga ngoma ( drum) ili kuwasaidia kupanga mapigo na sauti ya wimbo.
Uwe makini na uanzaji wa nyimbo na umalizaji, uanzaji wa vyombo, ishara za mikono , chanzo au kiini (tone) na ufunguo wa wimbo, mwendo au miondoko ya wimbo (Rhythm), ukimudu haya ibada itakuwa tamu na nzuri na usipomudu itakuwa mbaya na itawakera watu. Kusifu na kuabudu ni kipimo kikubwa cha kanisa lililokomaa au kanisa changa kiroho. Kamwe usipuzie vigezo hivyo, vitilie maanani kila unapoanza wimbo
Watu watajiunga na kanisa au kulihama kanisa kutegemea ibada yenu mnavyo iendesha. Ibada ya mbinguni haina ubabaishaji wala makelele Ufu. 5:7-14. Ibada ni biashara nzito na kitu cha kuheshimiwa sana. Acha kuimba ovyo, malaika wanaanguka na kusujudu mbele za Mwana Kondoo. Sisi tufanyeje? Inatupasa kufanya vyema ili ibada yetu impendeze Mungu na wanadamu pia.
SURA YA TANO
FAIDA ZA KUABUDU
Sifa ya kweli ya mkristo ni jinsi anavyomwabudu Mungu si mavazi yake, wala elimu yake. Sifa nzuri ya kanisa si jengo zuri ama sare za watumishi, ratiba za ibada zao na katiba ya kanisa. Bali ni jinsi gani kanisa linamwabudu Mungu katika Roho na Kweli. Umaskini mkuu kwa mkristo na kanisa ni kutojua jinsi yakumwabudu Mungu katika Roho na Kweli na katika uzuri wa utakatifu. Kanisa litakalo mwabudu Mungu katika Roho kisha likawa na utaratibu mwingine ni jambo jema.
Mw 1:26-27
Natufanye mtu kwa mfano wetu. Haya ni maneno ya kwanza kabisa toka kinywani mwa Mungu yakionyesha USHIRIKA na MAHUSIANO matukufu yenye msingi wa Ibada ya ajabu. Mz 3:8-9 Mungu alimuumba mtu ili awe na ushirika naye Mungu alimtafuta Adamu Akamwita. Mungu angali anamtafuta mtu, anataka kusema nasi, anakuita katika ibada. Mungu anasema, na mtu hujibu, hili pekee ni tendo la kuabudu. Ibada ikikatika, Mungu husikitika usikitika na kuhuzunika, ibada ni kazi ya kudumu na ya milele.
Yoh 15:16 Si ninyi mlionichagua mimi bali ni mimi niliyewachagua ninyi, ni katika ibada tutapewa lolote tuombalo kwa maana yeye ametuchagua. Bado Mungu anamtafuta mtu Ms 13-15 unaonyesha kwamba wewe si mtumwa bali rafiki, kama rafiki ametujurisha yote. Yesu amechukua nafasi ya kwanza kututafuta. Anataka tumwonyeshe kumkubali kwa kumwabudu na hapo tutakuwa na ushirika wenye furaha pamoja naye.
Kuabudu ni kumtambua Mungu na kumfanya rafiki, huu siyo uhusiano wa utumwa. Zab 23:6 Hakika wema na fadhili zako zitanifuata, siku zote za maisha yangu. Kwa nini zikufuate, kwa maana wewe ni rafiki. Ibada ya kweli inaanzia kwa kutambua uhusiano wako wa karibu na Mungu. Ukaribu huu unazaa shauku ya kutaka kuwa kama yeye.
Kama watoto tuliozaliwa na kukombolewa na damu ya Yesu kutoka dhambini na mauti tunamkubali mwokozi na muumba wetu kwa upendo wa dhati. Katika hali hiyo Shauku yetu ni kuwa kama Mungu, Kuwa kama Mungu ni tendo linalipatikana katika kuabudu. Hamu hii itaendelea kuongezeka kadri tunavyokaa naye. Ukaribu wa wana ndoa huwafanya wafanane kwa tabia na maneno kwa kadiri wanavyoishi pamoja na kufanya mawasiliano ya kila wakati. Mawasiliano ni kiunganishi muhimu katika kuabudu. Isaya 41:21 Mungu anasema leteni maneno yenu na hoja zenu zenye nguvu. Huu ni uhusiano wa karibu unaopatikana katika mawasiliano ya karibu.
Faida za Ushirika na Mungu ambazo zinatupa kufanana na yeye zinaonekana katika vifungu vifuatavyo:-
Mz 5:22-24, 6:9 Henoko alimcha Mungu na akakumbatia njia za Mungu. Amos 3:3 Je, watu wawili waweza kutembea pamoja wasipokuwa wamepatana? Henoko alitembea na Mungu mpaka akanyakuliwa kwenda mbinguni. Alimwabudu, alishirikiana naye akaondolewa duniani. Pia Nuhu alikwenda pamoja na Mungu bega kwa bega. Dunia iliharibika kwa dhambi lakini alimcha Mungu, alimwabudu Mungu, Mungu akamwokoa na gharika. Nuhu alikuwa mswalihina na akajitenga na uovu, nakushikamana na Mungu katika kizazi kilicho potoka .
Kutoka 34:28-35. Musa alifunga siku 40 hakula hakunywa akapanda mlimani kwa Mungu, akiwa huko uso wa Musa uling’ara kwa sababu alikuwa katika uwepo wa Mungu. Tunapomwabudu tunabadilishwa tufanane naye. Tunapewa maono, ufunuo, na hekima. Musa aliporudi kutoka mlimani sura yake ilikuwa inang’ara na watu walimkimbia.
Hii ndiyo tofauti ya mtu wa ibada ya kweli na anayeshirikiana na Mungu na mtu wa kawaida ambaye hana utakatifu, hana upako, wala nguvu, hatishi. Maombi yake ni dhaifu wala pepo hawaondoki. Kaa katika uwepo wa Mungu kutoka hapo wewe siyo mtu wa kawaida utamnyanyasa shetani na kazi zake zote. Tunaona pepo wa mgerasi walipiga kelele wakisema, tuna nini nawe Yesu mwana wa Mungu? Nakuapishwa kwa Mungu usinitese. Yesu akasema ewe pepo mchafu mtoke mtu huyu. Mak 5:7-8 pepo walimtoka mara moja na kuwaingia nguruwe na nguruwe wakajitupa Baharini.
Ukitaka kuwa mkuu, kaa mbele za Mungu utakuwa mtu wa kutisha. 2Kor 3:18. Kwa uso usiyotiwa utaji tukiurudisha utukufu wa Bwana kama katika kioo, tunabadilishwa tufanane naye na mfano huo huo toka utukufu hata utukufu kama vile utukufu utokao kwa Bwana aliye Roho “We are made in by a reflective material “- tunapokaa na Bwana tunanyonya sura yake, na sura yake huumbika kwetu. Tunakuwa kioo chenye sura yake. Je unanyonya sura gani? Dunia au fedha, kama Yesu ni mshindi na sisi je ni washindi? nikiona mtindo wa maisha yako, nitafahamu ni Mungu gani unayemwabudu. Mtu wa Mungu anajulikana sura yake na mtu wa shetani anajulikana pia.Kaa karibu na Mungu mpaka sura yako ifanane naye.
IBADA HUMBADILISHA MTU
Zab 106:19-20 Walifanya ndama huko Horebu, wakaisujudia sanamu ya kuyeyusha. Wakaubadili utukufu wao kuwa mfano wa Ng’ombe mla majani. Zaburi hii inatupa mfano wa nguvu za miungu juu ya tabia za Israeli. Walipobadilisha Mungu na tabia zao zilibadilika, hapo ndipo kuna umuhimu wa kuabudu katika Mungu wa kweli atakaye umba sura yake kwetu. Ms 37-38 Naam walitoa wana na binti zao kuwa dhabihu kwa mashetani. Wakamwaga damu isiyo na hatia, damu ya wana wao na binti zao waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanani, nchi ikatiwa unajisi kwa damu. Mungu huyu wa ndama akabadili mfumo wao kabisa wakutoa sadaka za watoto kwa mashetani. Hata leo ibada zinazo fanywa kwa miungu zinaiharibu nchi na kuinajisi na kusababisha laana, Mungu aliumba nchi njema ili mwanadamu akae humo na kumwabudu yeye peke yake Mw 1: 31 4: 9 – 12
Hii inamaanisha kwamba kitu unachokiabudu kina uwezo wa kuyabadili maisha yako. Hata leo zipo dini ambazo kuua si dhambi kwa kigezo cha Mungu wao alivyo, Wafuasi wa dini hizo hawaoni tatizo kuua maana mungu wao anapenda kuua. Kwa hiyo ibada ya kiroho kwa Mungu hututengeneza na kutupa mwelekeo sahihi na kuwa na mfumo wa mbinguni Math 6-10 Rum 8:29 Lakini ikiwa Roho Wa Mungu anakaa ndani yenu nyinyi hamfuati mwili bali mwaifuata Roho. Hii ndiyo Baraka ya pekee kama tukijiachia kwa Roho.
Roho atatupeleka katika Ushirika na Mungu Mungu ataumba sura yake na ya Kristo ndani yetu, huu ndio mpango wake. Anatamani tufanane naye Yesu ili tuwe sehemu ya familia yake milele. Yoh 8:38 Tenda unayoyaona kwa baba yako. Kama Baba kama Mwana.Yoh 1.12-13 Roho atakufanya uwe mtoto wa Mungu.
ZIPO FAIDA MBILI KUU ZA IBADA
1. USHIRIKA NA MUNGU
2. BADILIKO LA MTU BINAFSI.
1. USHIRIKA NA MUNGU
Tunapokuwa katika Uwepo wa Mungu kila kitu huchukua maana mpya, hata yaliyo magumu hubadilishwa, kumbuka Esta na Modekai walivyookolewa katika msiba mkuu Esta nane na tisa. Petro 1:8 anasema,tunapokuwa katika uwepo wa Mungu tunapewa furaha isiyoneneka furaha hii ni matokeo ya ibada ya kiroho, ambayo haivurugwi na mazingira yanayotuzunguka, kwamba ni mazuri au mabaya.Kama ambavyo huzuni ya Wayahudi kwa ajili ya kuangamia kwao iligeuzwa na kuwa furaha kuu.
Bila ibada ya kweli hamna furaha. Luka 24:52 wakamwabudu, wakarudi wenye furaha kuu, tunapokuwa katika uwepo wake tunajazwa na furaha kuu mno. Lakini pasipo ibada ya kweli utaingia kanisani na mizigo moyoni na kutoka na mizigo. Tunaona wanafunzi walikuwa hekaluni. Hekalu ni mahali Mungu alikuwepo Israeli walikwenda hapo kuabudu. Sisi pia tuna makanisa au mahali pa makutano. Hapo ni makimbilio rufaa, kliniki ya kiroho na kufunguliwa. Petro alifahamu ukweli huo, akasema, twende wapi Bwana, nawe una maneno ya uzima. Usikubali kuondoka mahali alipo Bwana.
IKor 6:19 Miili yetu ni hekalu la Mungu – Roho Mtakatifu kwa hekalu hili popote tulipo tunaweza kukutana na Mungu tukahisi furaha, amani, katika uwepo wake. Maombi yangu kwako ni wewe kukaa na kutulia katika uwepo wake siku kwa siku mpaka sura yake ionekane katika kipaji cha uso wako. Siku zote mngoje Bwana hekaluni mwake na utamuona.
2. BADILIKO LA MTU BINAFSI
Zab 42:11, 36:7-9 Changamko la Uso lipo katika kuabudu na kusifu, kumtumaini Mungu kunaleta afya ya uso wako, huzuni, kuinama, kufadhaika kupo kwa mtu asiyeabudu. Basi kimbilia katika mbawa za Mungu, katika nyumba yake ambapo kuna unono, katika ibada utanyweshwa mito ya furaha, ndani ya ibada zipo chemchemi za uzima, hizo ni hekima na maarifa, vipawa, kutoka kwa Roho Mtakatifu. Mfanye Yesu kuwa mtu wa katikati maishani mwako, fikiri yaliyo juu. Mambo ya dunia yasipate nafasi moyoni mwako. Huu ndiyo MOYO WA IBADA utakaoleta mabadiliko.
SURA YA SITA
UMUHIMU WA MWILI KATIKA KUABUDU
Yoh. 4:24
A. Kimsingi kuabudu ni tendo linalofanyika rohoni, ibada inapofanywa rohoni, mwili unahusika. Mungu ni Roho Wamwabuduo lazima wamwabudu katika Roho na Kweli, Mambo mawili huhitajika ili kukamilisha ibada yako mbele za Mungu.
1. Matumizi ya mwili kwa utukufu wa Mungu
2. Kazi ya Roho Mtakatifu
I. MATUMIZI YA MWILI
War 12:1 Paulo anasema: “Itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai takatifu ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” Mwili ni chombo cha ibada na kuwekwa wakfu kwa kazi hiyo.
Mungu hakutosheka na kuabudiwa na malaika ambao ni Roho. Alitaka mtu amwabudu maana ana mwili, mawe na viumbe vingepiga kelele za sifa mbele zake, lakini hakuna kiumbe ambacho kingemridhisha na kumgusa Mungu kuliko mwanadamu. Uf 4:8-11 Hapa tunaona harakati kubwa za ibada mbele ya kiti cha enzi zikifanywa na viumbe wa mbinguni. Viumbe hao wanasema umestahili wewe Bwana.viumbe hao ni roho.
Pamoja na maneno haya matukufu kwa Mungu, Mungu hatoshelezwi na ibada hiyo, anamtaka mwanadamu kwanza. Kwanini imekuwa hivyo? Kwasababu mwanadamu ni mavumbi, ameumbwa kwa udongo na mikono ya Mungu mwenyewe.Efeso 4.24 ameumbwa katika utakatifu,haki na kweli. Asili hii ya mwili wetu inatupa nafasi ya pekee kunyenyekea kwa Mungu kiasi cha kumwangukia pasipo kujali mwili kwa kumwabudu. Isaya 66:2 Maana mkono wangu ndiyo umefanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana, lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye Roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu. Katika hali hii ya mwili tunamtosheleza Mungu.
Jambo kuu na la mwisho kwa mwanadamu sio ,utajiri,ukuu, sifa au ufalme bali kumpa utukufu Mungu aliemuumba na kumfurahia milele. Kwa maana furaha ya Bwana ndio nguvu yetu. Neh 8:10 Kwa kujua kwamba sisi tu kazi ya mikono yake na ni udongo hilo linatupa kutambua kuwa miili yetu imeumbwa kumwabudu na ndiyo kazi kuu ya mwili. Kamwe mwili wa mwanadamu haukukusudiwa kuwa chombo cha kumpa utukufu shetani. Lakini kwa huzuni kubwa shetani ameuteka mwili nakufanya kuwa chombo cha kuonyesha utukufu wake, na kumdhalilisha Mungu na mwanadamu mwenyewe kwa kutumia mwili kinyume na kusudi lake.
2. KAZI YA ROHO MTAKATIFU
I. NDANI YA HEKALU
IKor 3:16 IIKor 6:16-17 Mwili ndilo hekalu la Roho Mtakatifu na ndipo mahali anapokaa na kufanya kazi zake kwa ajili ya Mungu. Hekalu hili limetengwa maalum kwa kazi ya Mungu ambayo ni ibada na sifa na utumishi mwingine. Kuwepo kwa Roho ndani ya hekalu kunampa nafasi Mungu kutembea katika maisha ya mwamini na kumfanya mali yake. Lakini ajabu tunamkataa Roho ndani ya hekalu lake na kulifanya pango la wanyang,anyi
IKor 14:15-16 War 8:26 Nitaomba kwa roho nitaimba kwa akili. Maana yake ni kwamba Roho Mtakatifu anamvuvia mwamini kama anavyomjalia sawasawa na mapenzi ya Mungu kiasi cha kunena kwa lugha na kupewa karama za Roho kama apendavyo yeye.Mwili ni makao ya Roho Mtakatifu
IKor 12:7-10 Katika upako huo mwamini anaweza kupomoka katika maombi na kuimba, kusifu na kumshukuru Mungu katika lugha yake, pia katika lugha ya Roho Mtakatifu- ambapo Roho Mtakatifu anamuombea mambo muhimu kwa ajili yake. Roho Mtakatifu hutusaidia udhaifu wetu kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
Kwa hekima ya kibinadamu hatuwezi kugundua na kupambanua hitaji halisi linalotakiwa kulipa kipaumbele katika maombi yetu, shauku na hamu zetu katika maombi zinaweza kuwa kinyume na mapenzi ya Mungu, na ndiyo maana anatuombea akitusaidia udhaifu wetu War 8 26- 27 Roho anaichunguza mioyo na nia zetu na kuturejesha katika nia yake kama apendavyo Mungu. Hiyo ni kazi ya Roho Mtakatifu kwetu. Kumkosa Roho Mtakatifu katika ibada ni kuabudu katika desturi na mapokeo ya kidini ambapo ni kujidanganya wenyewe. Ni vema Roho Mtakatifu apewe nafasi ya kuongoza na kutawala ibada. Alipo Yesu yote yanawezekana hapo Roho Mtakatifu yupo kuikamilisha ibada.
• ROHO WA UTUKUFU
Petro 4: 14
Roho wa utukufu anahusiana na kuabudu, Isaya anasema, alimuona Bwana ameketi katika kiti cha Enzi, ameinuliwa sana na pindo za vazi lake zikaijaza Hekalu, Malaika wakimwabudu wakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu” Bwana wa Majeshi, Dunia yote imejaa Utukufu wake. Isaya 6: 1 – 4. Huu ni ufunuo wa Roho wa utukufu kwa Nabii Isaya juu ya Mungu mkuu katika mazingira ya utukufu mwingi anavyostahili kupewa heshima hekaluni mwake na kuabudiwa. Kadri Roho wa Utukufu anavyo mkalia mtu, ndivyo kiwango cha kuzama katika kuabudu kinavyo ongezeka.Roho wa utukufu humshawishi mtu kuabudu katika mazingira ya aina yoyote pasipo kuogopa mateso ama majaribu. Angalia Mitume Mdo 4: 27 – 31 ujasili wa mitume ulitokana na Roho wa Utukufu katika maombi yao walipo jaribiwa na viongozi wa Kiyahudi lakini hawakuogopa mateso.
Katika Matendo 6.8—15. Mungu alikua akimtumia Stefano kwa maajabu na ishara kubwa, Watu kutoka sinagogi la Mahuru wakamshitaki na kumsingizia kwamba anakufuru kwa vile aliwashuhudia injili ya kweli ya Yesu, wakataka kumpiga kwa mawe,Mdo 7.51—60.Maneno yake yakawachoma moyo na wakaanza kumsagia meno, Naye akijaa Roho Mtakatifu akakaza macho yake mbinguni akauona utukufu wa Mungu na Yesu amesimama mkono wa kuume wa Mungu, Ndipo wakamrukia kwa nia moja wakampiga kwa mawe.Huku akipigwa mawe Ms 59—60. akaomba, Bwana pokea roho yangu,akapiga magoti akasema Bwana usiwahesabie dhambi hii. Ujasiri na ustahimilivu wa Stefano ulitokana na Roho wa Utukufu aliyekuwa juu yake katika mateso hayo
Tunaweza kuomba na kuabudu pamoja lakini tukatofautiana katika mguso unao tokana na Roho wa Utukufu anavyo mkalia mtu na kumpa ufunuo na nguvu kuliko mwingine. Kadri Roho wa utukufu anavyokuwa ndani ya Kanisa, ndivyo ibada za kanisa zinavyo kuwa na nguvu za Mungu na kuwafanya watu wamuone Mungu katika utisho wake kama Isaya alivyo ona.
• ROHO WA UTUKUFU NA TENZI ZA ROHONI
Kol 3: 16
Roho Mtakatifu humuwezesha mtu kuimba sifa na kuabudu kwa Zaburi na Tenzi za Rohoni. Tenzi za rohoni ni sifa na kuabudu kunako toka moyoni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwa njia ya kunena kwa Lugha katika wimbo ambao huibuka ndani yake bila kujua sauti ya wimbo. Lakini papo kwa hapo mtu huanza kuimba kwa lugha asiyo ijua ama lugha anayo ijua kama Roho anavyo mjalia kutamka.T enzi za Rohoni sio nyimbo za kufundishwa, Ndio maana Paulo anasema, Huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu. Tunahitaji Neema yakumwimbia Mungu kwa Tenzi za Rohoni kwa viwango hivyo. Tenzi za Rohoni huimbwa na mtu binafsi ama ndani ya ibada hasa wakati wa maombi ya pamoja au wakati mtu ana faragha na Mungu Tenzi za Rohoni haziwezi kuimbwa kama wimbo wa kitabuni na kila mtu Tenzi za Rohoni ni aina Fulani ya kunena kwa lugha kwa njia ya kuimba.
II YESU ALIUVAA MWILI
Waebrania 10:5-7 Kwa hiyo ajapo ulimwenguni asema. Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili uliniwekea tayari, sadaka zakuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo ndipo niliposema tazama nimekuja katika gombo la chuo nimeandikiwa, Niyafanye mapenzi yake Mungu. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
A. MWILI WA YESU
Mwili ni muhimu katika kuabudu kiasi kwamba Yesu aliuvaa mwili. Yesu anasema – Lakini mwili uliniwekea tayari ili niyafanye mapenzi ya Mungu Math 3:17. Mungu mwenyewe anasema na Yesu akiwa katika mwili, Huyu ni mwanangu mpendwa ninayependezwa naye, Roho Mtakatifu akaja juu yake yaani ndani ya Yesu katika mwili. Hii ilikuwa kielelezo cha unyenyekevu wake katika mwili kwa Baba, tangu hapo aliendelea kumpendeza Mungu.
ITim 3:16 Ebr 5:7 Yeye siku hizo za mwili wake alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu, haya yalifanyika katika mwili. Maisha ya utauwa ni lazima yaonekane katika mwenendo wako wa kila siku. Yesu alidhihirishwa kuwa Mungu katika mwili. Akajulikana kuwa na haki katika roho. Akaaminiwa katika ulimwengu, akachukuliwa juu katika utukufu. Kama Yesu angekuwa Roho tusingemuona akichukuliwa juu katika utukufu. Kanisa lingekosa ujasiri kuhusiana na fundisho kuu la kupaa kwa Yesu, maana kupaa kwa Yesu kulionekana katika mwili.
Mwili wa Yesu uliandaliwa kuwa dhabihu ya dhambi kwa ulimwengu, dhabihu ni toleo la hali ya juu katika kumheshimu Mungu maishani mwa mtu anayemwabudu. Kama Yesu alivyoyafanya mapenzi ya Mungu katika mwili wake.
B: MWILI UTAMDHIHIRISHA YESU
II Kor 4:7-12 (Mwili wa mwamini)
Pasipo mwili Kristo hatadhihirika wala kutukuzwa. Mwili ndiyo chombo cha udongo ambapo kuna hazina ya Uzima. Katika mwili tunachukua kuuwawa kwa Yesu ili yeye aonekane yu hai. Kwa kufanya hivyo tunatoa miili kama dhabihu na sadaka iliyo hai kuwa ibada ya maana, na ya kumpendeza.
Katika historia ya kanisa tunaelezwa watakatifu waliokufa na kumwaga damu yao kwa imani yao katika Kristo. Huu ni ushuhuda kwamba kanisa limejengwa juu ya msingi wa damu ya watakatifu waliokufa, wakimdhihirisha Kristo katika miili yao.
I Kor 6:19
Miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu. Mwili kama chombo cha Ibada ni lazima uwe mtakatifu. Ili kudumisha matumizi yake ya ibada takatifu. Ikor 9:27 Paulo anasema, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha isiwe nikisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa. Mwili ni mahali pa harakati muhimu kuonyesha unyenyekevu na utii kwa Roho Mtakatifu IKor 6:20 Pia anasema mtukuzeni Mungu katika miili yenu War 6:12-13. Toeni viungo vyenu kuwa silaha za haki. Utaua, na utakatifu utatafsiriwa kwa matendo katika mwili. Umuhimu wa mwili unaonekana sana katika Yesu. Waeb 10:5, Zab 16:10 Mdo 2:25-31, Zab 34:20.
Roho (mwanadamu) inapotishwa chini ya Roho wa Mungu inatibua mwili mzima kuabudu. Mwili unapoitikia nia ya moyo wako kwa Roho wa Mungu hutokea Hisia. Hisia zinafichua mawazo yetu yaliyomo moyoni. Hisia zetu zinapofichuliwa lazima zitawaliwe na Roho ili kudhihirisha hisia safi zenye staha kwa Mungu na zenye ushuhuda, unaompa Mungu utukufu. Hisia za Rohoni zitajitokeza nje katika mwili kwa furaha, sifa, maombi, na kelele za shangwe na kwa kupiga makofi au vigelegele na machozi ya furaha. Hivi vyote vinatendeka katika mwili na kuwa ibada inayo mpendeza Mungu.
C: KUABUDU KWA VIUNGO VYOTE VYA MWILI
Kila kiungo cha mwili wako ni cha muhimu katika kumwabudu na kumsifu Mungu. Zab 63:15, 42:1-2
• Nafsi – (soul) inakuonea kiu, hiyo ni hamu, na shauku ya kumkaribia Mungu
• Mwili wangu wakuonea shauku, utoshelevu wa matakwa ya mwili ni katika Mungu. Huwezi kutosheleza mwili kwa vitu au hisia. utadai kukutana na Mungu mwenyezi. Ni Mungu tu atakayemaliza na kukomesha shauku za mwili.
• Midomo yangu itakusifu sifa ziko midomoni. Sifa za Mungu zijae vinywani mwetu na kumbariki Mungu. Mungu anabarikiwa na ibada ya kinywa chako. Zab 19:14 Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, ee Bwana, mwamba wangu na mwokozi wangu. Kupata kibali kunaonyesha Mungu anaikubali ibada ya viungo vyako.
• Kwa Jina lako nitainua mikono yangu, kuinua mikono ni kujitolea kwake kutarajia kupokea kitu.
• Kinywa, nafsi, midomo itakusifu kwa furaha. Mwili una sehemu ya muhimu katika kumwabudu MUNGU. Katika sehemu hii tumeona viungo vya mwili vikimwabudu Mungu. Ikimaanisha kwamba Mungu alimuumba mwanadamu ili amwabudu kuanzia utosi wa kichwa chake hadi uwayo wa miguu yake pamoja na viungo visivyoonekana vilivyo ndani ya mwili wake, viko kwa ajili yakumfanyia Mungu ibada. Lakini mara nyingi tumemhuzunisha mmiliki mkuu wa mwili Roho Mtakatifu kwa kutokuvitoa viungo hivi vimwabudu Mungu. Badala yake vimetumika kuziridhisha tamaa za mwili, sawa sawa na kosa alilofanya Adamu na Hawa.
SURA YA SABA
MATUMIZI YA MWILI KATIKA KUABUDU
A: KUABUDU KWA KUTUMIA MIKONO
Kuinua mikono kumetajwa katika Biblia mara 28, Zab134:2 Painulieni mikono yenu patakatifu na kumhimidi Bwana. Katika desturi ya Wayahudi wanaume walipewa kipaumbele katika shughuli, kwa hiyo katika ibada wanaume waliinua mikono walipokuwa wanaomba. Hiyo ni ishara ya kujiachia katika mapenzi ya Mungu ITimotheo 2:8 Tunaona Kanisa la kwanza waliomba huku mikono Imeinuliwa kuonyesha Yesu juu ya msalaba. Zab141:2. Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni. Mikono yako ni Dhabihu, Zab 28:2, ITim 2:8. Bado mkazo wa Wanaume kumwinulia Mungu mikono yao upo, anaposema wanaume inueni mikono yenu mitakatifu, mikono ni kitu kitakatifu mbele za Mungu. Tumia mikono yako kumwabudu Mungu, piga makofi ukimshangilia Mungu kwa nguvu pasipo ulegevu.
B. HUDUMA YA MIKONO
Kwa mikono yako Mungu atakutumia kufanya huduma. Mikono imetumika kubariki Mw 48:14-28, Lawi 16:20-22, Marko 10:16, 16:18-50. Mikono imetumika kuwekwa juu ya watu kwa ajili ya maombi ya uponyaji Yak 5:14-15. Mikono imetumika kumpaka mafuta mgonjwa. mikono inahusika sana katika huduma na kuabudu. Yesu ataitumia mikono yako kuachilia uzima na baraka kwa watu unaowahudumia.
MAONYO
Zab 24:3-4, Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama patakatifu pake. Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, wala hakuapa kwa hila. Isaya 1:15-16. Nanyi mkunjuapo mikono yenu nitaficha macho yanu nisiwaone, na muombapo maombi mengi sitasikia, mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni, ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele ya macho yangu, acheni kutenda mabaya. Mikono iwe safi Math 15:1-20 Ni muhimu kuosha mikono au kuosha moyo, hapa maana halisi ni kujitakasa, mikono yako inauwakilisha moyo.
C: KUABUDU KWA KUCHEZA Zab 150:4. Biblia inaagiza kumsifu Mungu kwa kucheza tukitumia vyombo vya muziki. Kucheza ambako tumeagizwa hakukusudiwa kuwe katika njia za uovu. Bali kucheza kuwe katika hali ya utakatifu kunakomletea Mungu sifa. Kucheza kuonyeshe furaha ya moyo wa Ibada, na kusikokuwa na lengo la kushawishi fikra na hisia za uovu. 2 Sam 6:14-23 Ipo dhana potofu kwamba Daudi alicheza mpaka nguo zikaanguka hilo sio sahihi Ms wa 5 unasema Daudi na nyumba yote ya Israeli wakacheza mbele za Bwana kwa nguvu zao zote. Ndipo tunaona mke wake Ms 20 Mikali binti Sauli akatoka aende kumlaki Daudi ,naye akasema Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo namna gani ,akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake mfano wa watu baradhuri ajifunuavyo mwili wake asipoona haya, Basi Mikali mkewe alimbeza . Daudi akasema, Mikali ilikua mbele za Bwana aliyenichagua mimi juu ya baba yako na juu ya nyumba yake ,ili kuniweka niwe mkuu juu ya watu wa Bwana,juu ya Israeli kwa hiyo , mimi nitacheza mbele za Bwana ,Kisha nitakua hafifu zaidi nami nitakua mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe,lakini kwa wale vijakazi uiiowanena ,kwao nitaheshimiwa Basi Mikali mkewe alipigwa kwa laana ya utasa kwa sababu aliidharau ibada ya mtu wa Mungu maana si kweli kwamba Daudi alicheza mpaka nguo zake zikaanguka. Kucheza lazima kuwe na nidhamu na heshima.
Luka 6:23, Yesu aliwambia wanafunzi wafurahi na kushangilia na kurukaruka – kushangilia ni kupiga kelele, vifijo na nderemo. Mdo 3:1-10 Mtu kiwete alipoponywa alicheza pasipo mpangilio, alicheza na kurukaruka kwa furaha akimtukuza Mungu. Hakucheza kuwashawishi watu wawe na hisia chafu. Furaha ya moyo hujitokeza nje kwa mwili mzima kufurahia. Mhubiri 3:1-4 anasema, Kila jambo kuna wakati wake, wakati wa kuabudu ni wakati wa kucheza siyo wakati wa huzuni.
D: KUABUDU KWA KINYWA AU MIDOMO.
Kiungo cha muhimu sana katika kuabudu ni midomo Josh 1:8 Kitabu cha sheria kisiondoke kinywani mwako- maombi, kusoma neno na kutafakari ni kuabudu Luka 6:45 Moyoni mwa mtu hutoka au kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake. Jaza moyo sifa nazo zitatoka midomoni mwako. Wakati kinywa chako kimejaa sifa, kuabudu na nyimbo za Bwana kwa kinywa chako utaifunua furaha njema ya moyo. Ruhusu NENO liwe katikati ya mtu wa ndani, neno hilo litatoka kinywani mwako kama neno la uzima.
MAONYO
Yak 3:9-10
Hapa tunaonywa kutotumia kinywa kwa kulaani, maana kinywa ni kwa ajili ya sifa kwa Bwana. Acha kutumia kinywa chako kwa maneno machafu na usitumie kinywa kulaani watu. Zab 126:2-6 anasema Mateka waliporejeshwa Sayuni; kinywa kilijaa kicheko na ulimi ulijaa kelele za furaha. Kuabudu lazima kuhusishe mwili, nafsi, na roho yako, yaani mtu mzima. Ibada ni mtu mzima. Paulo anasema anampigia Baba magoti, pia Waeb 13:15 midomo yetu itoe dhabihu ya sifa ambayo ni tunda la sifa tunalotakiwa kumpa Mungu. Je unatoa tunda hilo? Hakikisha una matunda kutoka midomo yako na sifa kinywani mwako. Kinywa ni chombo kikuu cha ibada . Zaburi 141: 3 Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu. Zaburi hii inatushauri tumuombe Bwana alinde vinywa vyetu visitende dhambi.
SURA YA NANE
BIBLIA – MWONGOZO WETU WA IBADA
Biblia ni kitabu cha ibada ambacho kinatupa maelezo ya watu mbalimbali waliomwabudu Mungu kuanzia kitabu cha Mwanzo mpaka Ufunuo. Ukichunguza jinsi walivyofanya ibada zao utagundua wale waliomwabudu Mungu katika kweli na ambao hawakumwabudu katika kweli na tutaona matokeo ya watu hao wote yalikuwa nini.
Hebu angalia mchakato ufuatao na kutathimini aina za ibada zinazokubaliwa na ambazo hazikubaliwi na Mungu. Kusudi la tathmini hii ni kuona makosa waliyofanya, ili na sisi tujisahihishe na kumfanyia Mungu ibada itakayomridhisha na kumbariki na sisi tukabarikiwa.
MCHAKATO WA MIFANO
• Wewe na mimi ni sehemu ya jeshi kubwa la waabuduo kuanzia ibada ya mtu wa kwanza katika Mwanzo 3:8-9, ni vyema tuone mifano ya ibada zao.
• Adamu alikuwa na ushirika na Mungu. Ushirika wowote na Mungu lazima uwe katika mfumo wa ibada, hapa tunaona wakati wa jua kupunga, Mungu alikuja kuwatembelea katika bustani ya Edeni. Hiyo ilikuwa ni ibada ambayo Adamu alimfanyia Mungu na kumwabudu. Ibada ya kweli lazima Mungu awepo. Mwanzo 3:8-9
• Habili na Kaini walimwabudu Mungu kwa kutoa sadaka mazao yao. Kaini hakuabudu katika Roho na kweli bali Habili alipata kibali mbele za Mungu maana alitoa kwa imani. Kibali cha Mungu kwako kitategemea moyo wako ulivyo, Mungu haangalii sura bali anaangalia moyo. Mwanzo 4:4-6
• Henoko alitembea na Mungu. Hii inamaanisha alimwabudu Mungu katika roho na kweli mpaka akanyakuliwa angali hai na kutoweka usoni pa nchi, hii inaonyesha ibada inakuleta mahali alipo Mungu. Mwanzo 5:24
• Abrahamu anahojiana na Mungu katika maombi juu ya mtoto atakayekuwa mrithi wake. Hiyo ni ibada ya kweli. Mwanzo 15:1-4
• Yakobo anamwabudu Mungu akimwomba ulinzi safarini na kumwahidi kumtolea fungu la kumi la kila atakachopata. Ibada ya kweli inauleta moyo kuachilia vyote kwa Mungu. Mwanzo 28:18-22
• Musa alikutana na malaika wa Bwana akavua viatu vyake, maana mahali hapo palikuwa patakatifu sana. Kijiti kiliwaka moto lakini hakikuteketea. Musa alikuwa tayari kumsikia Mungu kwa wito mkuu wa utumishi. Kutoka 3:1-6
• Israel wakiongozwa na Musa wanamsifu Mungu aliyewavusha bahari ya shamu na kuwaokoa kutoka mkono wa mfalme Farao aliyekuwa akiwafuata nyuma awarejeshe Misri. Ibada ya kweli haikosi shukrani. Kutoka 15:20-21
Musa anamwabudu Mungu hemani na akamwona Mungu uso kwa uso hii ni ibada ya ajabu. Kutoka 33:7-11
Walawi 10:1-3 Nadab na Abihu wakaleta moto wa kigeni katika ibada – Mungu hakukubali ibada hiyo wakaliwa na moto wa Mungu wakafa. Hili ni onyo kwamba ibada ni tendo takatifu haipaswi kufanywa kiholela
• Hesabu 18:23-24 Walawi walihudumiwa kwa sadaka na mafungu ya kumi, waliyoleta watu wakati wa ibada. Haipaswi kufanya ibada mikono mitupu lazima umtolee zaka na dhabihu.
• I Nyakati 29:10-13 Mfalme Daudi amsifu Mungu mbele ya makutano ya Israeli Ms10 – 13 Kwa hiyo Daudi akamhimidi Bwana mbele ya mkutano wote naye Daudi akasema, uhimidiwe, ee Bwana, Mungu wa Israeli Baba yetu, milele na milele. Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi, maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako, ufalme ni wako, ee Bwana, nawe umetukuzwa, uu mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe nawe watawala juu ya vyote, na mkononi mwako mna uweza na nguvu tena mkononi mwako mna kuwatukuza nakuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Huu ni Moyo ulio jaa sifa kuu kwa Mungu Mkuu
• Zaburi 146 mpaka150 Zaburi hizi ni za kumsifu Mungu maana zinaanza na Neno “HALELUYA” ambalo lina maana ya Bwana Asifiwe. Zaburi hizi ni nyimbo zinazotakiwa kuimbwa katika ibada zetu na ndivyo zilitumika katika Agano la Kale. Wito: imbeni zaburi katika ibada za Kanisa kwa kubuni sauti .
• Zaburi 147:1-6 Imejaa moyo wa sifa na kuabudu
• Isaya 1:15-17 Nabii anafunua ukweli wa ibada chafu isiyompendeza Mungu ambayo Israeli walikuwa wakifanya
• Isaya 58:5-9 Nabii analia kwa ajili ya upotofu katika kumwabudu Mungu kwa njia isiyo sawasawa na kuwa shauri njia inayofaa kuomba na kufunga. Je kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi? Na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je utasema ni siku ya kufunga na yakukubaliwa na Bwana? Je saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifunguo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuacha huru walioonewa. Je siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako na kuwaleta maskini nyumbani kwako?. Umwonapo mtu aliye uchi umvike nguo wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara na haki yako itakutangulia, utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na Bwana ataitika, utalia, naye atasema mimi hapa. Je una jibu gani mbele za Mungu kwa maswali haya kuhusu saumu, maombi na kufunga na jinsi unavyomwabudu Mungu. Je ndivyo Bwana amekuamuru? Tafakari na utende kama Bwana anavyosema.
• Amosi 5:21-27 Yeremia 14:11-15-19 Haya ni maonyo ya kusikiliza manabii wa uongo na kuyatii maneno yao kwa kudhania wametumwa na Mungu na kupelekea kujihudhurisha katika ibada zao na kuabudu. Mungu hata sikiliza ibada hizo ni machukizo matupu. Ibada hizo hazifai
• Luka 1:67-79 Luka 1:46-55 Kuhani Zakaria anamsifu Mungu kwa ukombozi wa Israeli na wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake. Mariamu anamwimbia wimbo wa sifa Bwana Mungu mwokozi wake.
• Luka 2:2, 13-14 Jeshi la malaika wengi lamsifu Mungu mbinguni wakati wa tangazo la kuzaliwa kwa Mwokozi wa ulimwengu – YESU. Hii ni sifa inayompa Mungu utukufu.
• Mathayo 2:2 Mamajusi wa Mashariki walisafiri maili nyingi kwenda Bethlehemu ili wamsujudu na kumwabudu mtoto Yesu aliyezaliwa mjini mwa Daudi, na kumtolea dhabihu zao. Ibada ni pamoja na kutoa gharama ya muda na mali zetu
• Luka 24:52-53 Wanafunzi walipoabudu wakapanda Yerusalemu wenye furaha kuu. Ibada huleta furaha na tofauti maishani.
• Ufunuo 4:5-11, 5:9-13 Viumbe wenye uhai, wazee 24 na malaika wanaabudu Mungu mchana na usiku wakisema: Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu Mungu aliyekuweko, aliyeko na atakayekuwepo. Ibada ni kumtambua Mungu ni nani na kumpa sifa za umilele.
Naamini mifano hii itakupa changamoto na mvuto katika mwanga mpya wa mtazamo wa kibiblia katika maisha yako ya ibada, na kujiunga na watakatifu wa vizazi vilivyopita na kizazi chetu, kumwabudu Mungu katika roho na kweli, na Utakatifu, na nguvu, na Utukufu hata milele.
Ningependa ufahamu kwamba kuabudu:-
a. Ni shughuli inayofanywa na mtu mwenye akili timamu na, ufahamu kamili na hekima ya kweli katika Neno.
b. Kunahitaji Uongozi wa ki-Mungu na hasa Roho Mtakatifu ili usitumbukie katika udanganyifu, hila za shetani, kwa kujichanganya na waabuduo shetani na miungu na ibada tupu.
c. Kunahitaji kujitenga na mambo yote ya kipagani na utu wa kale, na kuweka kando udini.
d. Ni uamuzi wa dhati usiorudi nyuma kuangalia mazingira, vikwazo na heshima yako, bali kusudi la moyo wenye njaa na kiu ya kumtaka Mungu.
e. Ni shughuli inayokuletea furaha ya kweli na ya kudumu katika mazingira yote.
f. Ni njia inayokuwezesha kumwona mwana wa Mungu katika uhalisia wake kama alivyokuwa na wanafunzi wake miaka 2000 iliyopita na alivyo sasa katika utukufu wake.
g. Ni pamoja na kumpa Mungu kile kilicho bora kabisa maishani mwako ukianzia na moyo wako, roho yako, akili zako, na nguvu zako, pamoja na mali zako.
Nami nakutakia ufanisi wa ibada zako mbele za Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo, Waebrania 13:20-21 Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji mkuu wa kondoo, kwa damu ya Agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye nyinyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo, utukufu una yeye milele na milele. Amina ,Sasa tafakari ibada zako je unazifanya kwa mujibu wa Neno la Mungu.
SURA YA TISA
ZANA ZA MUZIKI KATIKA SIFA NA IBADA
a) Uchunguzi katika maandiko
b) Angalizo kwa wana Muziki
Katika ibada ya kweli iliyoendeshwa na watumishi wa Mungu katika agano la kale vyombo vya muziki vilitumika. Biblia inatoa mkazo mkubwa sana kutumia zana za muziki katika ibada. Mapema kabisa katika sura ya 4:21 Mwanzo, tunaona andiko linalosema kuhusu vyombo, unaweza kuona vyombo vya muziki ni kitu cha zamani sana katika harakati za mwanadamu na muziki.
a) Uchunguzi katika maandiko
Kutoka 15:1-21 Mariamu na wana wa Israeli waliimba kwa matari katika
kusherehekea muujiza wa kuvuka bahari ya shamu.
ISamweli 16:23 Daudi alipiga kinubi mbele ya Sauli na roho mbaya ikamwacha Sauli, hakuomba bali alipiga kinubi roho mbaya ikatoka kwa Sauli. Sauti nzuri yaweza kumtoa nyoka pangoni. Huo ni ukweli hata leo, unaweza kutoa roho mbaya kwa watu kwa njia ya kinubi
2 Nya. 5:11-14 Walawi walisimama hekaluni wenye matoazi, vinanda na
vinubi katika ibada ya kuweka wakfu hekalu hapo tunaona kitu cha ziada au sifa walikuwa wamefundishwa, wamejiweka wakfu, wana ujuzi, walikuwa na umoja, wamejiandaa, wamevaa sare, wako nadhifu.
2Nyak20:13.24-28 Mfalme akawaweka watakaomwimbia Bwana, wakaimba na kusifu na Bwana akawapiga maadui zao, wakafika Yerusalemu wenye vinubi, vinanda, na mapanda kwenda hekaluni. Hili ni jeshi linaloongozwa na kwaya. Bunduki zao zilikuwa vinanda, vinubi, zeze, tarumbeta. Hata leo vyombo vya muziki vina nguvu katika ibada, na vinaweza kuporomosha jeshi la shetani linalotukabili.
2 Nyak.29:25-30, 5-12 Ibada nzito ilifanywa na mfalme Hezekia baada yakulisafisha hekalu nakurejesha upya sadaka za kuteketezwa ambazo waliacha kutoa. Hapo tunaona wimbo wa Bwana unaimbwa kwa mapanda na vinanda ulikuwa wakati wa uamsho wa ibada ya kiroho.
Yoshua 6.1-20 Mji wa Yeriko ulikuwa na kuta nene zilizo uzunguka ,ulikuwa umefungwa kabisa kwa hofu ya Israeli ili wasingie.Lakini Bwana alimwambia Yoshua atwae tarumbeta saba na makuhani saba ,wauzunguke mji wa Yeriko mara moja kila siku na wenye silaha wawe mbele ya makuhani saba wapige tarumbeta.Siku ya saba wazunguke mji mara saba na ule mzunguko wa saba makuhani wapige tarumbeta zao , wakafanya hivyo, ndipo watu wote wakapiga kelele kuu na mji wa Y eriko ukaanguka kabisa na Israeli wakauteka .Iko siri ya nguvu kuu ya ajabu katika sifa zinazo ambatana na sauti za zana za muziki kiasi cha mji wenye kuta Yeriko ukaanguka.Sifa za muziki zinafungua milango aliyoifunga shetani na kuteka mateka watu waliofungiwa ndani ya vifungo wawe milki ya Bwana.
Neh.12:27-43 Wakati wa ujenzi wa ukuta wa Yerusalemu waimbaji 245 walishiriki kuimba na kumsifu Mungu, bila shaka walikuwa na zana za muziki.
Zab. 1-150 Imejaa zana mbalimbali za muziki zilizotumika kama ifuatavyo:-
– Zaburi 1-41 Kuabudu na kumpenda Mungu
– Zaburi 42-72 Kuabudu na kumshangaa Mungu
– Zaburi 73-89 Ibada ya vizazi vyote
– Zaburi 90-106 Ibada ya mamlaka
– Zaburi 106-150 Ibada ya kukubalika
Zab 33:1-3 na Zab 150:3-6 Tunapewa agizo la kumsifu Mungu kwa vyombo mbalimbali vya muziki, vinanda vya nyuzi kumi. Tunahimizwa tuvipige kwa ustadi na siyo kwa ulegevu au kwa kuburunda, ni lazima tujifunze kuvitumia vyombo vya muziki, na hasa katika kizazi chetu ambapo tuna vyombo vya kisasa vilivyo bora kuliko wakati wa mfalme Daudi na Mwalimu Mkuu Asafu
Asili ya vyombo vya muziki si shetani, bali ni Mungu Ezekiel 28:11-13 Lusifa (shetani) aliumbwa akiwa na vinanda ndani yake ili amsifu Mungu. Uwezo huo wa kuwa na vinanda ndani yake ni wa Mungu. Katika kitabu cha ufunuo tunaona shughuli za ibada zinapewa uzito mkubwa sana, na ibada hizo zinaongozwa na malaika wenye vyombo vya hali ya juu sana na kila shughuli inakwenda sambamba na muziki
? Ufunuo 5:8-9 Wazee 24 Wana vinubi wakiimba wimbo mpya mbele za kiti cha Enzi wakiabudu.
? Ufunuo 8:1-2 Malaika wakapewa baragumu saba. Hizi baragumu zinapigwa sambamba na hukumu ya Mungu kwa ulimwengu wakati wa dhiki kuu
? Ufunuo 14:1-3 Sauti ya wapiga vinubi yasikika mbinguni, Yesu akiwa na watu 144.000 wenye muhuri wa Mungu
? Ufunuo 15:2-4 Wale walioshinda kutoka katika dhiki kuu wenye vinubi vya MUNGU wanaonekana wakifanya ibada kando ya bahari ya kioo – mbele za Mwanakodoo wakiimba.
? Ufunuo 18:22-23 Mfumo mwovu wa shetani umebadili matumizi matakatifu ya vyombo vya muziki na kuwa silaha yake. Kwa kuvitumia katika starehe na uovu mwingi. Shetani Ni mwizi lakini tusifuatishe wala kuigiza namna ya dunia, Mungu bado hajafilisika. Tukiomba atatupa ubunifu wa miziki ya Kiroho iliyo mitakatifu na yenye vionjo vya mbinguni.
? I Thesalonike 4:16 Malaika Mkuu atapiga parapanda ya Mungu, ndipo kwa sauti hiyo wafu walioko makaburini waliokufa katika Yesu wataisikia, maana ina uhai wa kufufua miili iliyokufa. Sauti ya parapanda ina uwezo wa kubeba mamilioni ya watu walioko duniani na kuwapandisha (kuwanyakua) mpaka hewani atakapokuwepo Yesu naye atawalaki katika mirindimo hiyo hiyo ya parapanda.
Leo sauti za vinubi, vinanda, zina uwezo huo huo ndani ya Kanisa la Kristo lenye kujali ibada ya Mungu kama ilivyokuwa tangu asili. Ni lazima Kanisa limwabudu Mungu kwa vinubi, matoazi, zeze, vinanda, parapanda na matari. Hiyo haikwepeki, maana hiyo ndiyo asili ya ibada ya kiroho.
Daudi alitengeneza vyombo hivyo na kuwapa walawi wavitumie Hekaluni, akina Daudi wa leo wapo Walawi wapo waimbaji wapo, basi tumfanyie Bwana ibada tukiwa na zana za muziki. Ulimwengu umefika mbali katika swala la muziki. Je Kanisa tuko wapi? Nani awe bora na apendeze zaidi. Ili tuwe bora kila mtu atoe mchango wake wa vyombo ili Bwana atukuzwe katika sifa. Kanisa lijitahidi iwezekanavyo kupata vyombo vya ibada. 1Kor 14:6-8 Paulo anaelezea umuhimu wa vyombo mbalimbali katika kuboresha sauti za nyimbo zetu kila zana ina aina ya sauti yake na kuleta tofauti inayoboresha wimbo, kwa kuwa utamu wa sauti za vyombo unaleta usikivu mzuri na fahari kwa wanaosikia na utukufu kwa Mungu.
B) Angalizo kwa wana Muziki
Bila shaka Mungu anabarikiwa sana na sauti za vyombo vya muziki unaopigwa kwa ustadi na mwana muziki aliyejaa Moyo wa Sifa. Kwa hiyo wapigaji wa vyombo wanapaswa wajitunze katika usafi wa Roho na Mwili kama watumishi watakaotoa hesabu yao mbele ya Kristo. Inawapasa kukataa aina yote ya sifa na kiburi, bali wawe wanyenyekevu na wa pole mbele ya uongozi kama kwa Bwana mwenyewe. Wasiotegemea ujuzi wao bali maombi na Roho Mtakatifu apewe nafasi kubwa katika huduma yao.
Muziki una mvuto wa nguvu kumnasa mtu katika majaribu na kumharibu pasipo yeye mwenyewe kufahamu. Hivyo ni vyema kila mwanamuziki ajiweke wakfu kwa Bwana na kutaka nguvu za Roho Mtakatifu katika huduma yake, Ili akwepe mitego na hila pamoja na tamaa za mwili zilizo karibu naye.
Lusifa alianguka baada ya kutukuka sana katika huduma ya sifa mbele za Mungu, maana alikuwa na vinanda mwilini mwake alivyotumia kumsifu Mungu kwa ustadi wa hali ya juu sana, kiasi kwamba malaika wote walimsikiliza na kutii alichosema katika ibada yao kwa Mungu. Uovu ukapata mwanya hapo na akataka kuwa kama Mungu ili aabudiwe, mara moja akatupwa chini. Jambo hili linapaswa kuzingatiwa sana na kila mwanamuziki lisimpate. Fahamu Roho ya Lusifa inavizia kuwanasa wanamuziki na kuwangamiza.
SURA YA KUMI
NAFASI YA KWAYA KATIKA IBADA
1. KILA MTU AIMBE
Ni muhimu kila mwamini ajue kuimba nakumsifu Mungu kwa midomo yake, kusifu nakuabudu si kwa watu Fulani au kundi maalumu tu. Bali uimbaji ni wajibu wa kila mtu ndani ya ibada. Ni muhimu iwepo tahadhari kwa kanisa kutojisahau jukumu la kuimba kuiachia kwaya na wengine wakawa wasikilizaji na watazamaji, hilo ni jambo la hatari na ni anguko mbele za Mungu. Kanisa lidumu katika sifa daima kwa ujumla.
2. KWAYA NI NJEMA
KWAYA: Ni chombo chema sana ndani ya ushirika. Kama tunavyoona katika neno la Mungu INyak 16:4 INyak 23:30, IINyak 5:12-14 Haya ni maandiko yanayoelezea huduma ya kwaya katika ibada ilivyo muhimu. INyak 16:4-7 Walawi walitengwa wamtumikie Bwana katika kumkumbusha Mungu nakutoa shukrani na sifa. Asafu alikuwa kiongozi mkuu wa huduma hii hekaluni INyak 23:30-31 Kazi ya kwaya ilikuwa ni kutoa huduma ya sifa na shukrani katika ibada ya asubuhi na jioni kila siku hekaluni. Ratiba hii ya huduma inatakiwa idumishwe hata leo. Ni makosa kudhani kwamba kwaya ni ya siku maalum ama Jumapili tu, kwaya ipewe kuhudumu katika kila ibada.
IINyak 5:12-14. Waimbaji walibaki ndani ya hekalu wakiwa na roho moja, wakiimba sauti zao kwa mpangilio, wakimsifu na kumshukuru Mungu, na kuimba sambamba na muziki wa vyombo wakimsifu Bwana kwa wema na fadhili zake. Hekalu likajawa na utukufu wa Mungu, wingu la uwepo wa Mungu likawafunika. Huduma ya kwaya ni muhimu kama tunavyoona hapo juu, kushusha uwepo wa Mungu na kuliongoza kanisa kumsifu nakumshukuru Mungu kwa wema wake.
Hii inamaanisha kwaya ina jukumu la kutoa huduma ya sifa na shukrani, na kutunga nyimbo zenye mfumo huo bila kusahau utakatifu wa maisha yao. Utunzi wa nyimbo uzingatie maadili ya kiroho, neno, mazingira, mahitaji ya kijamii, ubora wa mashairi, usanifu wa kitaaluma, Uongozi wa Roho Mtakatifu. Si vema kuibuka na wimbo usiku mmoja na kuutumbukiza katika huduma. Wimbo unaweza kuutunga kwa muda mfupi ama kwa muda mrefu kutegemeana na kuridhika kwako ukizingatia hayo yaliyo tajwa hapo juu.
Ni jambo muhimu pawepo na maongozi makini katika kwaya kama Asafu alivyoongoza kwaya ya hekalu. Kwaya ni huduma haipaswi kuongozwa kwa mfumo wa kisiasa (kupiga kura) bali kwa mfumo wa huduma na malengo ya kihuduma na hasa kumtukuza Mungu ambapo kiongozi mkuu ni yule aliye na maono, na mbeba huduma ambaye ni mwalimu. Mwalimu ni kiongozi Mkuu wa kwaya kwa mujibu wa maandiko.
Uongozi wa aina hiyo pamoja na kamati zake utaendeleza huduma kama ilivyo katika neno. Mwalimu hapaswi kupigiwa kura bali anakuwa mwalimu kwa kipawa alichopewa na Mungu, hicho ndicho kinampa nafasi ya kuwa kiongozi wa kwaya. Kila kanisa la mahali pamoja lizingatie kwa makini kulea vipawa na kuwatambua Walawi (waimbaji) waliopo kanisani na kuwasimika katika huduma hiyo kama mfalme Daudi alivyofanya INyak 16:1-7. Mchungaji awe karibu sana na kwaya katika utendaji wa siku kwa siku ili kudumisha mshikamano wa huduma yake na kwaya na kanisa, na kutoa msaada matatizo yanapotokea.
3. ITEGEMEZE KWAYA
Kanisa zima liwe mdau mkuu wa kutegemeza kwaya kwa hali na mali ili iweze kusonga mbele katika fani ya uimbaji pasipo kukwama. Kumbuka asilimia sabini na tano ya shughuli za kanisa katika ibada ni kusifu (kuimba), kwa hiyo ni jambo jema wakristo wakawekeza nguvu zao katika kwaya ya kanisa. Kwaya zenye mafanikio ni zile ambazo nyuma yao iko nguvu ya kanisa kwa hali na mali, na maombezi.
Nimeshuhudia katika huduma hii, ambayo nimetumikia miaka 30, Mungu akiwabariki watu kiroho na kimwili kupitia huduma ya kwaya. Nimeona Mungu akiliongeza kanisa kiidadi toka washirika 250 mpaka washirika 2000 kupitia huduma hii ya kwaya. Nimeona watu wakiokoka mahali mahali kwa nyimbo zenye upako na kuponywa magonjwa yao wengine wakiwa hospitalini, kanisani, na majumbani kwa kusikiliza nyimbo za kwaya niliyokuwa na hudumu nayo nikiwa mwalimu.
Mara mbili tukiwa madhabahuni Dar es Salaam na kule Nairobi Kenya katika huduma, Roho alishuka katika ibada na watu wote walishindwa kuendelea kutusikiliza na kujikuta wameanguka chini wakimwabudu Mungu katika Roho, huku wakinena kwa lugha, na huduma ya unabii ikaanza kufanya kazi kupitia kwa mama mmoja wa kizungu aliyekuwepo katika ibada hiyo, kiasi kwamba Mchungaji alikosa neno la nyongeza na kuahirisha ibada maana watu tayari wamehudumiwa na Mungu kupitia kwaya.
Kwaya ina mvuto wa ajabu kwa watu, katika matukio mbalimbali ya kijamii. Kwa hiyo ni vema ipewe nafasi ya kutoa huduma katika matukio hayo, kama vile mikutano, semina , misiba, harusi , sherehe za kanisa na za kijamii maadamu kinachofanyika hakipingani na imani yetu na hakimdhalilishi Yesu. Matukio ni uwanja mzuri kwa kwaya kumhubiri Yesu kupitia ujumbe wa nyimbo. Kama Kanisa litailea kwaya vizuri litavuna matunda ya baraka yasiyo na kifani.
4. MAFUNZO NI MUHIMU
Kanisa liimarishe na kufanya juhudi za makusudi kuwawezesha waimbaji wote kwa kuwapa mafunzo ya kusifu na kuabudu katika Roho na kweli, na kuhakikisha waimbaji wana viwango vya uimbaji vinavyokubalika. Ibada ni kitu kitakatifu ambacho kinatakiwa kufanyika kwa utaratibu, hofu na unyenyekevu na kwa tahadhari kubwa ili kumpa Mungu heshima inayomstahili, kwa kila tendo na dhamira ya moyo iliyo safi. Utaratibu huu ulikuwepo katika ibada ya Agano la kale na unapaswa kuendelezwa katika kanisa la leo.
INyak 25:6-8, Zab 33:1-2 Kila mwimbaji wa sifa na kwaya lazima ajue kwamba huduma hii iko moyoni mwa Mungu, maana yeye amezungukwa na viumbe pamoja na malaika milioni nyingi wanaomwabudu mchana na usiku Uf 5:7-14. Hivyo ni vema kufanya huduma hii kwa kicho na kujitoa kwa dhati katika unyenyekevu wote, kwa bidii, na ustadi wa hali ya juu. Ni vibaya kufanya huduma hii kwa lengo binafsi, ama manufaa mengine mbali na kusudi la kumwadhimisha Mungu.
5. ANGALIZO KWA MWANAKWAYA
Ni jambo la muhimu kwa mwanakwaya na muimbaji wa sifa aelewe kwamba, Mungu pekee ndiye anayestahili kupewa sifa na kuinuliwa katika huduma hiyo. Muimbaji ajitambue kwamba ni chombo cha sifa kwa Bwana, kwa hiyo achunge sana kipawa hicho kisitumike kwa Bwana mwingine. Nasema hayo baada ya kuona waimbaji wengi walioinuka na kuwa juu, hawashikiki, hawaambiliki na kufunikwa na roho ya kiburi.
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba, waimbaji wazuri waliotamba katika majukwaa ya injili kwa kipawa cha uimbaji, leo wako katika majukwaa ya shetani wakitumia kipawa hicho hicho kumsifu shetani. Usisahau kwamba Mungu aliyekuita katika huduma siku moja atakutaka utoe hesabu ya utumishi wako, 2Wak 5:10. Ndipo ule wimbo wa zamani unaosema “Kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe mbele za Mungu, na kumalizia kwa maneno, SIKU HIYO INAKUJA” utakuwa halisi.
Simama na huduma mtu yeyote asikunyang’anye taji yako. Ukifahamu huduma hii ni huduma ya mbinguni, wewe ni mtu unayeheshimiwa sana na Bwana, maana Bwana anakaa katika SIFA. Jivunie heshima hii, jiendeleze, na kutumika bila masharti kwa utukufu wa Mungu.
MFANO ULIO HAI.
MZEE AMULIKE MWAKITEKA
Mzee Amulike Mwakiteka ni mtumishi wa Mungu tangu miaka ya 1950,Mungu alimwita maalum kwa huduma ya uimbaji katika kanisa la Assemblies of God. Huduma yake ilipata mpenyo mkubwa sana sehemu za nyanda za juu kusini mwa Tanzania . Mungu alimwinua sana kiasi kwamba kwaya aliyo kua anaiongoza ilijulikana kwa jina la kwaya ya moto,nakila wakati Mzee huyu aliposimama kuhudumu nguvu za Mungu zilionekana na watu walibarikiwa kwa huduma hiyo.
Hatimaye huduma yake ilivuka mipaka ya mikoa ya kusini na kuenea nchi nzima ,mikoa ya Kigoma ,Mwaza, Arusha, Tanga,na Dar es Salaam.Kutokana na umahili wake katika uimbaji alipata umaarufu ndani na nje ya Kanisa na kupelekea viongozi wa kisiasa kumuomba ajiunge na chama chao ili awasaidie kuhamasisha siasa ndani ya chama chao kwa njia ya nyimbo zake.
Mzee Amulike Mwakiteka hakukubaliana na ombi hilo ,akawambia viongozi hao wa kisiasa kwamba wito wake ni kumwimbia Mungu tu na si vinginevyo. Jambo hili lilifanya watu wamshangae na kumcheka,maana kuwa mwimbaji wa nyimbo za siasa kungelimnufaisha sana kimapato maana aliahidiwa kulipwa pesa nyingi ,lakini hakuweza kushawishiwa na mshahara mkubwa kuliko kumtumikia Mungu wake. Watu walisema mzee huyu ameutema mkate mdomoni mwake natazama hali yake bado inendelea kuwa duni.Mtumishi wa Mungu Amulike Mwakiteka ameendelea kumtumikia Mungu katika huduma ya uimbaji,pia ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT huko Rungwe Mwakaleli akiwa na umri wa miaka 82 bila kukata tamaa.
Mwimbaji ni chombo kitakatifu cha Bwana ,Mfalme Daudi alifahamu vyema jambo hilo akachukua hatua ya kuwaweka WAIMBAJI WAKFU MADHABAHUNI pa Bwana kuonesha kwamba wametengwa rasmi kwa huduma hiyo.
Mwaka wa 1991 nilipokuwa naendesha semina ya sifa na kuabudu katika kanisa la TAG Chunya Mbeya, Mchungaji Mwabwanga aliyekuwa makamu askofu mkuu wa TAG aliniuliza je katika huduma hii unayofanya uliwahi kuwekewa mikono ,akimaanisha kufanyiwa maombi rasmi ya kuwekwa wakfu kwa huduma hiyo , nikamwambia sijawahi kufanyiwa maombi kama hayo.Ndipo mzee Mwabwanga akasema unapaswa kuwekwa wakfu mbele za Bwana maana hii ni huduma takatifu.Kwahiyo nikapata nafasi ya kuwekwa wakfu kwa maombezi ya mtumishi wa Mungu huyo mbele ya mchungaji mwenyeji na kanisa zima,tangu hapo mimi ni mpakwa mafuta wa Bwana kwa huduma hiyo.
Ikumbukwe kwamba Mungu hakukubaliana na mfalme Belishaza alipovitumia vyombo vitakatifu vilivyotwaliwa kutoka Hekalu la Yerusalemu na baba yake Nebukadreza. Hebu angalia Mungu alivyochukizwa na jambo hilo. Danieli 5.22—28Na wewe mwanawe, Ee Belishaza hukujinyenyekeza moyo wako ,ijapokuwa ulijua hayo yote, Bali umejiinua juu ya Bwana wa Mbingu nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako na wewe ,na wakuu wako na wake zako na masuria wako mmevinywea nawe umeisifu miungu ya fedha nay a dhahabu nay a shaba nay a chuma na mti nay a mawe wasioona wala kusikia wala kujua neno lolote,na Mungu yule ambae pumzi yako ii mkononi mwake ,na njia zako zote ni zake hukumtukuza .Ndipo kile kitangaa cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake na maandiko haya yameandikwa , MENE MENE,TEKELI NA PERESI. Na tafsiri ya maneno haya ni hii, MENE . Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha ,TEKELI, Umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka, PERESI Ufalme wako umegawanyika nao wamepewa Waamedi na Waajemi.
Haya ni maonyo makali kwa mtu ambaye anakitumia chombo cha Mungu kinyume na matumizi yake,hivyo hivyo Mungu hayuko tayari kuona vipawa alivyotupa vinatumika hovyo mbali na kusudi la huduma hii,maana mafuta tuliopewa sio ya kisiasa wala burudani.Ni muhimu kuwa na unyenyekevu na heshima na kujiepusha na kitu chochote kinachokuondoa katika utumishi wako kwa Mungu .Linda sana ulicho nacho na wito wako mtu asikunyanganye.
Mambo yaliyompata mfalme Belishaza baada ya kuvitumia vyombo vya Bwana vibaya katika msitari wa 30 unasema,usiku huo huo akafa.Hii ni hatari inayomkabili mtumishi yeyote anayekiuka kutumia vibaya kipawa na karama aliopewa na Bwana .Kwahiyo kila mwimbaji wa sifa ambaye amepakwa mafuta na Mungu ni chombo cha Bwana hapaswi kutumia kipawa chake nje ya huduma ya Mungu.
SURA YA KUMI NA MOJA
KANISA NA KIZAZI KIPYA
a) NJIA PANDA
Kanisa la leo lipo katika njia ya panda likipambana na mabadiliko ya mitazamo katika maadili ya kiroho, haya yamelikumba Kanisa kutokana na utandawazi uliopo duniani, katika Nyanja mbalimbali za maisha na kupelekea kujichanganya katika suala zima la jinsi ya kuabudu na kusifu, na kuathiri vijana wetu ambao ni kizazi kipya. Ipo hatari ya kupoteza dhana ya kusifu na kuabudu kama Biblia inavyofundisha kutokana na utandawazi huo, Kanisa likajikuta linaabudu na kusifu kinyume na maandiko, maana hali ya utandawazi uliopo unawapa vijana uhuru wa kuabudu bila mipaka, ya kujua nini kifanyike na nini kisifanyike.
Watu wako huru kufanya lolote mradi kufanya hivyo ni tendo la ibada na linafanywa kanisani kwa ajili ya Mungu. Mimi nikiwa mdau mkubwa wa huduma hii ya sifa na kuabudu, Nimeshuhudia na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya Nyimbo za Injili na uimbaji wa sifa makanisani, (madhehebu) kuanzia kanisa la RC, KKKT, Moravian, Anglicana, TAG, na makanisa ya Kipentekoste yote, na huduma zote kwa muda wa miongo miwili.
Katika uchunguzi wangu nimegundua kwamba makanisa yamebadilika kutoka aina ya ibada yalizokuwa nazo na kuvutwa na wimbi la utandawazi, na kuathiri kwa kiasi kikubwa vionjo vya sifa na ibada ya Kibiblia.
Maaskofu, wachungaji na wakristo kwa ujumla tumenyamaza na tumekubali nakuridhika na vionjo hivi vya kizazi kipya, na kuendelea na ibada za namna hii pasipo kushtuka wala kukemea. Vionjo hivi vipo katika aina nyingi na maeneo mengi na kutumika katika ibada zetu.
Kwa mafano:
I. Kucheza kwa nguvu sana bila kujali jinsia, na viungo vya mwili ambavyo haifai kuvichezesha, na kunengua viuno kadiri iwezekanavyo bila kujali muonekano wa mchezaji. Na bila kujali ujumbe wa wimbo unahitaji ishara, tendo, mchezo wa aina gani,ili kukaza ujumbe, bali lililo kubwa kwao ni kucheza tu ili kuwafurahisha watu na kuwaburudisha kisha kujipatia umaarufu na fedha.
II. Miundo ya sauti za kuimba na mitindo ya upigaji wa zana za muziki, imejaa vionjo visivyoendana na uzuri wa utakatifu bali utu wa kale na udunia, umetawala majukwaa na kupata mashabiki lukuki ndani ya kanisa.
III. Mavazi yanayovaliwa na wanakwaya wetu, na viongozi wa sifa, yanashawishi na kuvuta mawazo ya mtu kufikiri maovu, na muonekano mzima kuwa kinyume na mwabuduo wa kweli, na yamepata kibali na meza kuu ya kanisa na kuvuta hisia za watu kinyume na lengo lililowaleta kuwepo hapo ,na kupandikiza dhana potofu dhidi ya uimbaji wa kikristo.
IV. Ujumbe wa nyimbo umekosa viina vya maadili ya kiroho, lugha na maneno ya heshima kwa Mungu hayapo katika ujumbe wa nyimbo hizo, na hivyo kushusha hadhi ya kanisa, na kuwa sawa na kuwepo katika majumba ya starehe na burudani.
V. Kuto kuwapa maonyo waimbaji binafsi, wanaposhiriki na wasioamini katika kuandaa album zao, na kuimba pamoja nao katika makongamano,na kuzama mno katika injili ya biashara na uchumi. Yanalipaka matope kanisa na kumnadi Yesu katika soko la imani kwa bei rahisi, na kuharibu kabisa lengo la kumhubiri Yesu kwa njia ya nyimbo.
VI.Matamasha ya kusifu na kuabudu yamepoteza maana hiyo na kugeuzwa
miradi ya kiuchumi na burudani na maonyesho ya mitindo ya sanaa na
sio sifa na kuabudu kwa Mungu.
Najua haya yanafanywa na wasanii hawa kwa uhuru namna hiyo kwa madai mazito kwamba hayo ni haki yao, na sehemu ya ibada aliyowaibia shetani. Sasa wanayarejesha ndani ya kanisa. Haya ni madai ya ajabu sana. Huyu shetani aliyeiba na kuyaibua tena hapa duniani akiwa mwasi, je anapayaibua yanabaki kuwa mazuri na matakatifu? shetani ni adui wa Mungu je atakaa na kitu hicho kikiwa salama na safi? si kweli, lazima atakinajisi na kukitemea mate na kukivuruga kabisa. Tusidanganyike, miziki, na michezo na mitindo hiyo inatoka kuzimu ikiwa imevuviwa na kunajisiwa na shetani kwa lengo la kuangamiza ulimwengu na kanisa.
Si vema kuikumbatia na kuitumia mitindo hiyo katika ibada na kwaya pia. Kufanya hivyo ni kubeba virusi vyenye sumu ya shetani na kuvipandikiza kanisani.naweza kusema sifa na kuabudu kumeingliwa na virusi vibaya.
Mimi nimekuwa mwalimu wa kwaya na mwanzilishi wa michezo ya kwaya hapa nchini. Mnamo miaka ya 1990 kurudi nyuma hapakuwepo na kwaya au kanisa lililokuwa linafanya ibada na kwaya kwa kucheza nakufanya sarakasi kama za leo. Tuliimba na kusifu tukiwa tumesimama ama tumekaa huku tukipiga makofi tukiwa na ngoma, vinanda na gitaa na vifaa vingine vya muziki. Uwepo wa Mungu ulishuka na Baraka zilikuwepo. Na madhabahu ya Mungu iliheshimiwa na kanisa lilitakaswa kwa hofu na kutetemeka.
Watu walijaa furaha ya Bwana isiyoingiliana na furaha inayotokana na kusisimuliwa na vituko vya kurukaruka na kuinama. Furaha ilianzia moyoni mwa mtu kwa kuguswa na nguvu za sifa iliyojitokeza nje kwa mtu kujaa Roho Mtakatifu, na kunena kwa lugha, na kicheko kitakatifu. Mambo haya yamekuwa adimu sana katika ibada zetu za leo.
b) MABADILIKO YAANZA.
Miaka ya 1986 -1990 na kuendelea nchi yetu ilikuwa inapitia katika uamsho na mlipuko wa Injili chini ya huduma ya “The Big November Crusade”. Mikutano hii iliwaleta maelfu kwa Yesu. Huduma ya kwaya ilichangia sana ufanisi wa mikutano hii kuleta matunda ya watu kumpa Yesu maisha yao.
Kwa vile kwaya zilihusika sana katika mikutano hii yenye mvuto wa umati wa watu, Mungu alitupa maono ya kuwavuta watu kupitia vitendo (steps) vilivyokaza ujumbe wa nyimbo tulizoimba mbele ya umati huo. Kila neno tulilotamka katika wimbo lilipewa ishara ya tendo kwa mikono, au miguu, macho au kucheza mchezo jukwaani kwa baadhi ya waimbaji wakati wimbo ukiendelea.
Kamwe hatukufanya tendo, ishara nje ya ujumbe wa wimbo, na dhamira yetu haikuwa kuburudisha wala kufurahisha watu au kujipatia umaarufu wa jina, bali kuipeleka injili ya Yesu kwa mwenye dhambi kikamilifu ili aokolewe. Ingawa watu walifurahi na kucheza, mwisho walikamatwa na Yesu na kuokoka. Huduma hii ilibuniwa na Victory Singers, kwaya ya Kanisa la TAG Kinondoni Dar es Salaam, ikavuma na kuigwa na kwaya, vikundi, na watu binafsi, kila mahali na mpaka leo michezo hiyo imevuka mipaka na lengo tulilokuwa nalo sisi waasisi.Ni muhimu maono yaende pamoja na maarifa.bila maarifa upo uwezekano kutoka nje ya maono na kupotea.
Kitu kinachoendelea leo ndani ya uimbaji ni kipya, japokuwa kina mizizi kutoka kwa waasisi, Mimi kama mwasisi nawaomba waimbaji wote turudi mahali petu pa kwanza, tumwabudu Mungu katika roho na kweli, tusikubali kujifananisha na dunia bali tugeuzwe upya nia zetu na kuitoa miili yetu (michezo iliyovuka mipaka isitishwe) kwa Mungu, hii ndiyo ibada yetu yenye maana ya kumpendeza Mungu. Rum 12:1-2
Japokuwa mjadala huu ni mkali na hoja nyingi zipo kutetea ibada za aina hii kwamba kwaya ziendelee, ukweli unabaki palepale kwamba Mungu wetu anaabudiwa katika Roho na Kweli na Mungu ni wa utaratibu. Bado mtume Paulo anaonya akisema: Lolote mfanyalo kwa Neno au kwa tendo fanyeni kama kwa Bwana kiasi kwamba tunapewa onyo hata katika masuala ya kula, asemapo Basi, mlapo au mnywapo au mtendapo neno lolote fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu IKor 10:31, Kol 3:17
Je sarakasi hizi zinazofanywa wakati wa huduma zinampa Mungu utukufu? Ukweli hazimpi Mungu utukufu. Je tuendelee kuzikumbatia sarakasi hizi kwa vile zinavuta umati wa watu? Nilazima tuelewe kizazi hiki kitaibuka na wokovu chotara kama hatuta acha. Mungu hana wokovu na Ukristo chotara bali analitaka kanisa lisilo na kunyanzi, safi bila doa wala mawaa. Waef 5: 26 – 27, Hali ya Kanisa la leo ni mbaya ,lina ugonjwa wa UKIRO ambao ni ugonjwa wa UPUNGUFU WA KINGA ROHONI,kama ukimwi usivyo na dawa ,hivyo ndivyo na Kanisa liko katika hatari ya kukosa dawa ya kuponya UKIRO,Kanisa linahitaji maombi ya kulia kama nabii Habakuki ,Ee Bwana fufua kazi yako katika ya miaka . Hii ndiyo dawa itakayo tuponya UKIRO na kurejea katika uhai wetu wa kwanza na kuviondoa virusi vilivyojingiza ndani ya Kanisa.
Harakati zinazoendelea leo na kuvuma kama nyimbo za Injili na pambio ndani ya ibada, zisipobaki katika mipaka ya neno ambalo ndilo mamlaka ya Imani ya mkristo na kanisa, kwa uhakika tujue hilo ni janga na anguko kubwa ambalo kila mtumishi wa kweli wa Kristo anapaswa kumlilia Bwana, ili liondoke ndani ya kanisa. Ufu 3: 15 – 20 Bwana anasema, anayajua matendo yako, hubaridi wala humoto, umnyonge mwenye mashaka, kipofu na uchi, lakini anashauri ujipatie dawa ya kujipaka macho upate kupona. Kama utaisikia sauti yake atafungua mlango na kula pamoja naye. Ni juu yako kuyapokea maneno haya.
c) TAFAKARI SANA JUU YA IBADA
Ili ibada ya kweli irejeshwe katika kanisa lako na huduma ya kwaya na sifa isiwe chombo cha uharibifu, ni muhimu utafakari na kurudi katika roho na kuacha ushindani wa kisanii uliopo, na kumuomba Mungu akuepushe na mivuto ya mitindo hiyo na akuokoe na anguko hilo. Wito wangu kwa kila mtumishi ni huu, kwamba macho yetu ya kiroho yatiwe nuru na kuona hila za shetani anazozipenyeza kwa siri. Kemea na kuonya juu ya wimbi hili ili kanisa lisitumbukie katika mtego wa shetani, kwa kudhani tunamtumikia Mungu kumbe tayari tunamtumikia shetani.
Mungu wetu ni mwaminifu tukiomba atatusaidia na kuturejesha tena katika huduma yake. Kumbuka Nabii Isaya 57:14-15 Itengenezeni njia, kiondoeni kila kikwazacho katika njia ya watu wangu maana yeye aliye juu aliyetukuka akae milele ambaye jina lake ni Mtakatifu, asema hivi, nakaa mimi mahali palipoinuka palipo patakatifu pamoja na yeye aliye na Roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua Roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu. Kwa moyo huu wa unyenyekevu tukiomba Bwana ataponya kanisa na huduma ya kwaya na sifa. Pia Isaya anasema katika sura ya 55. Ms 6—7. Mtafuteni Bwana ,maadam anapatikana,Mwiteni maadam yu Karibu,Mtu mbaya na aache njia yake Na mtu asiye haki aache mawazo yake,Na amrudie Bwana ,Naye atamrehemu Na arejee kwa Mungu wetu Naye atamsamehe.Mimi nionavyo tunapaswa kuchukua hatua hii ya Nabii Isaya kumtafuta na kumwita Bwana ambaye anapatikana na hayuko mbali bali yuko karibu atatusamehe
SURA YA KUMI NA MBILI
SIKU TEULE YA IBADA TAKATIFU
MWANZO WA SIKU YA BWANA
Wazo la siku ya ibada takatifu ni wazo la Mungu mwenyewe alipomaliza kazi ya uumbaji kwa kilele cha kumuumba mwanadamu siku ya sita, alipumzika siku ya saba na kuitathimini kazi yake na kuona ni kamilifu. Mw 1.31 akasema kila kitu alichokifanya tazama ni chema sana .Kusudi la siku hii ni mapumziko maana hata yeye baada ya kazi hiyo ya uumbaji wa siku sita, siku ya saba,alipumzika akaacha kufanya kazi yote aliokuwa anafanya
Katika hekima Ya Mungu isiyochunguzika aliona upo umuhimu kwa mwanadamu kupumziko baada ya kazi nyingi za siku sita.Jambo hili ni la kawaida kabisa katika mazingira ya mwanadamu ,Mwili, akili na mfumo mzima wa maumbile ya mwanadamu hufika wakati lazima upate nafasi ya kupumzika .Ndiyo maana watu hupenda kutoka nje ya mazingira yao ya kawaida ili waburudishe mwili na akili mbali na shuguli zao za kila siku, huenda ufukweni, hotelini, mbuga za wnyama, na kusafiri nchi za mbali ili wabadilishe hali ya hewa na kupata nguvu kwa kazi zilizoko mbele yao.
Mungu alifululiza kufanya kazi muda wa siku sita, na siku ya saba alipumzika, kupumzika kulikuamo katika ratiba yake haikutokea tu alipanga,Kwahiyo siku ya saba Mungu aliitenga rasmi iwe ya mapumziko kwa mwanadamu ili apate kumwabudu Mungu na kustarehe baada ya kazi ya siku sita amtafakari Mungu na kupumzisha mwili na akili .Mapumziko ni muhimu kama kazi ilivyo muhimu.Siku ya saba imeendelezwa mpaka wakati wa agano jipya baada ya Bwana wetu Yesu kufa na kufufuka siku ya kwanza ya juma. Kanisa na mitume wakaifanya iwe siku ya ibada takatifu kwa Bwana.Luka 24.1—6.
Kabla sijaingia ndani sana kuijadili siku teule ya ibada takatifu ni vema niweke bayana kwamba siku zote ni takatifu mbele za Mungu na mbele zetu kufuatana na Imani yetu kwa Mungu katika neno lake, Lakini ni muhimu iwepo siku maalum ambayo imetengwa kumfanyia Bwana Ibada Takatifu kama kielelezo cha Imani yetu kwake na kuwa ushuhuda kwa ulimwengu kwamba sisi ni MALI yake.Siku sita ni zetu kwa kazi zetu ingawa tunaabudu pia,lakini lazima iwepo siku moja maalum ambayo tumeitoa kumwabudu Mungu kama yeye alivyopumzika siku ya saba akaacha kufanya kazi zake za uumbaji.
Muendelezo wa siku ya Bwana ambayo ni mapumziko hatimaye ikawa ndiyo SABATO ya Kiyahudi kufuatana na sheria za Musa. Mtume Paulo anajadili sana desturi za Kiyahudi yaani torati na sheria za Musa ambazo zilipewa umuhimu kuliko ibada ya kiroho na kusema haifai mtu akajisifu kwa kuishika sabato na sikukuu, na mwandamo wa mwezi kwamba hayo ni kivuli cha mambo halisi yajayo.Kolosai 2.16—23. Paulo hayuko kinyume na sabato wala sheria bali anasema ikiwa vitendo vya sheria vinafanywa kwa jinsi ya mapokeo na desturi pasipo kumkubali Yesu ambaye ni kichwa cha mwili yaani Kanisa ibada hiyo haifai ms 17—19 Na ikiwa madai ya sheria ni kumtawala mtu kwa nguvu ya makatazo na si kutoka ndani ya moyo basi ni bure. Ms 20—21.
Baada ya ufafanuzi huo ,sasa napenda tuiangalie siku hii teule iliyo takatifu kumfanyia Bwana Ibada takatifu.Hebu tungalie maandiko matakatifu
B.SIKUYABWANA. Mw 2.2—3 Kut 20.8—11. Math 12.1—2.
1.Siku ya Bwana ni siku yenye maana kubwa zaidi kuliko ufahamu wetu juu ya siku moja yenye masaa 24 Kwakuwa siku moja kwa Bwana ni miaka 1000 na miaka1000 ni siku moja,Lakini hebu tuiangalie siku hii kama wakati maalum uliotengwa kwa ajili ya ibada ,pia tukitilia maanani ile siku ya ufufuo wa Bwana wetu Yesu Kristo kwamba ni siku ya kwanza ya juma.Wazo la siku ya Bwana tumelipata wakati Mungu alipopumzika siku ya saba kabla ya sheria ya Musa.Neno la Kiebrania SABATON—linalomaanisha Mapumziko ambalo ni SABATO yaani siku takatifu maalum kwa mapumziko na kustarehe kwa kukumbuka kazi alioifanya Mungu siku sita katika kuumba ulimwengu. Ni siku ya kusherehekea ukuu wa Mungu.
Mungu alifanya iwe siku ya ibada na kuabudu na kua na ushirika na Mungu huku tukiacha kazi zote. Hili ni jambo jema maana watu huheshimu sana matukio yao na kuyapa nafasi ya kuyatukuza kama vile , siku ya kuzaliwa ,siku ya uhuru wa nchi yao,siku ya kuhitimu,siku ya ndoa, uzinduzi wa kitu muhimu,.Haya yote yanapewa heshima na wakati ,na siku maalum,Kwahiyo siku ya Ibada ni muhimu kuliko matukio yote ya mwanadamu anayoyapa heshima Siku hiyo ni lazima ipewe uzito maalum kuliko jambo lolote alifanyalo.
SABATO
Kut 16.29 31.12—17. Sabato ni siku ya saba katika kalenda ya Kiyahudi ambayo ni siku ,ya Jumamosi, Siku hii iliwekwa iwe wakfu kwa ajili, ya ibada na kujitoa kwa Mungu peke yake .Ms 23-30 Israeli walikula mikate –mana-huko jangwani ambayo waliruhusiwa kuokota ndani ya siku sita tu na siku ya sita waliokota mikate ya siku ya saba pia, maana siku ya saba ni siku ya utakatifu wa Bwana na sabato ni siku ya starehe na mapumziko.Hawakuruhusiwa kuokota mana katika siku ya saba walipumzika.
Mungu ambaye hana mipaka katika uwezo wa kutenda alijizuia kufanya kazi siku ya saba akapumzika na kustarehe akaacha kufanya kazi ya uumbaji akaitakasa.Ingawa Mungu hana hitaji la mapumziko na starehe maana yeye hachoki wala hafifi ama kuzimia na hahitaji kupumzisha akili zake,alifanya siku hiyo iwepo.
C.JINSI SIKU HIYO ILIVYO ANZA
Mw 2.3 Sabato ,Maana yake ni, Mapumziko yaani KUACHA. Kuacha kufanya kazi ili upumzike,Kupumzika ni mpango uliowekwa na Mungu sambamba na uumbaji alioufanya ndani ya siku sita na siku ya saba ikawa ni mapumziko.Ili Siku hiyo iwe chanzo cha baraka na mafanikio ya mwanadamu, kwa kumfanyia Mungu ibada na kumwabudu.Kut 31. 13—17.Hii inaendana na agizo alilompa Adamu, kwamba miti yote ya bustani anaweza kula bali matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya asile.Mungu aliweka utaratibu huu uwe mwongozo kwa Adamu kufurahia baraka za Mungu katika bustani ya Edeni ili kwa utashi wake amtii Mungu na kuheshimu agizo hilo kwa shukurani na kuendeleza ushirika wao. Mw 2.17
Adhabu ya mtu ambaye alipuuza sabato ilikua ni kifo sawasawa na Adamu kwa kupuza agizo la Mungu kama angekula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya angekufa. Uhai wa mtu ulitegemea kuheshimu agizo la Mungu na kuishika sabato na kuitakasa kila baada ya siku sita na kupumzika.Kama tunavyoona kwa Adamu alipokula alikufa kiroho nakufuatiwa na kifo cha mwili ambacho haikuwa mpango wa Mungu bali mpango wa Mungu ulikua ni kuishi milele.
D. SABATO IKAFANYWA AMRI
Kut 20. 8—12.
Ipo siri kubwa ndani ya moyo wa Mungu kuhusiana na siku ya Bwana kuonyesha umuhimu wa mapumziko, Sabato akaifanya Amri , hii ni amri ya nne katika amri za Mungu. Amri hii ina mkazo ule ule wa kupumzika, kuitakasa na kuacha kufanya kazi.badala yake mtu afanye ibada na kumwabudu Mungu. Ni vema tuelewe kwamba huu ni mkakati wa Mungu kumtaka mwanadamu aabudu.Haileti mantiki jambo zito kama hili liachwe bila kanuni au bila mwongozo,Huu ndio mwongozo yaani hiyo sabato.Sabato humwongoza mwanadamu kwenda katika ibada na Mungu wake kwa kutambua maana ya mapumziko hayo kwamba yanahusu uhusiana wake na Muumba wake.
Amri hii ikazidishwa makali yake kwa kupiga marufuku mwanadamu na mnyama wasifanye kazi siku ya sabato bali iwe ni siku ya kukumbuka neema ya Mungu alivyowakomboa Israeli kutoka katika nchi ya utumwa huko Misri Kut 19.4—6.
E. UMUHIMU WA SIKU YA BWANA KWETU. Math 12. 8
Tumeona tokea mwanzo Mungu ameweka siku moja teule takatifu na kuagiza itakaswe. Yesu mjumbe wa agano jipya ambaye ni Mungu Mwana na mkombozi wa ulimwengu ni BWANA WA SABATO. Ubwana wake anaupata kwa kazi ya ukombozi aliyoifanya pale msalabani. Kazi hii ni kamilifu kabisa katika kumletea mwanadamu Pumziko Halisi Amekamilisha kumpa mwanadamu uhuru wa kweli na kumpumzisha kiroho na kumfungua kutoka katika vifungo vya dhambi,magonjwa na mateso. Lengo la kupumzika ni kupata Raha, Yesu amewapa Raha ya kweli. Mwanadamu si mtumwa wa dhambi tena. Heb 4.3—5, 9—10.Hapa ndipo tunapata maana ya dhana ya sabato kwamba ni pumziko linaloleta raha moyoni mwa mtu aliyekombolewa na Yesu Bwana wa Sabato.
1 Faida za Sabato Kiroho Math 11.28
—-Tunapewa pumziko la Kiroho la Mungu na tunakua makao yake.
—-Mzigo wa dhambi Yesu ameuchukua mioyoni mwetu.
—-Tunapewa amani na Raha na kusamehewa
—-Tunakombolewa kutoka Sheria ya dini ambayo haina nguvu Ya kutuwezesha kuwa huru kiroho na kimwili. 2Faida za Sabato Kimwili Tunapewa uponyaji wa mwili mbali na magonjwa na Nguvu za kumtumikia Mungu kwa siku sita zilizoko mbele ,Tunapokea baraka za mali na ulinzi wa Mungu ,Tunaingia katika ushirika wa kweli na upendo wa dhati kwa , Waamini wenzetu na kutimiza sheria ya Mpende jirani yako Kama nafsi yako. Pumziko hili la Raha ya sabato tunaanza nalo hapa duniani na kutunganisha na Bwana ili mahali alipo nasi tuwepo kiasi kwamba hata mauti haiwezi kututenga naye mpaka mbinguni milele. Ufu 14.13 Yoh 14.1—3.
F. KUISHIKA SABATO NI LAZIMA
Sabato ilikua ni agano la Israeli na Mungu ,Lakini sisi hatuishiki sabato kama amri au sheria bali tunaishika sabato katika kumtii Yesu aliyetuweka huru na kutupa pumziko la kweli mioyoni mwetu kwa msingi wa neema. Kwahiyo ni muhimu kuiheshimu sabato ambayo kwetu ni siku, ya Bwana kwa uzito ule ule uliokuwepo katika sheria ya Musa.Maana sasa sisi tuko chini ya AGANO JIPYA ambalo ni ishara kwamba tu mali ya KRISTO 1PET 2.9-10 Sisi ni mzao mteule ukuhani wa kifalme, taifa takatifu,watu wa milki ya Mungu, kazi yetu ni kutangaza fadhili zake ,ambao hapo kwanza hatukuwa taifa bali sasa ni taifa la Mungu,ambao hatukupata rehema sasa tumepata rehema kwa kazi ya Yesu msalabani kufa na kufufuka kwake tumepumzishwa.
G. SIKU YA BWANNA JUMAPILI
Luka 24, 1—6, Mdo 20. 7, 1Kor 16. 2.l
Siku ya kwanza ya juma ni siku,ya Jumapili katika kalenda ya kiyahudi Siku hii ni siku ambayo Bwana wetu YESU ALIFUFUKA KUTOKA KWA WAFU .Ni siku ya kilele cha kazi ya Yesu ya ukombozi wa mwanadamu ambayo Bwana wa Sabato aliuweka huru ulimwengu mbali na utumwa wa dhambi,Akafufuka toka kwa wafu na kuishinda mauti na dhambi kwa ushindi mkuu.Kufufuka kwa Yesu ni muhimu sana katika kukamilisha kazi ya ukombozi. ,Kama asingefufuka mwanadamu asingewekwa huru na kupata pumziko na raha .Yesu ameitimiliza torati kwa kumpatia mwanadamu pumziko na raha halisi ya kiroho ambayo inadhihirishwa na tendo la nje la Kanisa kusherehekea ushindi wa Yesu kufufuka siku ya kwanza ya juma ambayo ni JUMAPILI
Kutokana na uzito wa kazi hii ambayo imemgarimu Mungu kumrejesha mwanadamu katika pumziko na raha alioikusudia tangu kuumbwa kwake Mw 3,15,Kwa kumtoa Mwana wake wa pekee Yoh 3.16, kutimiza ahadi yake kwa mwanamke kwamba uzao wake utamponda kichwa nyoka [shetani] nakurejesha tena ibada alioipoteza pale EDENI , SASA Yesu amemponda kichwa shetani .Tangu hapo kalenda yetu ya siku ya IBADA iliyo sahihi ni ile ya ufufuo wa YESU.Siku ya JUMAPILI imekuwa ni siku teule Takatifu ya ibada iliyotengwa kumwabudu Mungu kwa kukusanyika pamoja na kuacha kufanya kazi, na kuitakasa, Kwamba mkristo kwa uaminifu wa dhati aiheshimu siku hii teule kwa ibada bila udhuru wowote, isipokuwa kwasababu za kweli na za haki mbele za Mungu kama Yesu anavyobainisha mambo yaliyo halali kufanyika siku ya sabato. Mathayo 12.1–8.
H. SIKU HII HAIJATANGULIWA Math 5.17
Yesu aliiheshimu torati Hakuja kuitangua bali kuitimiliza Torati ilidai maisha ya uadilifu pale amri kumi zinapo sema USIZINI, USIIBE, USIUE, USIIBE, huo ni uadilifu katika mahusiano ya mwanadamu na mwanadamu.
Pia ilidai Usiwe na miungu mingine, Ikumbuke siku ya sabato na kuitakasa, huo ni uadilifu wa kiroho wa mwanadamu kwa Mungu,Madai haya ya torati yanatuhusu sisi leo pia,Tutayatekeleza madai haya kwa kumtii Yesu. Rumi 3, 31 Basi , Je ,Twaibatilisha sheria kwa Imani hiyo Hasha , Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.Imani yetu kwa Yesu inatuwezesha kutekeleza madai ya Torati katika kumtii Rumi 8.2—4. Kwasababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru mbali na sheria ya dhanbi na mauti ,Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwasababu ya mwili ,Mungu , kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwasababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili ili maagizo ya Torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili,bali mambo ya roho .Hoja hizi zina weka wazi kwamba madai ya Torati kuhusu sabato hayajatanguliwa Ila kwamba sisi ndio wadau halisi tutakao itekeleza torati kwa ukamilifu wake wote katika msingi wa agano jipya kwamba siku ya Jumapili ni siku rasmi ya ibada Takatifu kwa Bwana.
I. UTII MKAMILIFU KWA YESU
Kumtii Yesu kwa ukamilifu ndiyo msingi wa kwanza kuyatimiza madai ya Torati maana sisi hatuko chini ya Torati bali tuko chini ya Yesu Kristo.Torati inaagiza usizini, usiibe ,usiue. Hatutayafanya hayo kwa kuitii Torati bali kwa kumtii Yesu.Torati inadai Ikumbuke siku ya Sabato na kuitakasa , Usiwe na miungu mingine Ila Mimi.Basi kwa kumtii Yesu Tutaikumbuka na kuitakasa siku ya sabato na hatutakuwa na miungu mingine.Agano jipya linatia mkazo wala msiache kukusanyika pamoja kama ilivyo kawaida ya watu wengine. Kwa kumtii Yesu hatutaacha kufika katika makusanyiko ya ibada hayo hususani Jumapili kumwabudu Mungu Waeb 10.25. Hakuna sababu inayokubalika usiwepo katika siku ya ibada mbali na yale ambayo Yesu ameyasema katika Math 12; 2—3.
J. JUMAPILI NI SIKU YA UTAKATIFU WA BWANA
Isaya 58. 13—14.
Isaya anaielezea siku ya Bwana kwa undani sana kama ifuatavyo.
Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato ,usifanya anasa yako siku ya utakatifu wangu , ukiita sabato siku ya furaha,na siku takatifu ya Bwana yenye heshima , ukiitukuza kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe,wala kuyatafuta yakupendezayo,wala kusema maneno yako mwenyewe, Ndipo utakapojifurahisha katika Bwana,nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka,nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako,kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.Hivi ndivyo Bwana anavyoiheshimu siku yake Takatifu.Jumapili ni siku ya utakatifu wa Bwana yaani siku, ya saba alioitenga rasmi kwa ajili ,yake mwenyewe ,Kila mkristo anatakiwa kujitoa mzima mzima kwa mawazo,,maneno, akili, na matendo kupumzika ili aweze kufanywa upya na kurejesha nguvu za kiroho na kimwili apate kumtumikia Bwana kwa ukamilifu kwa siku zilizo mbele yake.
Angalia Nabii Isaya anavyosema,
1 Usigeuze mguu wako ukaihalifu sabato yaani kutopumzika na kwenda kwingineko.SIKU HIYO NI SIKU YA KUKAA MBELA ZA BWANA .
2 Usifanye anasa siku ya utakatifu wangu yaani ujitenge na Kila kitu chenye manufaa kwako kinachostarehesha mwili, roho, yako bali uitakase siku hiyo na kustarehe mbele za Bwana tu.
3. Uite sabato siku ya furaha na siku takatifu ya Bwana yenye heshima, yaani ujiandae kuabudu katika moyo wa utakatifu.
4. Itukuze kwa kutofanya mambo yanayokupendezesha yaani simamisha miradi na mambo yako yote utawaliwe na ibada na kuweka kando kila kitu
5. Usiseme maneno yako bali ujae sifa kinywani mwako na kufunikwa na Roho Mtakatifu.
6.Bwana atakupandisha na kukuinua mahali pa juu katika nchi kama Danieli, Shadraka, Meshaki, na Abednego walipokuwa Babeli walifanywa wakuu katika ufalme huo. Bila shaka ukimwinua Mungu naye atakuinua.
7. Atakulisha urithi wa Yakobo yaani utahesabiwa miongoni mwa waliobarikiwa na Bwana Mungu wa Israeli na kupewa baraka za Ibrahimu mbarikiwa.Siku hii inaambatana na baraka nyingi kwa ajili yako.
K. MADHARA YA KUTOJALI IBADA SIKU YA BWANA
Yapo matokeo mabaya kwa mkristo asiyejali ibada siku ya Bwana
Tafakari kwa makini mambo yafuatayo .
A. Atamfanyia dhambi Mungu kwa kutomtii katika neno.Haya ni madhara kwa upande wa kiroho.
B. Atakwenda kinyume na kanuni ya uumbaji wa Mungu ina yomtaka apumzike.Haya ni madhara kwa upande wa afya ya mwili.
C. Hukumu ya Mungu itamwangukia maana ni muasi.Haya ni madhara ya mahusiano yanayopelekea hatari kubwa ya kupoteza uzima wa milele.
D. Magonjwa na udhaifu wa mwili na roho vitampata na kuwa maskini kiroho na kimwili
E. Atakosa ushirika wake na Mungu na kutengwa na ushirika wa watakatifu na Kanisa.
F. Atauchafua ushuhuda wake mbele ya ulimwengu kwa kuonyesha roho ya ukaidi kwa Yesu na kulinajisi Kanisa la Mungu.
G. Atakengeuka na kwenda mbali na neema na kuanguka.Hii ni hatari sana kwa mtu kuikosa neema ya Mungu.
Tunahitaji badiliko la haraka tumtii Bwana katika uaminifu wote na kuifanya Ibada katika siku ya Bwana kama alivyo kusudia katika hekima yake ya kiungu,Bila shaka tutapokea baraka zake,Hivyo basi kila mwenye kujua kutenda mema asiyatende kwake huyo ni dhambi . Ni ombi langu asiwepo mtu atakaye tumbukia katika dhambi hii, Mungu atusaidie.
KILA MWENYE PUMZI NA AMSIFU MUNGU
SURA YA KUMI NA TATU
A] NYIMBO
B] ZABURI
A] Ningependa usome nyimbo hizi kwa kutafakari kama sehemu yako ya Ibada japokuwa badhi yake huzijui,lakini utabarikiwa nazo.
USICHEZE NA DHAMBI
1. Neema imefunuliwa,
Neema yake Bwana Yesu,
Neema kutoka mbinguni
Neema ni kwa ajili yako x2
Yatufundisha kuacha mabaya,
Na kujikana mambo ya dunia
Na kukata maisha ya dhambi,
Na kuziacha anasa za nchi x2
Neema Neema Neema
Neema yake Mungu wetu
Usicheze na dhambi
Itakuangamiza x2 kabisa 3
2. Watu wamejisahau,
Wamekinai maisha,
Yote kwao ni sawa
Mema na mabaya hawaoni,
Yote kwao ni sawa ,
Wanajiliwaza Mungu ni Upendo Hawezi kuchoma wanadamu motoni, Kwani ametuumba tuwe na furaha, Fahari ya nchi ni kwa ajili yetu, Ole Ole Ole kwa wanadamu, Usicheze na dhambi Itakuangamiza kabisa x3
SIJAONA KAMA YESU
1. Nitendeje kumtendea Bwana,
Kwa fadhili na Pendo lake kwangu
Aliyoyafanya kwangu ni mambo makuu,
Kweli mimi sikustahili
Alivyonitoa katika giza nene,
Giza la dhambi Yesu akaniokoa
Sitasahau muujiza wa wokovu,
Wokovu wangu muujiza kila siku
Sijaona kama Yesu sijaona
2. Najimimina kama hivi nilivyo,
Sitabakiza lolote ndani yangu
Wewe ni Bwana na mtawala wangu,
Sema na mimi nitakusikiliza
Muda mwingi nilioupoteza,
Wanihimiza kutumika kwa nguvu
Sitaogopa mabaya yakifika,
Nitasimama maana wewe ni Bwana
Sijaona kama Yesu
KITAMBO KIDOGO
1. Ni kitambo kidogo sana maisha yadumu,
Mwanadamu hana maisha yaliyo marefu
Kwa kitambo kidogo sana maisha yapita,
Yanakwenda kwa kasi sana ni kama upepo
Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke,
Siku za kuishi si nyingi na hujaa taabu
Huchanua kama maua na kisha hukatwa,
Hukimbia kama kivuli na hakai kamwe
2. Uhai wako ulionao watoka kwa Mungu,
Kutoka huko utatwaliwa umrudie
Wala huwezi kuikata sauti yake,
Ikuitapo ee mwanadamu utaondoka
Hekima yote ya mwanadamu hufikia mwisho,
Anapoona mauti yake yeye hunyamaza
Ingawa yeye angelipenda kuishi milele,
Uhai wake si mali yake bali ni wa Mungu
Ukumbuke Ukumbuke Ukumbuke
Maisha yako ni mafupi sana x2
Maisha ya dunia unayofurahia,
yasikudanganye moyoni na kumsahau Mungu
Fahari ya dunia unayofurahia,
Ni furaha ya kitambo lakini milele uchungu
Ujirekebishe na kutengeneza moyo,
Ujisahihishe na kumrudia Mungu
Tubia maovu na kuomba msamaha,
kabla haijakujia siku mbaya
NINAMPENDA YESU
1. Ninampenda Yesu Mwana,
wake Mungu aliyenifia pale msalabani
Kwa damu yake Yesu iliyo ya thamani,
alinikomboa kutoka dhambini
Ninampenda x2 Yeesu
Moyoni mwangu sina mwingine teena
Alitoka mbinguni kuja duniani,
Kutoka duniani kaenda msalabani
Kutoka msalabani kaenda kaburini,
Kutoka kaburini alikwenda kuzimu
Alipofika huko akamkuta shetani,
Amebeba funguo za kifo na mauti
Akamvua enzi na mamlaka yote,
Akatwaa funguo za kifo na mauti
2. Kisha akafufuka kutoka mautini,
kwa muujiza mkuu alipaa mbinguni
Akaiwakilisha damu ya ukombozi,
Mbele ya madhabahu ya
Mungu baba yake
Akaketi mkono wa kuume wa Mungu Baba,
Katika kiti kile cha enzi na utukufu
Ameniweka huru na kongwa la shetani,
Naburudika sana ndani ya Bwana Yesu
Giza limeondoka naona nuru mpya,
Uvuli wa mauti umekwisha toweka
Matumaini mapya ninayo moyoni mwangu,
Sitachukua tena laana ya dhambi Zangu
Naburudika sana ndani ya Bwana Yesu
Yesu aameshinda pale msalabani x2
Naona mapambazuko ya jua la mwokozi
Likiuangaza ulimwengu wote.
EE MUNGU BABA NINAKUPENDA
1. Ee Mungu baba yangu, Ninakupenda sana,
Wewe ulinipenda, Kwa upendo mkubwa
Hata ukamtoa Yesu msalabani,
Nikikumbuka yote uliyonitendea,
Lugha ya shukrani kwako inanishinda
Mimi ni kama nani mbele zako Jehova
Hata unanihesabu kati ya viumbe
Utoshelevu wangu hutoka kwa Baba wa mianga
Wala kwake hakuna kigeugeu cha uongo
Hupendelei mtu, hubagui unatufadhili
Wanyenyekevu wakujiao unawarehemu
Nifanye nini ili nilipe deni la upendo
Sitaliweza bali mimi najitoa mwenyewe
2. Ninapokutafakari sana moyoni mwangu
Ninasikia uwepo wako wanizunguka
Hapo ninakutamnani ningekuona uso
Ili nishibe upendo wako, ee Mungu baba
Fadhili zako naziona katika maisha yangu
Hakika unanijali na tena wanitunza
Tokea utoto wangu mpaka leo wanilinda
Niko mikononi mwako mwamba wangu salama
Utoshelevu wangu hutoka kwa Baba wa mianga
Wala kwako hakuna kigeugeu cha uongo
Ee Mungu wangu wewe si mtu hata udanganye
Umekamilika hujaribiwi uu Mtakatifu
Miungu yote ya ulimwengu na itokomee
Yehovayire Mungu wa kweli ni Mungu wangu
MITAA YA DUNIA
Tangu Yesu aliponiokoa nimekuwa mtumwa wa haki
Minyororo ya mwovu shetani Bwana Yesu akanifunguax2
Sijaona mwokozi aliye kama Yesu Awezaye kutenda
miujiza na kuokoa
Jina langu akaliandika katika kitabu cha uzima
Kwa kalamu ya damu yake Ili lisifutwe milele
Anayalinda maisha yangu Na kuniongoza
Malaika hufanya kituo Nyumbani kwangu
Ninaona mbingu imeshushwa Moyoni mwangu
Mungu Baba Mwana Roho Wanaishi moyoni mwangu x2
Oh Haleluya nimeokoka
Tazameni ya kale yote sasa yameshapita
Ninakiri ninakiri ninakiri ushindi x2
Japokuwa naishi duniani mimi Moyoni naishi mbinguni x2
Natembea mitaa ya dunia mimi Moyoni naishi mbinguni
Duniani misukosuko mingi ipo Moyoni ninayo amani
Ninakiri ninakiri ninakiri ushindix2
Nimeketi pamoja naye Yesu Katika makao ya mbinguni
Bwana ndiwe nguvu yangu Furaha na wokovu mkuu
Nitashikamana nawe Mpaka mwisho wa safari
PELELEZA NDANI YANGU
Peleleza ndani yangu, iwe safi nia Kwangu kama kwako Mungu Idhihiri pia
Peleleza moyo wangu, UnifunulieYaliyomo ndani yangu Nami niyajue
Kwanza washe zako tambi Kumefunga giza, Nijue ambavyo dhambi ni la kuchukiza
Peleleza na mawazo, ni mbegu za mambo Asili ya machukizo Maumbuo umbo
Zidi kuyapelezaKatikati yangu Hata wishe nifundisha Udhaifu wangu
Hapo nikikwinamia Mbele zako, Mungu Hakika nitakujua U mpenzi wangu
TAFUTA DAIMA UTAKATIFU
Tafuta daima utakatifu Fanya urafiki na Wakristo tu Nena siku zote na Bwana wako
Baraka uombe kwa kila jambo
Tafuta daima utakatifu,Uwe peke yako ukimwabudu Ukimwangalia mwokozi wako
Utabadilishwa kama alivyo
Tafuta daima utakatifu,Kiongozi wako awe Yesu tu, Katika furaha au huzuni
Dumu kumfuata Yesu mwokozi
Tafuta daima utakatifu,Umtwaze Roho moyoni mwako ,Akikuongoza katika haki
Hufanywa tayari kwa kazi yake
NITWAE HIVI NILIVYO
Nitwae hivi nilivyo, Umemwaga damu yako Nawe ulivyoniita Bwana Yesu naja
Hivi nilivyo, si langu Kujiosha roho yangu Nisamehe dhambi zangu Bwana Yesu naja
Hivi nilivyo, sioni Kamwe furaha moyoni Daima ni mashakani Bwana Yesu naja
Hivi nilivyo kipofu, Maskini na mpungufu Wewe u mtimilifu Bwana Yesu naja
Naa hivi utanitwaa Nisisubutu kukawa Na wewe hutanikataa Bwana Yesu na
Hivi nilivyo, mapenzi Yamenipa njia wazi Hali na mali sisazi Bwana Yesu naja
BABA, MWANA, ROHO
Baba, Mwana, Roho, Mungu mwenye enzi, Kila tukiamka tunakuabudu Baba, Mwana, Roho,
Mungu wa mapenzi Ewe Utatu, tunakusifu
Baba, Mwana, Roho, wakuaminio Wanakutolea shukurani zaoWakusujudia Malaika nao
Wewe u mwanzo, nawe u mwisho
Baba, Mwana, Roho, sisi tu gizani,Utukufu wako haoni mkosa,U Mtakatifu, nawe u mapenzi
U peke yako, mwenzio huna
Baba, Mwana, Roho, Mungu mwenye enzi,Ulivyoviumba vyote vyakusifu Baba, Mwana, Roho,
Mungu wa mapenzi Ewe Utatu, tunakusifu
BARAGUMU YAKE BWANA
Baragumu yake Bwana wakati ikipigwa,Na siku ya milele ikafika Hapo waliokombolewa
watakusanyika, Nitakuwako, jina kuitika
Na majina yaitwapo Na majina yaitwapo Na majina yaitwapo
Kuitika jina, nitakuwepo.
Wafu wa Kristo wafufukapo kwa siku ile, Tutashiriki na fahari yake , Waliochaguliwa
watakaribishwa kwake Nitakuwapo jina kuitika
Saa zote na tumfanyie Bwana kazi yake, Tangu asubuhi hata jioni Maisha yetu ikomapo
humu duniani Nitakuwako jina
PANDA ASUBUHI
Panda asubuhi mbegu ya fadhili,Panda adhuhuri, tena jioni,
Tutaingojea siku ya mavuno Tutafurahi kuleta mavuno
Leta mavuno, leta mavuno Tutafurahi kuleta mavuno
Leta mavuno, leta mavuno Tutafufahi kuleta mavuno
Na panda mwangani, tena kivuliniUsiwe na hofu kwa baridi mkuu
Na mwisho wa kazi kuvuna mavuno Tutafurahi kuleta mavuno.
Mvunieni Bwana kwa machozi mengi, Ijapo twaona taabu nyingi
Mwisho wa kilio tutakaribishwa, Tutafurahi kuleta mavuno.
B] ZABURI 71:
Nimekukimbilia wewe Bwana nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe, unitegee sikio lako, uniokoe.
Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu nitakakokwenda siku zote,
Umeamuru niokolewe, ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi
Katika mkono wake mwovu, mdhalimu.
Maana ndiwe faraja langu, Ee Bwana Mungu
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea wewe tangu kuzaliwa
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu
Ninakusifu wewe daima.
Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi, na wewe ndiwe kimbilio
Langu la nguvu.
Kinywa changu kitajazwa sifa zako, na heshima yako mchana kutwa
Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache.
Kwa maana adui zangu wananiambia, nao wanaoniotea roho yangu hushauriana.
Wakisema Mungu umemwacha mfuateni, mkamateni, hakuna wa kumponya.
Ee Mungu usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.
Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu
Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.
Nami nitatumaini daima, nitazidi kuongeza sifa zake zote,
Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako
Mchana kutwa maana sijui hesabu yake.
Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana Mungu
Nitawakumbusha watu haki yako wewe peke yako.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.
Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu usiniache
Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako
Na kila atakayekuja uweza wako.
Na haki yako, Ee Mungu, imefika juu sana
Wewe uliyefanya mambo makuu, Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?.
Wewe uliyetuonyesha mateso mengi, mabaya, utatuhuisha tena
Utatupandisha juu tena, tokea pande za chini ya nchi.
Laiti ungeniongezea ukuu,Urejee tena na kunifariji moyo.
Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu,
Nitakuimbia wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli.Midomo yangu itafurahi sana nukuimbiapo, na nafsi yangu uliyoikomboa.Ulimi wangu nao utasimulia, haki yako mchana kutwa.Kwa maana wameaibishwa, wametahayarika, wanaonitakia mabaya.
ZABURI 136
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Mshukuruni Mungu wa miungu, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Mshukuruni Bwana wa Mabwana, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye peke yake afanya maajabu makuu, kwa maana fadhili zake ni za milele
Yeye aliyefanya mbingi kwa fahamu zake, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji, kwa maanafadhili zake ni za milele.
Yeye aliyefanya mianga mikubwa, kwa maana fadhili zake ni za milele
Jua litawale mchana, kwa maana fadhili zake ni za milele
Mwezi na nyota zitawale usiku, kwa maana fadhili zake ni za milele
Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao
kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akawatoa Waisraeli katikati yao, kwa maana fadhili zake ni za milele
Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akawavusha Israeli, katikati yake, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akamwangusha Farao na jeshi lake katika bahari ya Shamu,
kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyewaongoza watu wake jangwani, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyewapiga wafalme wakuu, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akawaua wafalme mashuhuri, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Sihoni, mfalme wa Waamori, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Na Ogu, mfalme wa Bashani, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akaitoa nchi yao iwe urithi, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Urithi wa Israeli mtumishi wake, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Aliyetukumbuka katika unyonge wetu, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akatuokoa na watesi wetu, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Kila chenye mwili akipa chakula chake, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Mshukuruni Mungu wa mbingu, kwa maana fadhili zake ni za milele.
VITABU REJEA
(Reference Books)